Wakazi na
viongozi wa Kata za Sirari, Gwitiryo, Pemba na Mbogi pamoja na wakazi wa Kata
ya Isebania (Kenya) wameahidi kutoa ushirikiano wa dhati kwa vyombo vya Ulinzi
na Usalama vilivyopo mpakani ili kupambana na wimbi la wahamiaji haramu
wanaoingia nchini Tanzania na Kenya.
Hayo waliyasema
wakati wa mkutano wa Hadhara uliofanyika katika uwanja wa Tarafa katika Kijiji
cha Sirari, Wilayani Tarime.
Mkutano huo
ambao ni sehemu ya Warsha ya “Ushirikishwaji Wananchi katika Ulinzi na
Usimamizi wa Mipaka” unasimamiwa na Idara ya Uhamiaji kwa kushirikiana
na Shirika la Uhamiaji la Kimataifa (IOM) ni muendelezo wa kuwajengea uelewa
wananchi waishio maeneo ya mipakani ili kushiriki katika suala zima la Ulinzi
na Usimamizi wa mpaka katika maeneo yao.
Akifungua
mkutano huo, Mgeni rasmi Bwana Kemore Kemore ambaye ni Katibu Tarafa wa Inchugu
aliishukuru Idara ya Uhamiaji na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji kwa kuamua
kukutana na wananchi wa pande zote mbili kupawatia elimu juu ya Uhamiaji Haramu,
Usafirishaji Haramu, Usafirishaji wa Magendo wa Binadamu, na athari zake kwa
Usalama wa Nchi.
“Nashukuru sana
kwa Uhamiaji na IOM kuja hapa na kufanya mkutano na wananchi. Wananchi
wakielimika basi hata hizi changamoto za mpakani zitapungua au kwisha kabisa, na
niwaombe viongozi wenzangu na wananchi wote mliohudhuria hapa, yote
mtakayofundishwa basi nanyi muwe walimu kwa wengine ambao hawakufika hapa’’ Alieleza
Bwana Kemore.
Mkutano huu ulishirikisha
Wananchi wa kawaida, madereva bodaboda na mabasi, wafanyabiashara, mamalishe,
wajasiriamali, vijana, Viongozi wa vitongoji, vijiji, na Kata pamoja na
wawakilishi wa taasisi na idara za serikalini zilizopo mpakani kwa pande zote
mbili (Kenya na Tanzania).
Mzee Chacha
Magatti, mkazi wa Kijiji cha Sirari alisema kuwa baada ya kupata elimu juu ya
madhara ya wahamiaji haramu kwa usalama na uchumi wa nchi sasa yuko tayari
kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama wa nchi.
“Kwa kweli
inabidi wananchi wa maeneo ya mipakani tuwe wazalendo kwa nchi yetu. Unakuta
watu hawatambuliki wametokea wapi, wanapita vijijini kwetu, wanapitishwa na
bodaboda na mafuso kwenda Tarime. Ukichunguza unaweza kusema watu hao ni
wasomali au waethiopia. Sasa kwa jinsi tulivyoelimishwa katika mkutano huu,
nimeona kuanzia sasa si vyema kukaa kimya. Nikiwaona lazima nitoe taarifa kwa
wahusika ili wajiridhishe kama hawa watu wameingia kihalali.”
Alisema Mzee Magatti.
Diwani wa Kata
ya Sirari Mheshimiwa Nyangoko alisisitiza kuwa kuna haja ya kuwa na mikutano
kama hii angalau mara mbili kwa mwaka ili kujenga uelewa kwa wananchi na kuwakumbusha
wajibu wao kwa nchi yao kwani ulinzi wa nchi unaanzia ngazi ya familia,
kitongoji, Kijiji, kata, tarafa, wilaya, mkoa na Taifa kwa ujumla.
Akichangia mada
ya Magendo ya binadamu na bidhaa, Afisa kutoka TRA alisema kwamba pamoja na
juhudi zinazofanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania kudhibiti uingizaji na
usafirishaji nje bidhaa zinazotakiwa kulipiwa kodi, bado kuna baadhi ya watu
wanashiriki katika magendo lakini juhudi zinaendelea kuwadhibiti.
Nae mtoa mada
kutoka Polisi, Mkaguzi Msaidizi Juma alisema suala la uhalifu mpakani japo kwa
sasa limepungua lakini bado ni changamoto ambayo polisi wanaendelea kupambana
nayo. Wahalifu wakifanya matukio Tanzania wanakimbilia upande wa pili (Kenya).
Nao maafisa
Uhamiaji na wale wa Mamlaka ya Mapato kutoka Kenya waliwaasa wananchi kufuata
sheria wakati wa kuvuka mpaka ili kuepuka kuingia matatani kwani mtu anaevuka
mpaka ni lazima apite kituo cha uhamiaji na kama ana mizigo lazima apite KRA
kwa ukaguzi.
Diwani wa Kata
ya Gutiryo Mheshimiwa Adam Nyawambura aliungana na viongozi wengine katika
kuishukuru Idara ya Uhamiaji kwa kuandaa warsha na mikutano na wananchi kwa
kuwajengea uelewa wa mambo ambayo kwa mpakani yanaonekana kero kwa wananchi
lakini yanatakiwa kufuatwa kwa mujibu wa sheria.
“Ni jambo jema
kuja kwa wananchi na kuwaelimisha mambo yanayotakiwa kufuatwa kwa mujibu wa
sheria za nchi, kuna mambo mengi wananchi wanadhani wanaonewa. Kumbe wanakuwa
hajui sheria inasemaje, mfano mtu anaona shule ipo mita mia hapo Kenya
anampeleka mtoto wake shule bila kufuata taratibu kwa kuwa hajui anatakiwa
afanye nini, kumbe leo wananchi hasa wazazi wenye Watoto wao hapo Isebania
watafuata utaratibu wa kupata vibali vya masomo kwa Watoto wao. Bila mkutano
huu hii elimu tusingekuwa nayo.” Alieleza Mheshimiwa Nyawambura.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni