Matangazo

📢 IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA — KARIBU KWENYE BLOG RASMI   ✦   📰 UHAMIAJI HABARI BLOGU — TUNAKULETEA MATUKIO KILA SIKU   ✦   📲 FUATA IDARA YETU KATIKA MITANDAO YA KIJAMII   ✦   ✉️ WASILIANA NASI: info@immigration.go.tz   ✦   ☎️ +255-22-2850575/6

21 Novemba 2017

KAMISHNA JENERALI WA UHAMIAJI ATEMA ‘CHECHE’ KATIKA UZINDUZI WA ZOEZI LA UANDIKISHWAJI VITAMBULISHO VYA TAIFA,

Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna P. Makakala amemuagiza Afisa Uhamiaji Mkoa wa Mara kushirikiana kwa karibu zaidi na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ili kuhakikisha wanaopatiwa Vitambulisho vya Taifa ni raia wa Tanzania, wageni wanaoishi nchini kihalali (wakaazi) na wakimbizi. 

Akiongea katika uzinduzi wa zoezi hilo kwa mkoa wa Mara ambapo mgeni rasmi alikuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mheshimiwa Hamad Masauni, Dkt. Makakala pia aliwataka wananchi wa mkoa wa Mara kuwa wazalendo kwa kuwafichua wahamiaji haramu watakaojaribu kujiandikisha kwa ajili ya kupatiwa vitambulisho vya Taifa.

“Nimemuagiza Afisa Uhamiaji Mkoa wa Mara pamoja na mikoa mingine nchini kushirikiana kwa karibu na mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa kwenye zoezi la uandikishwaji ili kuhakikisha kuwa wanaopatiwa vitambulisho vya Taifa ni wale wanaostahili tu, pia nawaomba nanyi wananchi mjitokeze kuwafichua wahamiaji haramu ambao watajitokeza kuomba vitambulisho, toeni taarifa kwa Uhamiaji, NIDA na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi yao. Nawatahadharisha wahamiaji haramu na wengine wasiostahili kutojihusisha na zoezi hili kwani kufanya hivyo ni kinyume na sheria” Alisisitiza Kamishna Jenerali.

Uzinduzi huo ambao ulifanyika katika Viwanja Vya Mendoza Musoma Mjini siku ya tarehe 19 Novemba ulihudhuriwa na Naibu waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mheshimiwa Hamad Masauni, Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Adam Malima ambaye ndiye mratibu wa zoezi hilo katika mkoa wake, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama Mkoa, Kaimu Mkurugenzi wa RITA Bi.  Emmy Hudson na Maafisa waandamizi toka NIDA.  

Kadhalika NIDA inakusudia kutoa vitambulisho vya aina tatu ambavyo ni vya raia wa Tanzania, Wageni wakaazi na wakimbizi. Zoezi hili halitawahusu wahamiaji haramu na walowezi.


Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala akiwahutubia wananchi waliohudhuria katika Uzinduzi wa Zoezi la Uandikishwaji wa Vitambulisho vya Taifa wilayani Tarime mkoa wa Mara. 
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mheshimiwa Hamad Masauni akizindua zoezi la uandikishwaji

Dkt. Anna Makakala akifuatilia hotuba ya Mheshimiwa Naibu Waziri katika uzinduzi wa zoezi hilo jana

Afisa Uhamiaji akielezea namna ya uingizaji wa taarifa na utoaji wa vitambulisho unavyofanyika

20 Novemba 2017

UHAMIAJI YAFUNGA 'MITAMBO' YA UTAMBUZI KATIKA UWANJA WA NDEGE WA KIMATAIFA WA MWALIMU JULIUS NYERERE


Idara ya Uhamiaji katika Kituo cha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) imefunga Vifaa vyenye mfumo mpya wa utambuzi na ulinganisho wa sura (Facial Recognition and Matching System) kwa abiria wanaoingia nchini.

Akiongea baada ya kupokea vifaa hivyo, Kamishna wa Uhamiaji anayesimamia Divisheni ya Usimamizi na Udhibiti wa Mipaka Samwel Rhobby Magweiga, amesema kuwa huo ni muendelezo wa mikakati ya Idara katika kuimarisha na kuhuisha KANZIDATA ya wanaoingia nchini.

“Vifaa na mfumo huu utasaidia sana katika kukusanya taarifa za abiria wote wanaoingia nchini kupitia hapa (JNIA), kama mlivyofahamishwa, mfumo huu unachukua sura ya mtu na kulinganisha na sura nyingine zilizomo kwenye kanzidata ili kuhakikisha taarifa zilizo kwenye pasipoti yake ni za pekee na hakuna mtu mwenye sura kama yake au mtu mwenye sura ingine kuwa na taarifa kama zake.”Alieleza Kamishna Samwel Magweiga.

Awali wakati akabidhiana vifaa hivyo, Mwakilishi mkazi wa Shirika la Uhamiaji la Kimataifa (IOM) Dr. Qasim Sufi alisema kwamba IOM itashirikiana na Idara ya Uhamiaji katika suala zima la udhibiti wa uingiaji na utokaji wa raia na wageni.

Idara ya Uhamiaji kwa kushirikiana na shirika hilo, wamefunga vifaa vingine vyenye mfumo huo kwenye vituo vya Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA) pamoja na mpaka wa Holili kwa pande zote mbili za Tanzania na Kenya.

Kupitia ushirikiano huo na IOM, Idara ya Uhamiaji itaendelea kuimarisha maeneo yote ya mipaka kwa kufunga vifaa na mfumo huu wa kisasa zaidi kutumiwa hapa Afrika Mashariki.

Dr. Qasim Sufi Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji akifanyiwa majaribio katika mfumo wa utambuzi wa sura (Facial Recognition and matching system) katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es salaam

Kamishna wa Uhamiaji (Usimamizi na Udhibiti wa Mipaka) Samwl Magweiga (wa kwanza kulia) akisikiliza kwa makini namna mfumo huo unavyofanya kazi wakati wa ufungaji wa vifaa vyenye mfumo huo.


Nelson Gonzales (aliyeshika pasipoti) akielezea namna mfumo huo unavyofanya kazi Kamishna na Maafisa Uhamiaji wa Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere.







Kamishna Wa Uhamiaji (Usimamizi na Udhibiti wa Mipaka) akieleza kuridhishwa na namna vifaa na mfumo huo unavyofanya kazi ya utambuzi na ulinganishi wa sura na taarifa za abiria wanaoingia nchini



Kamishna wa Uhamiaji (Usimamizi na Udhibiti wa Mipaka) akikabidhiwa nyaraka za mfumo huo na Mwakilishi Mkazi wa IOM Dr. Qasim Sufi mara baada ya ufungaji wa vifaa hivyo.


10 Novemba 2017

IDARA YA UHAMIAJI YAPOKEA UJUMBE 'MZITO' KUTOKA JUMUIYA ZA KIMATAIFA

Idara ya Uhamiaji imepokea ujumbe wa Maafisa kumi na tisa (19) toka nchini Ivory Coast na Niger. Maafisa hao ambao ni viongozi waandamizi wa Serikali, Shirika la Uhamiaji la Kimataifa (IOM), Mashirika ya Kimataifa ya Kikanda ya AU, UEMOA na ECOWAS walifanya ziara ili kubadilishana uzoefu wa utendaji kazi baina ya mataifa hayo ya Afrika Magharibi na Tanzania.

Mwenyeji wao Kaimu Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Kamishna Hannelore Manyanga alipokea ujumbe huo katika Makao Makuu ya Uhamiaji Kurasini jijini Dar es Salaam, ambapo baada ya kusalimiana na kuingia ukumbi wa mikutano,  wajumbe hao walipata maelezo mbalimbali ya Huduma zinazotolewa na Idara ya Uhamiaji. 

Pia wajumbe hao walipata fursa ya kujifunza kuhusu taratibu za Uingiaji na Utokaji nchini, mifumo ya utambuzi na taarifa za wasafiri pamoja na masuala ya udhibiti na usimamizi wa mipaka.

Kiongozi wa ujumbe huo Bwana Ouba Ibrahim kutoka nchini Niger alimshukuru Kaimu Kamishna Jenerali kwa mapokezi mazuri na mkutano uliokuwa na lengo la kubadilishana uzoefu wa utendaji kazi kati ya Uhamiaji Tanzania na idara za uhamiaji, polisi na forodha  za nchi za Niger na Ivory Coast. 



Afisa TEHAMA, Sajini  wa Uhamiaji,Philip Masilingi  akiwasilisha andiko kuhusu Utendaji wa Mfumo wa kutambua na kuhifadhi taarifa za wasafiri mbele ya wajumbe wa Shirika la Uhamiaji wa Kimataifa, IOM kutoka nchi za Ivory Coast na Niger. Wajumbe hao ni pamoja na Maafisa Uhamiaji, Polisi na Forodha. 

Mkaguzi Msaidizi wa Uhamiaji, Godbless Swai akiwasilisha andiko kuhusu taratibu za uingiaji  na ukaazi nchini na kwa jumbe huo. 

Mkaguzi Msaidizi wa Uhamiaji, Omary Othman akiwasilisha andiko kuhusu udhibiti na usimamizi wa miopaka nchini kwa jumbe huo. 
Afisa kutoka Shirika la IOM nchini Bwana Marcellino Ramkishun akichangia mada katika Kikao cha Idara ya Uhamiaji na Ujumbe uliongozwa na Shirika lake.
Kaimu Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Kamishna Hannelore Morgan Manyanga mwenye Uniform katika akiwa katika picha ya pamoja na wageni wa IOM waliotembembelea Makao ya Makuu ya Uhamiaji kwa ziara ya Mafunzo


Kaimu Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Kamishna Hannelore Morgan Manyanga akiagana na Ouba Ibrahim kutoka Niger ambaye ni mmoja wa wajumbe waliotembembelea Makao ya Makuu ya Uhamiaji kwa ziara ya Mafunzo, kuria kwake ni Msemaji Mkuu wa Idara ya Uhamiaji, Mrakibu Ally Mohamed Mtanda  


08 Novemba 2017

Mwananchi onesha Uzalendo wako


"Mwananchi onesha Uzalendo kwa nchi yako, saidia Idara ya Uhamiaji kwa kufichua Wahamiaji Haramu" - Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dr. Anna P. Makakala

03 Novemba 2017

JUMLA YA MAAFISA UHAMIAJI 15 WAAGWA LEO KUELEKEA CHINA

Jumla ya Maafisa Uhamiaji 15 wameagwa leo jijini Dar es salaam tayari kwa safari kuelekea nchini China kwa ajili ya mafunzo ya wiki mbili.

Hafla hiyo fupi iliyofanyika Makao Makuu ya Uhamiaji Kurasini wilaya ya Temeke iliwakutanisha maafisa uhamiaji kutoa maeneo mbalimbali nchini ambao wanasafiri mwisho wa wiki hii.

Kaimu Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Hannelore Manyanga aliwatakia safari njema maafisa hao na kuwasisitiza kuzingatia mafunzo watakayopewa ili waje kutumia ujuzi watakaoupata kwa ajili ya maendeleo ya Idara.


Maafisa hao wanategemea kuondoka nchini mwishoni mwa wiki kuelekea jijini ShangChuan. 



Maafisa Uhamiaji wanaosafiri mwishoni mwa wiki kuelekea nchini China wakiwa katika picha ya pamoja

Kaimu Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Hannelore Manyanga (aliyekaa) katika picha ya pamoja na 'wasafiri'

Kiongozi wa Msafara, Mrakibu Mwandamizi wa Uhamiaji Mariam Mwanzalima akitoa neno la shukrani kwa niaba ya 'wasafiri'