Matangazo

📢 IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA — KARIBU KWENYE BLOG RASMI   ✦   📰 UHAMIAJI HABARI BLOGU — TUNAKULETEA MATUKIO KILA SIKU   ✦   📲 FUATA IDARA YETU KATIKA MITANDAO YA KIJAMII   ✦   ✉️ WASILIANA NASI: info@immigration.go.tz   ✦   ☎️ +255-22-2850575/6

14 Desemba 2017

MHESHIMIWA RAIS NA AMIRI JESHI MKUU AKABIDHI NYUMBA 63 ZA UHAMIAJI KATIKA ENEO LA IYUMBU, DODOMA.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amemkabidhi Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna P. Makakala nyumba mpya 63 zenye thamani ya zaidi ya Sh. Bilioni 3 zilizonunuliwa toka Shirika la Nyumba la Taifa, NHC jana eneo la Iyumbu, Manispaa ya Dodoma.

Nyumba hizi 63 zilizokamilika ni za  Awamu ya Kwanza ya Mradi mkubwa unaogharamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ujenzi wake kutekelezwa na Shirika la Wazalendo la NHC, ambapo matarajio ya Mradi ni kujenga nyumba 150 ambazo zitagawiwa kwa Taasisi mbalimbali za Serikali zilizoko Makao Makuu ya Serikali, Mjini Dodoma.  

Aidha, nyumba 63 alizozipokea Kamishna Jenerali ni sehemu ya nyumba 103 ambazo Idara ya Uhamiaji imetengewa toka Mradi huo ambapo ujenzi wa nyumba 47 zilizobaki utafanywa kipindi cha Awamu ya pili ya Mradi unaotegemewa kukamilika ifikapo Mwezi Mei 2018.

"Kwa kweli Uhamiaji mnafanya kazi kubwa sana, sio kama zamani. Naona kila mara mmekamata wahamiaji haramu. Hata sasa nina taarifa kuwa maafisa uhamiaji pale Airport wamesaidia kukamata dola milioni moja zilizokuwa zinaingizwa nchini kinyume cha sheria. Hongera sana mama, pia naomba ufikishe salamu zangu kwa Maafisa Uhamiaji wote, nafurahi sana kwenye utendaji kazi wenu.  Ndio maana nimewapa hizi nyumba ili mfanye kazi kwa bidiii."  alisema Mheshimiwa Rais.

Akipokea nyumba hizo Kamishna Jenerali wa Uhamiaji amemshukuru Amiri Jeshi Mkuu na kuahidi kuwa Idara inakusudia kuhamia Dodoma haraka iwezekanavyo na kwamba  nyumba hizo zitasaidia kutatua tatizo la Makazi ya Maafisa na Askari watakaohamia Makao Makuu Dodoma.

“Idadi ya Maafisa, Askari na Watumishi raia wa Uhamiaji wanaotarajiwa kuhamia Makao Makuu ya Serikali mjini Dodoma ni 300, hivyo upatikanaji wa nyumba hizi utasaidia kuwapatia makazi bora watumishi hao watakaohamia Dodoma pamoja na kupunguza changamoto ya nyumba ya makazi” alisema Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna P. Makakala.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba alimshukuru na kumpongeza Rais Magufuli kwa hatua anazochukua katika kutatua changamoto mbalimbali serikalini ambapo ameongeza ari kwa watumishi na tija katika uwajibikaji hususani kwa Idara ya Uhamiaji.

“Uzinduzi wa nyumba za makazi katika eneo hili la Iyumbu ni hatua muhimu na inayostahili pongezi kwani ni sehemu ya uboreshaji wa makazi kwa watumishi. Ni Imani yangu kuwa, nyumba hizi zitatatua changamoto ya makazi kwa maafisa na askari wa Jeshi la Uhamiaji. Pia zitasaidia kuongeza ari mpya kwani makazi haya yatawezesha kufanya kazi kwa ufanisi na hivyo kutekeleza kauli mbiu ya HAPA KAZI TU.”  Aliongeza Waziri Mwigulu.

Kadhalika, hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Mej. Jenerali Projest Rwegasira, Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Nyumba la Taifa Bi. Blandina Salome Joseph Nyoni, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Nyumba la Taifa Ndugu Nehemiah Mchechu, Viongozi mbalimbali wa Taasisi za Serikali, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama na Viongozi kutoka Sekta Binafsi.




Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli akisalimiana na Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala kabla ya tukio la kukabidhi nyumba 63 kwa Idara ya Uhamiaji eneo la Iyumbu Manispaa ya Dodoma siku ya tarehe 13 Disemba 2017.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai  na Kamishna Jenerali wa Uhamiaji  wakiwa kwenye tukio la kukabidhi nyumba 63 za Uhamiaji eneo la Iyumbu-Dodoma.
Kamishna wa Uhamiaji-Utawala na Fedha akifuatilia kwa makini tukio la kukabidhi nyumba 63 kwa Idara ya Uhamiaji

Afisa Uhamiaji Mkoa wa Dodoma DCI. Peter Kundy akisalimiana na Mkurugenzi wa NHC Bw. Nehemiah Mchechu kabla ya tukio la Rais kukabidhi nyumba 63 za Uhamiaji.
Maafisa Uhamiaji wakifuatilia tukio la kukabidhiwa nyumba 63 kwa Idara ya Uhamiaji 
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Afisa wa NHC na Afisa Uhamiaji Mkoa wa Dodoma wakielekea eneo la tukio

Kamishna wa Uhamiaji-Utawala na Fedha (kulia) Edward Chogero akifuatilia tukio la makabidhiano ya nyumba 63 Iyumbu Dodoma, kulia kwake ni Afisa Uhamiaji Mkoa wa Dodoma DCI. Peter Kundy.
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji akisalimiana na Mkurugenzi Mkuu wa NHC kabla ya shughuli ya Rais kukabidhi nyumba 63 za Uhamiaji eneo la Iyumbu Manispaa ya Dodoma.
Maafisa Uhamiaji wakifurahia jambo wakati wa hotuba ya Mheshimiwa Rais katika eneo la Iyumbu Manispaa ya Dodoma
Kamishna wa Uhamiaji-Utawala na Fedha Peter Chogero akiongea na Afisa kutoka NHC kabla ya tukio la kukabidhiwa nyumba 63 kwa Idara ya Uhamiaji eneo la Iyumbu-Dodoma

Baadhi ya nyumba mpya zilizokabidhiwa kwa Idara ya Uhamiaji eneo la Iyumbu Manispaa ya Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Joseph Pombe Magufuli akifuatilia shughuli za burdani kwenye viwanja vya tukio la kukabidhi nyumba 63 za Idara ya Uhamiaji, kulia ni Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna P. Makakala, Iyumbu , Dodoma.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Joseph Pombe Magufuli akisoma ujumbe ulio kwenye Jiwe la la ufunguzi wa Nyumba mpya zilizokabidhiwa kwa Idara ya Uhamiaji, huku akizungukwa na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Waziri Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi, Iyumbu, Dodoma.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Joseph Pombe Magufuli akikata utepe kuashiria ufunguzi wa Nyumba eneo la Iyumbu,Dodoma.

12 Desemba 2017

UHAMIAJI ILIVYOSHIRIKI SHEREHE ZA MIAKA 56 YA UHURU WA TANZANIA BARA

Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna P. Makakala aliungana na Wakuu wa Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama nchini kuadhimisha sherehe za miaka 56 ya Uhuru wa Tanzania Bara ambazo zilifanyika tarehe 9/12/2017.

 Kwa mara ya kwanza Sherehe za Uhuru zikifanyika mkoani Dodoma, Amiri Jeshi Mkuu wa Tanzania Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli amewaongoza Maelfu ya  Wananchi kwenye sherehe  hizo zilizofanyika katika uwanja wa Jamhuri.

Kamishna Jenerali wa Uhamiaji pamoja na Maafisa Waandamizi wa Uhamiaji waliungana na Wakuu wengine wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama  katika Sherehe za Miaka 56 ya Uhuru wa Tanzania Bara.

Sherehe hizo zilianza majira ya saa mbili asubuhi ambapo kama ilivyo taratibu za kiitifaki, Viongozi wakuu wa Serikali na Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama (akiwemo Kamishna Jenerali wa Uhamiaji) waliongozwa na Makamu wa Rais kumlaki Amiri Jeshi Mkuu.

Sherehe hizo pia zilihudhuriwa na marais wastaafu wa Awamu ya Pili (Mhe. Ally Hassan Mwinyi), Tatu (Mhe. Benjamin W. Mkapa) na Nne (Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete) zilipambwa na gwaride na maonesho mbalimbali kutoka vikosi mbalimbali vya majeshi ya ulinzi na usalama.












11 Desemba 2017

KAMISHNA WA UHAMIAJI ZANZIBAR AKAMILISHA ZIARA YAKE MKOA WA KASKAZINI UNGUJA KWA MAFANIKIO

Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar, Johari Masoud Sururu amefanya ziara ya kikazi katika Mkoa wa Kaskazini Unguja tarehe 06 Disemba, 2017.
    
Katika ziara hiyo, Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar, Johari Masoud Sururu amewaasa watumishi wa Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Kaskazini Unguja, kuzingatia Maadili ya kazi, Heshima na Uadilifu kuwa ndio nguzo kwa Utumishi uliotukuka.

  Afisa Uhamiaji Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mrakibu Mwandamizi wa Uhamiaji, Muhsin A. Muhsin akiwasilisha kwa Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar, Johari Masoud Sururu, taarifa ya utendaji kazi wa Ofisi hiyo kuanzia Julai hadi Novemba, 2017, alisema kuwa kumekuwepo na ongezeko la makusanyo ya maduhuli ya Serikali kwa kipindi hicho ambapo jumla ya Dola za Kimarekani 34,000/- zilikusanywa.

Akiwa katika Bandari ya Mkokotoni, Kamishna Sururu alipokewa na Mkuu wa Bandari ya Mkokotoni, Bwana Ahmed Salim Said ambapo  alioneshwa eneo linalotumiwa na baadhi ya Manahodha kushusha abiria kinyume na utaratibu wa Bandari hiyo, wakati alipofanya ziara ya kikazi kwenye maeneo ya utendaji kazi wa Ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar, Johari Masoud Sururu (juu), akiwaasa watumishi wa Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Kaskazini Unguja, kuzingatia Maadili ya kazi, Heshima na Uadilifu kuwa ndio nguzo kwa Utumishi uliotukuka. Alitoa nasha hizo leo tarehe 07 Disemba, 2017 wakati akihitimisha ziara ya siku tatu Mkoani Humo. Kulia kwake ni Afisa Uhamiaji Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mrakibu Mwandamizi wa Uhamiaji, Muhsin A. Muhsin na kushoto ni Afisa Utumishi, Mrakibu wa Uhamiaji, Ali J. Abdulkadir.


Afisa Uhamiaji Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mrakibu Mwandamizi wa Uhamiaji, Muhsin A. Muhsin akiwasilisha kwa Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar, Johari Masoud Sururu, taarifa ya utendaji kazi wa Ofisi hiyo kuanzia Julai hadi Novemba, 2017. Huku akitilia mkazo ongezeko la makusanyo ya maduhuli ya Serikali kwa kipindi hicho Dola za Kimarekani 34,000$ zilikusanywa. Alitoa taarifa hiyo leo tarehe 07 Disemba, 2017 wakati Kamishna Sururu akihitimisha ziara ya siku tatu Mkoani Humo. 

Koplo wa Uhamiaji, Mosi Shadhil Khatib akichangia hoja zilizojadiliwa katika Kikao cha Pamoja cha Wafanyakazi wote wa Uhamiaji Mkoa wa Kaskazini Unguja na Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar, Johari Masoud Sururu, Leo tarehe 07 Disemba, 2017 wakati alihitimisha ziara ya kikazi ya siku tatu Mkoani humo. 

Mkuu wa Bandari ya Mkokotoni, Bwana Ahmed Salim Said, akimuonesha Kamishna wa Uhamiaji Zaznibar, Johari Masoud Sururu na Maafisa aliombatana nao, eneo linalotumiwa na baadhi ya Manahodha kushusha abiria kinyume na utaratibu wa Bandari hiyo, wakati alipofanya ziara ya kikazi kwenye maeneo ya utendaji kazi wa Ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Kaskazini Unguja jana tarehe 06 Disemba, 2017.



Sheha wa Shehia ya Mnarani Bwana Mdungi Sharifu Makemi (picha ya juu) na Sheha wa Shehia ya Nungwi – Banda Kuu Bwana Mohamed Khamis Haji, akimuonesha Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar, Johari Masoud Sururu na Maafisa alioambatana nao, eneo lenye changamoto kubwa wanazokabiliana nazo za Uingiaji wa watu wasiofata sheria katika Ukanda huo.  Alipofanya ziara ya kikazi kwenye maeneo ya utendajikazi wa Ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Kaskazini Unguja jana tarehe 06 Disemba, 2017.

Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar, Johari Masoud Sururu (kulia), akimsikiliza kwa makini Sheha wa Shehia ya Kilindi Bwana Omar Ali Mussa (wa pili kushoto), akitoa shukran zake kwa Uongozi wa Idara kwa ushirikiano mkubwa anaoupata toka kwa Askari wa Uhamiaji. Akisisitiza kauli hiyo Sheha alisema “Ziara yako Kamishna imethibitisha kauli yangu na umeonesha kwa vitendo jinsi ulivyojipanga kushirikiana na wananchi wa eneo letu kutatua changamoto za baadhi wageni wanaoishi hapa bila ya kufata utaratibu” aliyasema hayo jana wakati Kamishna akiendelea na ziara ya kikazi Mkoa wa Kaskazini Unguja. 

08 Desemba 2017

SALAMU ZA MIAKA 56 YA UHURU KUTOKA KWA KAMISHNA JENERALI WA UHAMIAJI


Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. A. P. Makakala ametoa salaam za Heri ya Sikukuu ya Uhuru wa Tanzania bara kwa Watanzania alipokuwa akiwaaga watumishi wa Idara ya Uhamiaji Makao Makuu akielekea Mkoani Dodoma kuhudhuria maadhimisho ya miaka 56 ya Uhuru wa Tanzania bara.

Akizungumza Ofisini kwake Kamishna huyo amewataka Watanzania kudumisha uzalendo kwa kulinda Rasilimali, Ulinzi na Usalama wa nchi kwa faida ya kizazi kilichopo na kijacho. Hii ikiwa ndio njia pekee ya kuwaenzi waasisi wa Taifa letu.

“Uraia wetu una umuhimu wa kipekee kwani umebaki kuwa ndio msingi na utambulisho wetu unaotaunganisha wananchi wote bila ya ubaguzi ukilinganisha na utambulisho mwingine kama ukabila au dini na ndio utambulisho wetu kimataifa.Taifa lolote huru liwe kubwa au dogo haliwezi kukamilika bila ya kuwa na raia wake, ndiyo maana miaka 56 ya Uhuru wetu tunajitambua na kujivunia kuwa Watanzania” Alisema Kamishna Jenerali wa Uhamiaji.


Kwa msingi huo suala la kutambua nani ni raia na nani ni mgeni litabakia kuwa lengo kuu la Idara, kwakuwa raia ndiyo wanaotakiwa kunufaika na Rasilimali za nchi na Haki zinazotolewa na nchi kwa raia wake.

Pamoja na haki hizo za Kikatiba na za asili, lakini pia ni raia hao wenye wajibu wa kulinda Taifa lao dhidi ya uvamizi wowote na rasilimali za  Taifa kama zilivyopiganiwa na Mwasisi na Baba wa Taifa letu Hayati Mwl Julius K. Nyerere na kuongeza kuwa jukumu la ulinzi na usalama wa nchi ni la wananchi wote na hasa wazalendo.

Ni vyema kufahamu kuwa Uraia wetu ndio Utanzania wetu hivyo basi hatuna budi kuadhimisha siku hii adhimu tukiwa na ndoto na matarajio ya kuijenga Tanzania mpya ya Viwanda.




06 Desemba 2017

Uhamiaji Singida yaimarisha Doria na Misako ya Wahamiaji Haramu

Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Singida imeimarisha ukaguzi, doria na misako ili kudhibiti wahamiaji haramu; Doria na misako hiyo inajumuisha ukaguzi wa maghala, hoteli, maeneo ya starehe, magari ya mizigo pamoja na mabasi ya abiria.


Maafisa Uhamiaji wanaosimamia doria na misako wameonekana maeneo mbali mbali ndani na nje ya mji wa Singida wakitekeleza majukumu yao. Mkaguzi Msaidizi wa Uhamiaji Elizabeth Kichonge ambaye alikuwa akiongoza kikosi cha Maafisa na askari watano alionekana akikagua nyaraka za wageni katika stendi ya mabasi ya mikoani mjini Singida.


“Kutokana na wimbi la wahamiaji haramu kubadili njia na sasa kupitia Mkoani kwetu kuelekea kusini mwa nchi, tumeamua kuzidisha ukaguzi kwenye vyombo vya usafiri. Kupitia zoezi hili, kuna mafanikio ambayo tumeyaona; mfano kwa siku chache hizi tulizofanya kazi, tumeshakamata watuhumiwa zaidi ya thelathini” Alisema Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji Angela Shija ambaye ni Kaimu Afisa Uhamiaji Mkoa wa Singida.


Pamoja na ukaguzi, doria na misako inayoendelea kwa sasa, pia Uhamiaji Mkoa wa Singida wanatoa elimu ya Uhamiaji na Uraia kwa abiria wa mabasi, wananchi wa kawaida pamoja na vijana wanaoshiriki mafunzo ya Mgambo Mkoani humo. Pia Idara ya Uhamiaji Mkoani Singida inashirikiana kwa karibu na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) katika kufanikisha zoezi la uandikishwaji wa vitambulisho vya Taifa ili kuhakikisha watu wasiostahili hawajipenyezi kwa lengo la kuandikishwa.



Hadi sasa wahamiaji haramu 30 kutoka nchi za Maziwa Makuu (Rwanda, Burundi na DRC) tayari wameshakamatwa na hatua mbalimbali zimechukuliwa dhidi yao ambapo watu watano wamehalalisha ukaazi wao nchini, watu saba wameondoshwa nchini, watu 17 wanaendelea kuchunguzwa uhalali wa uwepo wao nchini na mmoja alifikishwa mahakamani na kukutwa na hatia ambapo alifungwa jela mwaka mmoja.



Mkaguzi Msaidizi wa Uhamiaji Elizabeth Kichonge akikagua nyaraka za wageni katika stendi kuu ya mabasi yaendayo Mikoani.

Koplo wa Uhamiaji Faraja Wanjara akitoa elimu ya Uhamiaji na Uraia  kwa abiria  

Mkaguzi Msaidizi  wa Uhamiaji Isack Maganga (mwenye shati la draft) na Koplo wa Uhamiaji Abdallah Makacha wakiwateremsha watuhumiwa wa uhamiaji kwenye basi mara baada ya ukaguzi.

Mkaguzi Msaidizi wa Uhamiaji Lawi Kumburu akimchukua maelezo mtuhumiwa alioingia nchini bila kibali cha Uhamiaji

Afisa Uhamiaji  akipekua  begi la mtuhumiwa 

Mkaguzi wa Uhamiaji Owden Kalengo na Mkaguzi Msaidizi wa Uhamiaji Lawi Kumburu wakimuhoji mtuhumiwa ili kujiridhisha juu ya uraia wake.

Mrakibu Msaidizi wa Uhamiaji Roman Mtono akitoa elimu ya maswala ya Uhamiaji  kwa vijana wanaoshiriki mafunzo ya awali ya Mgambo. 


Wahamiaji Haramu waliokamatwa katika  kizuizi cha barabara kuu iendayo Dar Es Salaam 

Timu ya Netiboli ya Uhamiaji Queens yamaliza safari yake kwenye Ligi ya Muungano kwa ushindi wa Pili


Mabingwa mara mbili mfululizo wa Ligi Kuu ya Muungano mpira wa Pete, Timu ya Uhamiaji Queens imemaliza mashindano hayo kwa kushika nafasi ya pili nyuma ya timu ya Jeshi ya JKT Mbweni ambayo ilifanikiwa kushinda katika pambano la fainali kwa magoli 31-29, mjini Zanzibar.

Makamu Bingwa hao walipambana kwa udi na uvumba ingawa bahati haikuwa yao baada ya kutoka sare robo ya kwanza na kutofautiana kwa magoli mawili robo tatu za mwisho hivyo kulazimika kuuachia ubingwa ambao waliushikilia kwa muda wa miaka miwili mfululizo.

"Tumeshindwa kwa kupoteza pambano la leo, tupo tayari kupambana zaidi na kushinda fainali zilizo mbele yetu", alikiri kocha wa Uhamiaji Queens, Mkaguzi Msaidizi wa Magereza Winfrida Emmanuel.

Katika mechi za Makundi, Uhamiaji walianza kwa kuwabamiza Mafunzo mabao 40 kwa 39, wakacheza na Zimamoto nayo wakaibugiza magoli 64 kwa 27.

Mechi zingine walizocheza ni dhidi ya Jeshi Stars ambapo Uhamiaji waliibuka na ushindi wa mabao 56 kwa 49 ambapo mechi ya mwisho katika makundi walicheza na Duma ambapo waliwafunga magoli 61 kwa 29 na kufanikiwa kuingia nusu fainali.

Timu ya Uhamiaji Queens ilicheza fainali na timu ya KVZ ambapo malikia hao waliendeleza wimbi la ushindi kwa kuifunga timu hiyo mabao 55 kwa 43 na kufanikiwa kutinga fainali.

Katika mchezo wa fainali, Malikia hawa wa Uhamiaji pamoja na kucheza kwa ustadi mkubwa, Uhamiaji Queens walilazwa kwa bao 31 kwa 29 na kuambulia nafasi ya pili.

"Tumecheza vizuri sana ingawa JKT Mbweni wametuzidi kidogo ila nao wanajua Uhamiaji Queens ni timu ya vipi. Mashindano yajayo tutawadhibiti tu, kufungwa leo sio kwamba ndio watatufunga kila siku." Alisema Bi. Neema ambaye ni nahodha wa Uhamiaji Queens.

Uhamiaji Queens imekuwa ni kinara katika mashindano ya Netball hapa nchini na imekuwa ikileta sifa kubwa kwa idara ya Uhamiaji.


Nahodha akikabidhiwa Kombe la Mshindi wa Pili wa Michuano ya Netball nchini


Kikosi cha Timu na Benchi la Ufundi kilichotwaa nafasi ya pili ya Mashindano ya Netball nchini