Visitors

IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA UHAMIAJI HABARI BLOGU KARIBU KWENYE BLOG RASMI YA IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA TUNAKULETEA MATUKIO YANAYOTOKEA KILA SIKU KATIKA IDARA YA UHAMIAJI TAFADHALI TUNAOMBA TUFUATILIE PIA KATIKA MITANDAO YETU YA KIJAMII

28 Machi 2019

Pasipoti Mpya ya Tanzania ya Kilektroniki yatunikiwa Tuzo ya Ubora

Kamishna wa Uhamiaji (Pasipoti na Uraia) Gerald Kihinga (katikati) akiwa na Tuzo hio


Pasipoti Mpya ya Tanzania ya Kielektroni imetunikiwa Tuzo ya Pasipoti Bora katika Ukanda wa Ulaya, Mashariki ya Kati na Afrika (Europe, Middle East and Africa - EMEA) kwa kukidhi Viwango vya Ubora wa Kimataifa vinavyopendekezwa na Shirika la la Umoja wa Mataifa linalosimamia Usafiri wa Anga (International Civil Aviation Organisation - ICAO) kwa Mwaka 2019 katika Sherehe zilizofanyika Kisiwa cha Malta siku ya Jumanne tarehe 26 Machi 2019.
Tuzo ambazo huaandaliwa na kutolewa na Taasisi ya RECONNAISSANCE ambayo huzingatia ubora na usalama wa Uchapishaji wa Nyaraka za Kielektroniki kama vile Vitambulisho vya Taifa, fedha za noti na Pasipoti. Vipengele vinavyozingatiwa katika Tuzo hizi ni pamoja na Usalama wa nyaraka, Usanifu, tekinolojia, na Utambulisho wa nchi.
Katika kipengele cha utambulisho wa nchi yetu (National Identity), Pasipoti hii imesanifiwa kwa kuzingatia utamaduni wa Kitanzania na maliasili tulizonazo ambazo ni fahari ya nchi yetu. Michoro iliyopo katika Pasipoti hiyo ni pamoja Wanyama, majengo ya kihistoria, Matukio ya Kitaifa na Nukuu za Hamasa za Hayati baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.
Katika kipengele cha Usalama, Pasipoti hii ina kifaa maalum chenye uwezo wa kutunza taarifa za mmiliki wa pasipoti “Micro Chip” na hivyo kufanya suala la utunzaji wa usalama wa pasipoti hizi kuwa wa hali ya juu zaidi. Pasipoti hii ina uwezo wa kutunza kumbukumbu za kibailojia (Biometric features). Pia pasipoti hii ni ngumu kughushiwa na wahalifu au watu wanaojaribu kuficha utambulisho wao kwa kutumia pasipoti zisizo zao.
Ikumbukwe kuwa, Utekelezaji wa Mradi huu umefanyika kwa muda mfupi takribani miezi minne tangu kusainiwa kwa mkataba na ukihusisha utoaji wa Pasipoti za aina tatu (Ordinary, Service & Diplomatic)
Tuzo hiyo ilipokelewa na Kamishna wa Uhamiaji (Pasipoti na Uraia) Gerald Kihinga kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Idara ya Uhamiaji. 

20 Machi 2019

SIRARI: WANANCHI WAFUNGUKA KUHUSU WAHAMIAJI HARAMU, WAAHIDI KUTOA USHIRIKIANO.
Wakazi na viongozi wa Kata za Sirari, Gwitiryo, Pemba na Mbogi pamoja na wakazi wa Kata ya Isebania (Kenya) wameahidi kutoa ushirikiano wa dhati kwa vyombo vya Ulinzi na Usalama vilivyopo mpakani ili kupambana na wimbi la wahamiaji haramu wanaoingia nchini Tanzania na Kenya.

Hayo waliyasema wakati wa mkutano wa Hadhara uliofanyika katika uwanja wa Tarafa katika Kijiji cha Sirari, Wilayani Tarime.

Mkutano huo ambao ni sehemu ya Warsha ya “Ushirikishwaji Wananchi katika Ulinzi na Usimamizi wa Mipaka” unasimamiwa na Idara ya Uhamiaji kwa kushirikiana na Shirika la Uhamiaji la Kimataifa (IOM) ni muendelezo wa kuwajengea uelewa wananchi waishio maeneo ya mipakani ili kushiriki katika suala zima la Ulinzi na Usimamizi wa mpaka katika maeneo yao.

Akifungua mkutano huo, Mgeni rasmi Bwana Kemore Kemore ambaye ni Katibu Tarafa wa Inchugu aliishukuru Idara ya Uhamiaji na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji kwa kuamua kukutana na wananchi wa pande zote mbili kupawatia elimu juu ya Uhamiaji Haramu, Usafirishaji Haramu, Usafirishaji wa Magendo wa Binadamu, na athari zake kwa Usalama wa Nchi.

“Nashukuru sana kwa Uhamiaji na IOM kuja hapa na kufanya mkutano na wananchi. Wananchi wakielimika basi hata hizi changamoto za mpakani zitapungua au kwisha kabisa, na niwaombe viongozi wenzangu na wananchi wote mliohudhuria hapa, yote mtakayofundishwa basi nanyi muwe walimu kwa wengine ambao hawakufika hapa’’ Alieleza Bwana Kemore.

Mkutano huu ulishirikisha Wananchi wa kawaida, madereva bodaboda na mabasi, wafanyabiashara, mamalishe, wajasiriamali, vijana, Viongozi wa vitongoji, vijiji, na Kata pamoja na wawakilishi wa taasisi na idara za serikalini zilizopo mpakani kwa pande zote mbili (Kenya na Tanzania).

Mzee Chacha Magatti, mkazi wa Kijiji cha Sirari alisema kuwa baada ya kupata elimu juu ya madhara ya wahamiaji haramu kwa usalama na uchumi wa nchi sasa yuko tayari kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama wa nchi.

“Kwa kweli inabidi wananchi wa maeneo ya mipakani tuwe wazalendo kwa nchi yetu. Unakuta watu hawatambuliki wametokea wapi, wanapita vijijini kwetu, wanapitishwa na bodaboda na mafuso kwenda Tarime. Ukichunguza unaweza kusema watu hao ni wasomali au waethiopia. Sasa kwa jinsi tulivyoelimishwa katika mkutano huu, nimeona kuanzia sasa si vyema kukaa kimya. Nikiwaona lazima nitoe taarifa kwa wahusika ili wajiridhishe kama hawa watu wameingia kihalali.” Alisema Mzee Magatti.

Diwani wa Kata ya Sirari Mheshimiwa Nyangoko alisisitiza kuwa kuna haja ya kuwa na mikutano kama hii angalau mara mbili kwa mwaka ili kujenga uelewa kwa wananchi na kuwakumbusha wajibu wao kwa nchi yao kwani ulinzi wa nchi unaanzia ngazi ya familia, kitongoji, Kijiji, kata, tarafa, wilaya, mkoa na Taifa kwa ujumla.

Akichangia mada ya Magendo ya binadamu na bidhaa, Afisa kutoka TRA alisema kwamba pamoja na juhudi zinazofanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania kudhibiti uingizaji na usafirishaji nje bidhaa zinazotakiwa kulipiwa kodi, bado kuna baadhi ya watu wanashiriki katika magendo lakini juhudi zinaendelea kuwadhibiti.

Nae mtoa mada kutoka Polisi, Mkaguzi Msaidizi Juma alisema suala la uhalifu mpakani japo kwa sasa limepungua lakini bado ni changamoto ambayo polisi wanaendelea kupambana nayo. Wahalifu wakifanya matukio Tanzania wanakimbilia upande wa pili (Kenya).
Nao maafisa Uhamiaji na wale wa Mamlaka ya Mapato kutoka Kenya waliwaasa wananchi kufuata sheria wakati wa kuvuka mpaka ili kuepuka kuingia matatani kwani mtu anaevuka mpaka ni lazima apite kituo cha uhamiaji na kama ana mizigo lazima apite KRA kwa ukaguzi.

Diwani wa Kata ya Gutiryo Mheshimiwa Adam Nyawambura aliungana na viongozi wengine katika kuishukuru Idara ya Uhamiaji kwa kuandaa warsha na mikutano na wananchi kwa kuwajengea uelewa wa mambo ambayo kwa mpakani yanaonekana kero kwa wananchi lakini yanatakiwa kufuatwa kwa mujibu wa sheria.

“Ni jambo jema kuja kwa wananchi na kuwaelimisha mambo yanayotakiwa kufuatwa kwa mujibu wa sheria za nchi, kuna mambo mengi wananchi wanadhani wanaonewa. Kumbe wanakuwa hajui sheria inasemaje, mfano mtu anaona shule ipo mita mia hapo Kenya anampeleka mtoto wake shule bila kufuata taratibu kwa kuwa hajui anatakiwa afanye nini, kumbe leo wananchi hasa wazazi wenye Watoto wao hapo Isebania watafuata utaratibu wa kupata vibali vya masomo kwa Watoto wao. Bila mkutano huu hii elimu tusingekuwa nayo.” Alieleza Mheshimiwa Nyawambura.

19 Machi 2019

SIRARI: WARSHA YA USHIRIKISHWAJI WANANCHI KATIKA ULINZI NA UDHIBITI WA MIPAKA YAFUNGULIWA NA MKUU WA WILAYA YA TARIME
Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mhe. Charles Kabeho amefungua Warsha ya siku tatu kuanzia leo tarehe 19 hadi 21 Machi, 2019. Ufunguzi wa hiyo umefanyika katika ofisi za kituo cha Uhamiaji Sirari, Wilayani Tarime Mkoa wa Mara.

Mkuu wa Wilaya ya Tarime aliwataka washiriki kuzingatia yale yote watakayofundishwa na kwenda kuyafanyia kazi katika maeneo wanayoishi. Pia alieleza kwamba maeneo ya mpakani kuna changamoto nyingi ambazo vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na taasisi nyingine za serikali zilizopo mpakani haziwezi kuzimaliza peke yake bila ya ushirikishwaji wananchi.

“Ndugu washiriki, kwanza napenda kuwapongeza kwa kuchaguliwa kwenu kushiriki, wengi wenye sifa kama ninyi hawakuipata hii nafasi. Basi naomba nafasi mliopata muitumie vizuri katika kujifunza na mafunzo mtayopata nanyi mkawaelimishe wana jamii wengine ambao hawakupata fursa hii.” Alieleza Mh. Kabeho.

Awali akimkaribisha Mkuu wa Wilaya kufungua warsha, Afisa Uhamiaji Mkoa wa Mara Naibu Kamishna Fredrick Kiondo aliishukuru Idara ya Uhamiaji Makao Makuu na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji(IOM) kuamua kuwafikia wananchi moja kwa moja ili kuwapatia elimu juu ya changamoto zinazokabili maeneo ya mipakani.

“Nawashukuru Uhamiaji Makao Makuu na IOM kwa juhudi zao kubwa kuelimisha jamii ya mipakani. Tunazo changamoto nyingi kwenye masuala ya wahamiaji haramu, magendo ya binadamu, usafirishaji haramu wa binadamu, magendo ya bidhaa, madawa ya kulevya (Mirungi) na uhalifu mwingine wa Kimataifa. Ni Imani yangu kuwa jamii ikipata uelewa itashirikiana vyema na Idara ya Uhamiaji na vyombo vingine vya ulinzi na usalama katika kufichua maovu hayo.”

Warsha hii ya siku tatu inashirikisha viongozi kuanzia kitongoji hadi kata, viongozi wa dini, wadau wa mpaka, viongozi wa bodaboda na mabasi ya abiria kwa upande wa Tanzania na Kenya kwa siku ya kwanza, na siku ya pili na ya tatu ni mikutano ya hadhara na wananchi wa Kata zinazozunguka mpaka wa Sirari. Ni imani kubwa kwa idara ya Uhamiaji Tanzania kuwa wananchi wengi watapata elimu katika masuala ya Uhamiaji, Uraia, Taratibu za Kuingia, Ukaazi na Utokaji nchini, Wahamiaji Haramu, Usafirishaji Haramu wa Binadamu, Uhalifu wa Kimataifa, Magendo ya Binadamu na masuala yote ya Ulinzi na Udhibiti wa Mpaka katika maeneo yao.15 Machi 2019

HOROHORO: WAKAZI WA MAENEO YA MPAKANI WAAHIDI KUSHIRIKIANA NA IDARA YA UHAMIAJI KATIKA UDHIBTI NA USIMAMIZI WA MPAKA.

Wakazi wa vijiji vya mpakani Wilayani Mkinga wasema wako tayari kushirikiana na Idara ya Uhamiaji katika suala zima la Udhibiti na Usimamizi wa mpaka. Wamesema hayo katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Idara ya Uhamiaji kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) uliyofanyika katika Uwanja wa Horohoro Customs katika Kijiji cha Horohoro.

Akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Horohoro Border Ndugu Mery Mery Mirio aliishukuru Idara ya Uhamiaji kwa kukutana na Wananchi ili kutoa elimu na kujadili changamoto zilizopo maeneo ya mpakani.

Awali akimkaribisha Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Msemaji Mkuu wa Idara ya Uhamiaji Mrakibu Ally Mtanda alisema kwamba, Idara ya Uhamiaji imeamua kwa dhati kabisa kuwashirikisha Wananchi katika Suala zima la Ulinzi na Usimamizi wa Mpaka kwani wao (wananchi) ndio wanafahamu mambo yote yanayoendelea mpakani kuliko maafisa Uhamiaji.

“Ndugu wananchi, tumekuja hapa ili kutoa elimu na kuwashirikisha katika Ulinzi na Usimamizi wa Mpaka, nyinyi ndio mnaofahamu watu wanaovusha wahamiaji haramu, wanaofanya magendo ya usafirishaji binadamu na wanaoishi na kuwauzia ardhi wahamiaji haramu. Tumeamua kuja kwenu kuwapa elimu ya uraia, umuhimu wa kushirikiana na idara ya Uhamiaji katika udhibiti na usimamizi wa mpaka tukiamini kuwa ninyi ndio wenye nchi na ndio mnaotakiwa kunufaika na Haki zinazotolewa na serikali kwa raia wake pamoja na rasilimali za Taifa. Kwahiyo mnao wajibu wa kuilinda nchi yenu ili iendelee kuwa salama.” Alieleza Mtanda.

Baadhi ya wananchi waliotoa maoni walisema kwamba wako tayari kushirikiana na Idara ya Uhamiaji kuwafichua wahamiaji haramu wanaoingia nchini. “Kwa maelezo hayo aliyotoa afande, nipo tayari kushiriki katika kuilinda nchi yangu kwani leo nimefahamu madhara yanayoweza kulikumba Taifa kwa kuwahifadhi wahamiaji haramu ikiwa ni pamoja na uwepo wa migogoro ya ardhi, kuongezeka vitendo vya kihalifu, ugaidi, usafirishaji madawa ya kulevya, na kupungua kwa na nafasi za ajira na huduma za jamii.” Alisema Mzee Ally ambaye ni Mkazi wa Horohoro kijijini.

Akifunga mkutano huo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Horohoro Border, aliishukuru Idara ya Uhamiaji kwa kutoa elimu kwa wananchi na kuitaka idara hiyo kuwa na utaratibu wa kukutana na wananchi mara kwa mara kwani wananchi wana taarifa nyingi lakini wanakuwa waoga kufika ofisi za Uhamiaji.
“Kwa mkutano huu, nimeshukuru sana, wananchi hapa wameingia hamasa na uzalendo wa kuilinda nchi yao, zamani walikuwa wanaona suala la ulinzi wa mpaka ni la vyombo vya dola pekee” Alisema Mwenyekiti huyo.

Mkutano huo ulikuwa ni kuhitimisha Warsha ya Siku tatu ya Ushirikishishwaji wa Wananchi katika Ulinzi na Usimamizi wa Mipaka iliyoanza tarehe 13 Machi na kufikia tamati leo siku ya Ijumaa, Machi 15, 2019.


13 Machi 2019

KUKABILIANA NA WAHAMIAJI HARAMU NCHINI: IDARA YA UHAMIAJI YAANZA ‘KUWAFUNDA’ WANANCHI MAENEO YA MIPAKANI

Idara ya Uhamiaji Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Uhamiaji la Kimataifa (IOM) limeanza kutoa mafunzo ya Ushirikishwaji wa Wananchi katika Ulinzi na Usimamizi wa Mipaka katika Kijiji cha Horohoro, mpakani mwa Tanzania na Kenya kwa siku tatu kuanzia leo tarehe 13-15 Machi, 2019.

Warsha hiyo ya Mafunzo ambayo imefunguliwa na Mkuu wa Wilaya ya Mkinga Mhe. Yona Maki, inashirikisha wananchi waishio mpakani wenye ushawishi katika jamii pamoja nao ni viongozi wa dini, wakulima, mgambo, viongozi wa vijiji na waendesha bodaboda.
Awali akifungua warsha hii, Mkuu wa Wilaya ya Mkinga aliipongeza Idara ya Uhamiaji kwa kuamua kutoa mafunzo yenye lengo la kuwashirikisha wananchi wa kawaida katika suala zima la ulinzi na usimamizi wa mipaka.

“Kwanza niwashukuru sana Idara ya Uhamiaji pamoja na watu wa IOM kwa kuamua kutoa mafunzo kwa wananchi wa kawaida. Ninaamini baada ya mafunzo haya, washiriki kwa kuwa ni watu wenye ushawishi katika jamii ya vijiji vya kata hii, watasaidia sana kufikisha ujumbe. Naona kuna viongozi wa bodaboda, hawa bodaboda ndio wanaosafirisha watu, miongoni mwa watu hao kuna wahamiaji haramu pia, naamini wakipewa elimu basi hawa bodaboda watakuwa ni sehemu muhimu katika Ulinzi na Usimamizi wa mipaka yetu”.

Mkuu huyo wa Wilaya alieleza kuwa Baba wa Taifa aliwahi kusema kuwa jukumu la ulinzi wa Taifa ni letu sote na hasa wazalendo. Hivyo jukumu hili la ulinzi si la vyombo vya ulinzi na usalama pekee, bali ni la kila Mtanzania.

Wakati akitoa taarifa kwa Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Afisa Uhamiaji Wilaya Mkinga alisema kwamba jumla ya wahamiaji haramu 216 kutoka mataifa ya Ethiopia, Somalia na Kenya walikamatwa katika wilaya ya Mkinga katika Mwaka 2018.


Warsha hii ya siku tatu imelenga katika kuwajengea uwezo washiriki juu ya Uhalifu wa Kimataifa, Makosa ya kiuhamiaji, Biashara ya Magendo ya Binadamu, Usafirishaji Haramu wa Binadamu, Uraia wa Tanzania na mambo yanayohusiana na Uhamiaji nje ya Mfumo rasmi.