Visitors

IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA UHAMIAJI HABARI BLOGU KARIBU KWENYE BLOG RASMI YA IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA TUNAKULETEA MATUKIO YANAYOTOKEA KILA SIKU KATIKA IDARA YA UHAMIAJI TAFADHALI TUNAOMBA TUFUATILIE PIA KATIKA MITANDAO YETU YA KIJAMII

21 Novemba 2017

KAMISHNA JENERALI WA UHAMIAJI ATEMA ‘CHECHE’ KATIKA UZINDUZI WA ZOEZI LA UANDIKISHWAJI VITAMBULISHO VYA TAIFA,

Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna P. Makakala amemuagiza Afisa Uhamiaji Mkoa wa Mara kushirikiana kwa karibu zaidi na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ili kuhakikisha wanaopatiwa Vitambulisho vya Taifa ni raia wa Tanzania, wageni wanaoishi nchini kihalali (wakaazi) na wakimbizi. 

Akiongea katika uzinduzi wa zoezi hilo kwa mkoa wa Mara ambapo mgeni rasmi alikuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mheshimiwa Hamad Masauni, Dkt. Makakala pia aliwataka wananchi wa mkoa wa Mara kuwa wazalendo kwa kuwafichua wahamiaji haramu watakaojaribu kujiandikisha kwa ajili ya kupatiwa vitambulisho vya Taifa.

“Nimemuagiza Afisa Uhamiaji Mkoa wa Mara pamoja na mikoa mingine nchini kushirikiana kwa karibu na mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa kwenye zoezi la uandikishwaji ili kuhakikisha kuwa wanaopatiwa vitambulisho vya Taifa ni wale wanaostahili tu, pia nawaomba nanyi wananchi mjitokeze kuwafichua wahamiaji haramu ambao watajitokeza kuomba vitambulisho, toeni taarifa kwa Uhamiaji, NIDA na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi yao. Nawatahadharisha wahamiaji haramu na wengine wasiostahili kutojihusisha na zoezi hili kwani kufanya hivyo ni kinyume na sheria” Alisisitiza Kamishna Jenerali.

Uzinduzi huo ambao ulifanyika katika Viwanja Vya Mendoza Musoma Mjini siku ya tarehe 19 Novemba ulihudhuriwa na Naibu waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mheshimiwa Hamad Masauni, Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Adam Malima ambaye ndiye mratibu wa zoezi hilo katika mkoa wake, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama Mkoa, Kaimu Mkurugenzi wa RITA Bi.  Emmy Hudson na Maafisa waandamizi toka NIDA.  

Kadhalika NIDA inakusudia kutoa vitambulisho vya aina tatu ambavyo ni vya raia wa Tanzania, Wageni wakaazi na wakimbizi. Zoezi hili halitawahusu wahamiaji haramu na walowezi.


Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala akiwahutubia wananchi waliohudhuria katika Uzinduzi wa Zoezi la Uandikishwaji wa Vitambulisho vya Taifa wilayani Tarime mkoa wa Mara. 
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mheshimiwa Hamad Masauni akizindua zoezi la uandikishwaji

Dkt. Anna Makakala akifuatilia hotuba ya Mheshimiwa Naibu Waziri katika uzinduzi wa zoezi hilo jana

Afisa Uhamiaji akielezea namna ya uingizaji wa taarifa na utoaji wa vitambulisho unavyofanyika

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni