Idara ya Uhamiaji katika Kituo cha Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) imefunga Vifaa vyenye mfumo mpya wa utambuzi
na ulinganisho wa sura (Facial Recognition and Matching System) kwa abiria
wanaoingia nchini.
Akiongea baada ya kupokea vifaa hivyo, Kamishna wa Uhamiaji
anayesimamia Divisheni ya Usimamizi na Udhibiti wa Mipaka Samwel Rhobby Magweiga,
amesema kuwa huo ni muendelezo wa mikakati ya Idara katika kuimarisha na
kuhuisha KANZIDATA ya wanaoingia nchini.
“Vifaa na mfumo huu utasaidia sana katika kukusanya taarifa
za abiria wote wanaoingia nchini kupitia hapa (JNIA), kama mlivyofahamishwa,
mfumo huu unachukua sura ya mtu na kulinganisha na sura nyingine zilizomo
kwenye kanzidata ili kuhakikisha taarifa zilizo kwenye pasipoti yake ni za
pekee na hakuna mtu mwenye sura kama yake au mtu mwenye sura ingine kuwa na
taarifa kama zake.”Alieleza Kamishna Samwel Magweiga.
Awali wakati akabidhiana vifaa hivyo, Mwakilishi mkazi wa Shirika la Uhamiaji la Kimataifa (IOM) Dr. Qasim Sufi alisema kwamba IOM itashirikiana na Idara ya Uhamiaji katika suala zima la udhibiti wa uingiaji na utokaji wa raia na wageni.
Idara ya Uhamiaji kwa kushirikiana na shirika hilo, wamefunga vifaa vingine vyenye mfumo huo kwenye vituo vya Kiwanja cha Ndege cha
Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA) pamoja na mpaka wa Holili kwa pande zote mbili
za Tanzania na Kenya.
Kupitia ushirikiano huo na IOM, Idara ya Uhamiaji itaendelea
kuimarisha maeneo yote ya mipaka kwa kufunga vifaa na mfumo huu wa kisasa zaidi
kutumiwa hapa Afrika Mashariki.
Kamishna wa Uhamiaji (Usimamizi na Udhibiti wa Mipaka) Samwl Magweiga (wa kwanza kulia) akisikiliza kwa makini namna mfumo huo unavyofanya kazi wakati wa ufungaji wa vifaa vyenye mfumo huo. |
Nelson Gonzales (aliyeshika pasipoti) akielezea namna mfumo huo unavyofanya kazi Kamishna na Maafisa Uhamiaji wa Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere. |
Kamishna Wa Uhamiaji (Usimamizi na Udhibiti wa Mipaka) akieleza kuridhishwa na namna vifaa na mfumo huo unavyofanya kazi ya utambuzi na ulinganishi wa sura na taarifa za abiria wanaoingia nchini
|
Kamishna wa Uhamiaji (Usimamizi na Udhibiti wa Mipaka) akikabidhiwa nyaraka za mfumo huo na Mwakilishi Mkazi wa IOM Dr. Qasim Sufi mara baada ya ufungaji wa vifaa hivyo. |
That's where we want to be. Security is our first priority to our Nation. Tanzania Kwanza.
JibuFuta