Visitors

IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA UHAMIAJI HABARI BLOGU KARIBU KWENYE BLOG RASMI YA IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA TUNAKULETEA MATUKIO YANAYOTOKEA KILA SIKU KATIKA IDARA YA UHAMIAJI TAFADHALI TUNAOMBA TUFUATILIE PIA KATIKA MITANDAO YETU YA KIJAMII

18 Desemba 2022

#Jeshi la Uhamiaji Nchini Laadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wahamaji Duniani

Na Amani Mbwaga.

Dar es Salaam.

Jeshi la uhamiaji nchini Tanzania leo tarehe 18 Disemba 2022 limeadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wahamaji Duniani (International Migrants’ Day), ambayo kwa Mwaka huu ina Kauli Mbiu isemayo “Mimi ni Mhamaji” yaani “I am a Migrant.”

Maadhimisho hayo yamefanyika Jijini Dar es salaam katika Ofisi ya Uhamiaji Kurasini huku yakiongozwa na Mgeni rasmi Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Jumanne Sagini (Mb)

Katika Hotuba yake Mhe. Waziri Jumanne Sagini amelipongeza Jeshi la Uhamiaji kwa kuadhimisha siku hii ili kutoa uelewa kwa watanzania juu ya dhana nzima ya Uhamiaji na Uhamaji.

“Tunapohama tuzingatie sheria Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inaungana na Mataifa mengi dunuani katika kuadhimisha siku hii adhimu”alisema  Mhe. Sagini. 

Aidha Mhe. Waziri Sagini pia ameipongeza serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuweka Mazingira mazuri kwa wahamaji ambapo serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanya marekebisho ya sheria na kanuni za Uhamiaji Sura 54 Rejeo la Mwaka 2016 ili kuwezesha utoaji wa vibali maalumu vya Ukaazi (Migrant Pass) kwa wahamaji walowezi na vibali vya wahamaji wa msimu (Seasonal Migrant Pass) kwa lengo la kuwatambua wahamiaji walowezi na kutataua tatizo la wahamiaji haramu hapa nchini.

Vile vile serikali imefanya mabadiliko ya sheria ya Uhamiaji Sura 54 kwa kupunguza ada ya kibali cha ukaazi kwa wawekezaji wa nje wenye asili ya Tanzania Diaspora toka dola za Kimarekeni 3050 hadi dola za Kimarekeni 1090 ili kuhamasisha raia hao kuja kuwekekeza katika nchi yao ya asili.

Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Uhamiaji nchini (CGI) Dkt. Anna Makakala alisema Jeshi la Uhamiaji linatambua na kupokea wahamaji kutoka duniani kote wanaoingia hapa nchini kwa madhumuni mbali mbali, na kwamba, wana haki ya kufaidika na fursa mbali mbali zilizopo hapa nchini, Hivyo, kupitia Sheria ya Uhamiaji Sura ya 54 Jeshi la Uhamiaji  limeendelea kutekeleza vyema jukumu muhimu la kuwezesha, uingiaji na utokaji wa wahamaji hapa Nchini.

Ili kwenda sambamba na mabadiliko ya mwenendo wa Kiuhamiaji na kasi ya teknolojia duniani, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Idara ya Uhamiaji imeboresha mifumo ya utoaji wa huduma za kiuhamiaji ili kukuza Utalii, Uwekezaji na biashara, Aidha, hatua hii ime wawezesha Watanzania kutafuta fursa mbali mbali zilizopo duniani.

Takwimu zinaonesha kwamba, katika kipindi cha mwezi Januari hadi Novemba, 2022 jumla ya raia wa kigeni wapatao 1,172,205 waliingia nchini kwa madhumuni mbalimbali ikiwemo Utalii, Matembezi, Masomo, na shughuli nyingine za muda mfupi, Kwa upande mwingine, jumla ya watu 983, 189 walitoka nchini.

Aidha, katika kipindi tajwa, jumla ya visa za kielektroniki 500, 711, Vibali vya Ukaazi vya Kielektroniki 16,022 vimetolewa kwa raia wa kigeni, ambapo jumla ya raia wa Tanzania 110,137 wamepatiwa Pasipoti Mpya za Kielektroniki tangu kipindi cha Januari hadi Novemba, 2022.

Kwa upande wa Watanzania waliorejea nchini kutoka Mataifa mbali mbali ni 220, 423 na waliondoka nchini ni 250, 540.

Pamoja na kutumia fursa za Uhamaji wa Binadamu, Jeshi la Uhamiaji limeendelea kudhibiti wahamaji wasio rasmi, yaani wasiofuata taratibu za nchi hususani wakati wanapoingia nchini au wanapokiuka taratibu hizo baada ya kuruhusiwa kuingia nchini. 

Lengo la udhibiti huo ni kuhakikisha kwamba, kundi hilo la Wahamaji halihatarishi usalama wa nchi yetu kwa kujihusisha na vitendo vya uhalifu kama Ujambazi, Ugaidi, Utakatishaji fedha na Usafirishaji haramu wa binadamu.

Katika kukabiliana na changamoto hii, Jeshi la  Uhamiaji limeendelea kufuatilia na kudhibiti wageni wasiofuata Sheria na Taratibu za Nchi kwa kuwakamata na kuwachukulia hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani na kuwaondosha nchini. 

Kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Novemba, 2022 jumla ya Wahamiaji haramu 18,289 walikamatwa na kuchukuliwa hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani na baadhi yao kuondoshwa nchini.

“Katika kuadhimisha siku hii ya Kimataifa ya Wahamaji Duniani, Jeshi la  Uhamiaji linapenda kutambua mchango mkubwa kutoka katika Shirika la Uhamaji la Kimataifa (IOM) – Tanzania chini ya Uongozi wake, Ndugu Maurizio Busatti kwa ushirikiano mkubwa ambao tumeendelea kuupata katika masuala mbali mbali ya Kiuhamiaji ikiwemo kuwaondoa raia wa Ethiopia walioko magerezani na hatimaye kuwarudisha kwao ambapo kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Novemba, 2022 jumla ya raia 993 wa Ethiopia waliokuwa magerezani walirudishwa kwao, ambapo kati ya hao 441 ni kupitia ufadhili wa IOM na raia 552 ni kupitia familia zao, Aidha,  tunawashukuru Watanzania na Wadau wa  Uhamiaji kwa kuweka nchi yetu salama pamoja na kupambana na  wahamaji wasiofuata taratibu” alisema Dkt. Makakala

Siku ya Kimataifa ya Wahamaji Duniani ilianza kuadhimishwa rasmi mnamo tarehe 04 Disemba, 2000 baada ya Azimio Na. 55/93 kupitishwa na Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Tangu kupitishwa kwa azimio hilo, nchi nyingi Duniani, Taasisi za Kimataifa, Taasisi za Serikali na Asasi zisizo za Serikali zimekuwa na utaratibu maalum wa kuadhimisha siku hii kila ifikapo Disemba 18 ya kila mwaka.

Hivyo, kwa kuadhimisha siku hii inaonesha dhahiri kuwa Serikali ya Jamhuri ya Tanzania kupitia Jeshi la Uhamiaji inatekeleza matakwa ya Umoja wa Mataifa.

HABARI PICHA NA MATUKIO
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Nchi Mhe.Jumanne Sagini (Mb) akitoa hotuba yake katika Maadhimisho ya Siku ya Wahamaji Duniani iliyofanyika leo tarehe 18 Disemba 2022 Kurasini Jijini Dar es Salaam.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Nchi Mhe. Jumanne Sagini (Mb) waliokaa (katika) akiwa katika picha ya pamoja na Wawakilishi wa Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama katika Maadhimisho ya Siku ya Wahamaji Duniani iliyofanyika leo tarehe 18 Disemba 2022 Kurasini Jijini Dar es Salaam.
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala akitoa Maelezo kuhusu Siku ya Wahamaji Duniani


Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Ng'wilabuzu Ludigija akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaaam katika kutoa  salamu za Mkoa.

Kiongozi wa Shirika la Uhamaji la Kimataifa (IOM) – Tanzania  Ndugu Maurizio Busatti akitoa salamu

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Nchi Mhe. Jumanne Sagini (Mb) waliokaa (katika) akiwa katika picha ya pamoja na Wakuu wa Uhamiaji Wastaafu na Makamishna Wastaafu wa Uhamiaji katika Maadhimisho ya Siku ya Wahamaji Duniani iliyofanyika leo tarehe 18 Disemba 2022 Kurasini Jijini Dar es Salaam.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Nchi Mhe. Jumanne Sagini (Mb) waliokaa (katika) akiwa katika picha ya pamoja na Makamishna wa Uhamiaji katika Maadhimisho ya Siku ya Wahamaji Duniani iliyofanyika leo tarehe 18 Disemba 2022 Kurasini Jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Nchi Mhe. Jumanne Sagini (Mb) waliokaa (katika) akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa Uhamiaji katika Maadhimisho ya Siku ya Wahamaji Duniani iliyofanyika leo tarehe 18 Disemba 2022 Kurasini Jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Nchi Mhe. Jumanne Sagini (Mb) waliokaa (katika) akiwa katika picha ya pamoja na Wakuu wa Vitengo katika Maadhimisho ya Siku ya Wahamaji Duniani iliyofanyika leo tarehe 18 Disemba 2022 Kurasini Jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Nchi Mhe. Jumanne Sagini (Mb) waliokaa (katika) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa dini katika Maadhimisho ya Siku ya Wahamaji Duniani iliyofanyika leo tarehe 18 Disemba 2022 Kurasini Jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Nchi Mhe. Jumanne Sagini (Mb) waliokaa (katika) akiwa katika picha ya pamoja na Bendi ya Jeshi la Uhamiaji katika Maadhimisho ya Siku ya Wahamaji Duniani iliyofanyika leo tarehe 18 Disemba 2022 Kurasini Jijini Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar es salaam ACP Jumanne Muliro nae alikuwepo akimwakilisha Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wahamaji Duniani
Uhamiaji Band Tanzania


(Picha zote na Amani Mbwaga - Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano)