Mkuu wa Wilaya
ya Tarime, Mhe. Charles Kabeho amefungua Warsha ya siku tatu kuanzia leo tarehe
19 hadi 21 Machi, 2019. Ufunguzi wa hiyo umefanyika katika ofisi za kituo cha Uhamiaji
Sirari, Wilayani Tarime Mkoa wa Mara.
Mkuu wa Wilaya ya
Tarime aliwataka washiriki kuzingatia yale yote watakayofundishwa na kwenda
kuyafanyia kazi katika maeneo wanayoishi. Pia alieleza kwamba maeneo ya mpakani
kuna changamoto nyingi ambazo vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na taasisi
nyingine za serikali zilizopo mpakani haziwezi kuzimaliza peke yake bila ya
ushirikishwaji wananchi.
“Ndugu washiriki, kwanza napenda kuwapongeza kwa kuchaguliwa kwenu
kushiriki, wengi wenye sifa kama ninyi hawakuipata hii nafasi. Basi naomba
nafasi mliopata muitumie vizuri katika kujifunza na mafunzo mtayopata nanyi
mkawaelimishe wana jamii wengine ambao hawakupata fursa hii.” Alieleza
Mh. Kabeho.
Awali
akimkaribisha Mkuu wa Wilaya kufungua warsha, Afisa Uhamiaji Mkoa wa Mara Naibu
Kamishna Fredrick Kiondo aliishukuru Idara ya Uhamiaji Makao Makuu na Shirika
la Kimataifa la Uhamiaji(IOM) kuamua kuwafikia wananchi moja kwa moja ili kuwapatia
elimu juu ya changamoto zinazokabili maeneo ya mipakani.
“Nawashukuru Uhamiaji Makao Makuu na IOM kwa juhudi zao kubwa kuelimisha
jamii ya mipakani. Tunazo changamoto nyingi kwenye masuala ya wahamiaji haramu,
magendo ya binadamu, usafirishaji haramu wa binadamu, magendo ya bidhaa, madawa
ya kulevya (Mirungi) na uhalifu mwingine wa Kimataifa. Ni Imani yangu kuwa
jamii ikipata uelewa itashirikiana vyema na Idara ya Uhamiaji na vyombo vingine
vya ulinzi na usalama katika kufichua maovu hayo.”
Warsha hii ya
siku tatu inashirikisha viongozi kuanzia kitongoji hadi kata, viongozi wa dini,
wadau wa mpaka, viongozi wa bodaboda na mabasi ya abiria kwa upande wa Tanzania
na Kenya kwa siku ya kwanza, na siku ya pili na ya tatu ni mikutano ya hadhara
na wananchi wa Kata zinazozunguka mpaka wa Sirari. Ni imani kubwa kwa idara ya
Uhamiaji Tanzania kuwa wananchi wengi watapata elimu katika masuala ya Uhamiaji,
Uraia, Taratibu za Kuingia, Ukaazi na Utokaji nchini, Wahamiaji Haramu,
Usafirishaji Haramu wa Binadamu, Uhalifu wa Kimataifa, Magendo ya Binadamu na
masuala yote ya Ulinzi na Udhibiti wa Mpaka katika maeneo yao.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni