Visitors

IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA UHAMIAJI HABARI BLOGU KARIBU KWENYE BLOG RASMI YA IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA TUNAKULETEA MATUKIO YANAYOTOKEA KILA SIKU KATIKA IDARA YA UHAMIAJI TAFADHALI TUNAOMBA TUFUATILIE PIA KATIKA MITANDAO YETU YA KIJAMII

26 Mei 2020

ACI Mwanjotile afanikiwa kusambaratisha wahamiaji haramu Mtwara


Mtwara,Tanzania Aliyekuwa Afisa Uhamiaji Mkoa wa Mtwara Kamishna Msaidizi (ACI) James A. Mwanjotile mapema wiki hii akikabidhi ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Mtwara kwa Kamishna Msaidizi Novati Dawson Kato alisema moja ya mafanikio yake makubwa anayojivunia wakati wa uongozi wake Mkoani hapo ni kupambana na kupunguza wimbi la wahamiaji haramu kwa kushirikiana na Wananchi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ambapo mpaka sasa hali ya Mkoa huo ni shwari.


Ameyasema hayo wakati wa makabidhiano ya ofisi ya uhamiaji Mkoa wa Mtwara mara baada ya Kamishina Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Peter Makakala kufanya mabadiliko madogo ya uongozi ndani ya Mkoa huo ambapo amemuhamisha Kamishina Msaidizi James A. Mwanjotile kwenda Jijini Dodoma Kuwa Afisa Uhamiaji Mkoa kuchukua nafasi ya aliyekua Afisa Uhamiaji jijini hapo  Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACI) Abdallah Kitimba ambae amestaafu kazi kwa mujibu wa sheria.

Mabadiliko hayo yameambatana na uteuzi wa Afisa Uhamiaji mpya wa Mkoa wa Mtwara Kamishna Msaidizi Novati Kato ambaye awali alikuwa Afisa Uhamiaji Msaidizi Mkoa wa Morogoro.

Akikabidhi Ofisi, Rasilimali watu na vifaa Kamishina Msaidizi Mwanjotile amewashukuru maofisa na askari wa Mkoa huo kwa kumpa ushirikiano wa kutosha kwa kipindi chote alichoongoza Mkoa huo na kuwataka kuendeleza ushirikiano huo kwa kiongozi mpya aliyewasili kuchukua nafasi yake.

Kamishina Msaidizi James A. Mwanjotile anaondoka Mkoa wa Mtwara akiwa amehudumu kwa kipindi cha miaka mitatu (3) Kwa nafasi hiyo ya Afisa Uhamiaji Mkoa na kuleta na mafanikio makubwa sana kwa Taifa, kutokana na Uongozi wake imara wenye Utii, Uhodari na Weledi wa hali ya juu.

HABARI PICHA NA MATUKIO


Aliyekuwa Afisa Uhamiaji Mkoa wa Mtwara Kamishna Msaidizi (ACI) James A. Mwanjotile (katikati) akiongoza kikao cha makabidhiano ya Ofisi kwa  Afisa Uhamiaji mpya wa Mkoa wa Mtwara Kamishna Msaidizi Novati Kato (wa kwanza kulia) wengine ni Maafisa na Askari wa Uhamiaji Mkoani hapo 

Kaimu Afisa Uhamiaji Wilaya ya Tandahimba Mkaguzi Msaidizi Raymund Mapunda (Aliyesimama) akitoa maelezo ya awali kuhusu kituo cha Uhamiaji wilayani hapo
Mfawidhi wa Kituo cha Mtambaswala kilichopo wilaya ya Nanyumbu Mkoani Mtwara Mkaguzi Emmanuel Mtosa (Kushoto) akitoa maelezo ya Mpaka wa Tanzania na Msumbiji katika daraja la Umoja wakati wa makabidhiano ya ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Mtwara

Makabidhiano ya Ofisi za Vituo Mbalimbali vya Uhamiaji yakiendelea






Mfawidhi wa Kituo cha Uhamiaji Kilambo Mkaguzi Nestori Riwa (Kushoto) akitoa maelezo ya kituo wakati wa Makabidhiano kituo hicho kipo Wilaya ya Mtwara Vijijini Mkoani Mtwara


(Picha zote na Ofisi ya Uhusiano Uhamiaji Mkoa wa Mtwara)

16 Mei 2020

RC Ruvuma Akagua Utayari wa Idara ya Uhamiaji Mipakani

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mhe.Christina S. Mndeme mapema wiki hii amefanya ziara ya  kutembelea vipenyo vya mkoa Ruvuma kukagua utayari wa Idara ya Uhamiaji na vyombo vya ulinzi  na Usalama kwa ujumla katika  kukabiliana na wahamiaji haramu hasa wakati huu wa Mapambano dhindi ya ugonjwa w Covid -19 unaosababishwa na Virusi vya Corona.

Ziara hiyo imemfikisha Mkuu wa Mkoa na Kamati yake ya Ulinzi na Usalama Wilayani Nyasa katika kipenyo cha Chiwindi kinachopakana na nchi jirani ya Msumbiji. 

Lengo kuu la ziara hiyo kufanyika  ilikuwa ni kujiridhisha na ulinzi na usalama mipakani ili kudhibiti matukio yoyote yanayoweza kutokea hasa wakati huu ambapo wengi wanaweza kutumia fursa hiyo kufanya vitendo vya kihalifu kama vile matishio ya kiusalama (ugaidi), usafirishaji wa wahamiaji haramu kwa njia za (Panya) vipenyo nk.

Aidha Mhe. Mndeme ameipongeza Idara ya Uhamiaji kwa kufanya kazi zake kwa makini katika mipaka hiyo na kusisitiza kuendelea kufanya doria za mara kwa mara na kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ili kuhakikisha ulinzi  na usalama wa Mkoa wa Ruvuma na Taifa kwa ujumla unaimarishwa wakati wote.

Hata hivyo ametoa wito kwa wananchi wa maeneo hayo ya mipakani  kuendelea kutoa ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa pale wanapoona wageni wasiowafahamu kuingia chini au wanapoona vitendo viovu vyovvote vinapotokea ambavyo ni kinyume na sheria basi watoe taarifa, kwani jukumu la kuilinda nchi ni la kila Mtanzania. 

HABARI PICHA NA MATUKIO
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mhe.Christina S. Mndeme akiwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wakipita katika moja ya kipenyo cha Chiwindi Wilayani Nyasa kinachopakana na nchi jirani ya Msumbiji  karibu na mpaka rasmi wa Mbababay  unaotenganisha nchi ya Tanzania na Msumbiji. 
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mhe.Christina S. Mndeme akitoa maelekezo  Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa baada ya kumaliza ziara ya mipakani

15 Mei 2020

NMB Yaikabidhi Idara ya Uhamiaji Vifaa vya Kujikinga na Virusi vya Corona (COVID 19)


Idara ya Uhamiaji nchini imepokea vifaa vya kujikinga na maambukizi ya Ugonjwa wa Covid 19 unaosababishwa na virusi vya Corona, kutoka katika Benki ya NMB, ikiwa ni moja ya jitihada za kuunga mkono serikali katika kupambana na kudhibiti maambukizi ya ugojwa huo ulioeneo duniani kote.

Mapema leo hii akipokea Vifaa hivyo katika Ofisi ndogo ya Makao makuu ya Uhamiaji Tanzania iliyopo Kurasini Jijini Dar es salaam Kamishna wa Uhamiaji Divisheni ya Pasipoti na Uraia Gerald Kihinga ameishukuru Benki hiyo kwa kutoa vifaa hivyo na kuahidi kuvitumia ipasavyo ili viweze kuwasaidia wananchi wanaokuja kupata huduma mbali mbali za kiuhamiaji sanjari na Maofisa, Askari na watumishi wa Idara  ili kuweza kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo.


“Kama mnavyojua maelekezo ya serikali ni kwamba tunapoendelea kutoa huduma zetu ni lazima kuzingatia maelekezo ya wizara ya afya na wataalamu wake kwa kuvaa vifaa kinga, kunawa mikono, na kupeana nafasi baina ya mtu na mtu na hilo tunalizingatia sana ili kuhakikisha Maofisa Askari na Wananchi kwa ujumla wanakuwa salama wakati wote” alisema

Aidha Kamishna Kihinga amewataka watanzania kutokua na hofu wanapoingia katika ofisi yoyote ya uhamiaji kupata huduma kwani tahadhari zote za kuwalinda na kujikinga na maambukizi zinachukuliwa kwa umuhimu wa hali ya juu sana.

Kwa Upande wake Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Dar es salaam Bw. Badru Idd akikabidhi vifaa hivyo ameishukuru Idara ya Uhamiaji kwa kufanya kazi Kwa ukaribu na NMB lakini pia amewataka watanzania kutokua na hofu bali wachukue tahadhari zote Kwa kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya.

Vifaa vilivyokabidhiwa ni pamoja na barakoa, vitakasa mikono, vifaa vya kuhifadhia vitakasa mikono na vifaa vya kuhifadhia sabuni.


HABARI PICHA NA MATUKIO
Kamishna wa Uhamiaji Divisheni ya Pasipoti na Uraia Gerald Kihinga (Kulia) akipokea Moja ya vifaa vya kujikinga na maambukizi ya Ugonjwa wa Covid 19 kutoka kwa Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Dar es salaam Bw. Badru Idd 
Kamishna wa Uhamiaji Divisheni ya Pasipoti na Uraia Gerald Kihinga Akitoa salamu za shukrani kutoka Uhamiaji mara baada ya kupokea vifaa
Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Dar es salaam Bw. Badru Idd akitoa malezo mafupi ya vifaa walivyotoa kwa Uhamiaji mapema leo hii katika Ofisi ndogo za Makao Makuu ya Uhamiaji Kurasini Jijini Dar es salaam



Viongozi Waandamizi na Maofisa mbali mbali wa Uhamiaji wakisikiliza kwa makini maelezo ya vifaa vilivyotolewa na NMB (Wengine ni Watumishi wa benki ya NMB) 

 



Picha ya Pmoja Baina ya watumishi wa Benki ya NMB Na Viongozi Kutoka Uhamiaji (Picha zote na Kitengo cha Uhusiano Uhamiaji Makao Makuu)