Visitors

IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA UHAMIAJI HABARI BLOGU KARIBU KWENYE BLOG RASMI YA IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA TUNAKULETEA MATUKIO YANAYOTOKEA KILA SIKU KATIKA IDARA YA UHAMIAJI TAFADHALI TUNAOMBA TUFUATILIE PIA KATIKA MITANDAO YETU YA KIJAMII

23 Februari 2019

MICHEZO YA MAJESHI YAFUNGULIWA RASMI UWANJA WA UHURU JIJINI DAR ES SALAAM.

Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mheshimiwa Balozi Seif Iddi leo tarehe 23 Februari 2019, amefungua Mashindano ya Majeshi ya Tanzania, Uwanja wa Uhuru, Temeke jijini Dar es salaam, ambapo Timu za soka (wanaume) JKT na Ngome ndizo zilizofungua dimba la michezo hii.

Mashindano haya yaliyoanza leo yanatarajiwa kufikia tamati tarehe 8 Machi 2019, yanahusisha Vyombo vyote vya Ulinzi na Usalama nchini ambavyo ni JWTZ, JKT, Polisi, Magereza, Uhamiaji, Zimamoto na Vikosi Maalumu kutoka Zanzibar.
Michezo hi itashirikisha wanamichezo wa soka (wanaume), ngumi (wanaume), Netiboli (Wanawake), Mpira wa Mikono, Wavu, Kikapu na kulenga shabaha zitashirikisha wanaume na wanawake.


22 Februari 2019

KAMISHNA JENERALI WA UHAMIAJI ATEMBELEA KAMBI YA WANAMICHEZO WA UHAMIAJI CHUO CHA MAGEREZA UKONGA JIJINI DAR ES SALAAM

Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Peter Makakala leo tarehe 22 Februari, 2019 amefanya ziara ya kuwatembela Wachezaji wa Timu za Mpira wa Miguu na Kikapu walioweka kambi katika Chuo cha Magereza Ukonga jijini Dar es salaam.

Lengo la ziara hiyo ni kupata taarifa ya maandalizi, kukagua timu hizo na kuwatia hamasa katika kuelekea katika Mashindano ya Majeshi yatakayoanza kutimua vumbi kesho Jumamosi Februari 23. Michezo hiyo ya Majeshi hufanyika kila mwaka na huandaliwa na Baraza la Michezo ya Majeshi Tanzania (BAMMATA).

Akitoa taarifa ya Maandalizi na hali za wachezaji, Mwenyekiti wa BAMMATA Kanda ya Uhamiaji Naibu Kamishna wa Uhamiaji Nasra Jumaa alimweleza Kamishna Jenerali kuwa wachezaji wote wako katika hali nzuri na wana ari ya kushindana.

“Afande Kamishna Jenerali tunashukuru kwa ujio wako hapa na napenda kukujulisha kuwa wachezaji wako katika hali nzuri, wana ari kubwa na wako tayari kuiletea ushindi na heshima idara yetu ya uhamiaji. Tunakuahidi ushindi tu” Alisema Naibu Kamishna Nasra.

Naye Mwalimu wa Timu ya Mpira wa Miguu ya Uhamiaji maarufu kama Kimbunga FC, Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji Wahid Mmanga akitoa taarifa kuhusu timu yake alisema kwamba wako tayari kupambana na kuleta ushindi dhidi ya timu nyingine za Majeshi kwani safari hii hawatokubali kuwa wasindikizaji.

Afande sie tumekuja kucheza ili tushinde, miaka iliyopita timu kutoka majeshi mengine walikuwa wakitumia wachezaji wa Timu zao ambazo ziko Ligi Kuu lakini kwa utaratibu mpya mwaka huu hakuna kutumia wachezaji wa timu za majeshi zilizo Ligi Kuu ya soka Tanzania hivyo tuna uhakika wa kuchukua kikombe” Alieleza Naibu Kamishna Mmanga.

Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Makakala alieleza kuridhishwa na maandalizi ya timu na kuwatakia wachezaji kila la kheri kwenye Mashindano hayo. “Nimefurahishwa na maandalizi, mnaonekana kweli mna ari na hamasa ya ushindi. Naomba mkacheze ili kuiletea heshima idara yetu, mimi na watumishi wote wa Uhamiaji tuko pamoja nanyi na tutawashangilia kila mnapocheza. Hii michezo inasaidia sisi kama jeshi la uhamiaji kujenga mahusiano mazuri na majeshi mengine ya nchi yetu, pia ni faida kwenu wachezaji kwani inawajengea afya bora kwa mazoezi mnayofanya. Niwatakie kila la kheri” .

Michezo ya Majeshi kwa mwaka huu itashirikisha timu za wachezaji wa Mpira wa Miguu, Kikapu, Kuvuta Kamba, Kulenga shabaha na Riadha. Michezo hiyo itafunguliwa rasmi kesho Jumamosi saa nne asubuhi katika Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es salaam.


Wachezaji wa Timu ya Mpira wa Miguu ya Uhamiaji 'Kimbunga FC' wakipasha mwili katika Uwanja wa Chuo cha Magereza Ukonga jijini Dar es salaam walipoweka kambi yao tayari kuanza michezo ya Majeshi.
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dokta Anna Makakala akiingia Uwanja wa Chuo cha Magereza Ukonga kukagua timu ya wanamichezo wa Uhamiaji watakaoshiriki Mashindano ya Majeshi

Kamishna Jenerali wa Uhamiaji akisikiliza ripoti ya Kambi ya wachezaji wa Timu za Mpira wa Miguu na Kikapu kutoka kwa Naibu Kamishna wa Uhamiaji Nasra Jumaa

Kamishna Jenerali wa Uhamiaji akiongea na Wachezaji wa timu ya Uhamiaji

Mwalimu wa Tmu ya Kimbunga FC Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji Wahid Mmanga akitoa taarifa ya timu yake  kwa Kamishna Jenerali
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji akiagana na Maafisa Magereza na Uhamiaji mara baada ya ziara yake kukagua kambini hapo

15 Februari 2019

KAMISHNA JENERALI WA UHAMIAJI AKAGUA VIPENYO VINAVYOTUMIWA NA WAHAMIAJI HARAMU KATIKA WILAYA YA BAGAMOYOKamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Peter Makakala amefanya ziara ya kikazi katika Mkoa wa Pwani kwa lengo la kutambua vipenyo vinavyotumiwa na wahamiaji haramu kuingia hapa nchini. Akiwa katika Mkoa wa Pwani, amefanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Pwani, Mhe. Mhandisi, Evarist Ndikilo ambaye alimueleza kwamba wamejipanga katika kupambana na wahamiaji haramu katika Mkoa huo.

"Kuna mtandao mkubwa nchi nzima ambao unajihusisha na biashara haramu ya usafirishaji na magendo ya binadamu, hivyo basi hatuna budi kuvishirikisha vyombo vyetu vyote vya ulinzi na usalama katika kuhakikisha kuwa wale wote wanaojihusisha na vitendo hivi viovu wanasakwa na kushughulikiwa kwa mujibu wa sharia,” alisema Mhe. Ndikilo.

Aidha, katika taarifa yake, Mhe. Ndikilo alieleza kuwa Mkoa wa Pwani una urefu wa zaidi ya Kilometa 1300 katika mwambao wa bahari na una bandari bubu 39 zinazotumika na wahamiaji haramu kuingia nchini.

Pia Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, ametembelea Wilaya ya Bagamoyo na kukutana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ambapo, Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Zainabu Kawawa   alimueleza kuwa Wilaya hiyo ina jumla ya Vipenyo 19, pamoja na pori kubwa la Ruvu ambalo hutumiwa na wahamiaji haramu kuingia nchini.

Mhe. Mkuu wa Wilaya alivitaja baadhi ya vipenyo vinavyotumiwa na wahamiaji haramu kuingia nchini kuwa ni pamoja na Kaole, Mbegani, Mlingotini, Changwahela, Gwaza na Kondo. Hata hivyo, alimueleza kuwa, Kamati ya Ulinzi na Usalama imejipanga kufanya doria na misako maalum (special operations) za mara kwa mara ili kukabiliana na uhalifu katika katika maeneo hayo.

Aidha, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji aliishukuru Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya Bagamoyo kwa ushirikiano wanaouonesha kwa Idara ya Uhamiaji katika kupambana na kudhibiti wahamiaji haramu nchini.

Akizungumza na Wananchi katika Kijiji cha Ruvu Darajani, Kata ya Bigwaza, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji amewataka wananchi kutoa taarifa za uwepo wa wahamiaji haramu kwenye maeneo yao na kuacha tabia ya kuwahifadhi wahamiaji hao; kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria na huhatarisha amani na usalama wa nchi yetu. Pia amewataka wnanchi kuwa makini na wahamiaji haramu kwani baadhi yao wanatoka kwenye nchi zenye machafuko hivyo, inawezekana wakawa wamekimbia na silaha.

“Napenda kutoa wito kwa Madereva wa vyombo vya moto kama vile magari binafsi, mabasi ya abiria, malori pamoja na bodaboda waache kuwasafirisha wahamiaji haramu, vitendo hivyo ni kosa kwa Mujibu wa Sheria ya Uhamiaji Sura ya 54, Rejeo la Mwaka 2016 pamoja na Kanuni zake. Ukithibitika kutenda makosa hayo adhabu yake ni Kifungo cha Miaka ishirini (20) au kulipa faini isiyozidi Shilingi Milioni ishirini (20) au vyote kwa pamoja,” alisisitiza Kamishna Jenerali wa Uhamiaji.

Pia Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, aliwataka Watumishi wa Idara ya Uhamiaji pamoja na Maafisa na askari wanaoshiriki katika misako na doria za wahamiaji haramu kufanya kazi kwa weledi na bidii na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.

Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Peter Makakala akiwa na baadhi ya wajumbe Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Pwani wakati akielekea katika moja ya Bandari bubu - Bagamoyo a kuakagua Vipenyo vinavyotumiwa na wahamiaji haramu kuingia nchini

Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Peter Makakala akiwa na Mwenyeji wake Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mhe. Zainabu Kawawa wakati alipomtembelea Ofisini kwake Bagamoyo

Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Peter Makakala akizungumza na Wazee wenyeji katika moja ya maeneo yanayopitisha Wahamiaji haramu

Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Peter Makakala akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Ruvu Darajani, Kata ya Bigwaza, Wilayani Bagamoyo.

14 Februari 2019

RAIA 8 WA ETHIOPIA WAZIKWA MAKABURI YA MANISPAA YA JIJI LA TANGA LEO FEBRUARI 14, 2019.

Raia wanane wa Ethipoia waliofariki tarehe 22 Oktoba 2018 hatimaye wamezikwa jijini Tanga katika makaburi ya Manispaa maafuru kwa jina la 'Neema'.

Mkuu wa Wilaya ya Tanga mjini Mhe. Thobias Mwilapwa aliongoza Mazishi hayo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, ambapo Balozi wa Ethiopia, viongozi wa dini pamoja na wanachi wa kawaida walihudhuria.

Balozi wa Ethiopia nchini Tanzania Mhe. Yonas Yosef Sanbe ameishukuru Serikali ya Tanzania, Uongozi wa Mkoa wa Tanga, Idara ya Uhamiaji, Hospitali ya Rufaa mkoa Tanga na Taasisi za kidini mkoa wa Tanga kwa ushirikiano waliouonesha kufanikisha mazishi ya raia hao. Pia alisema kuwa kila nci inao wajibu wa kupambana na wahamiaji haramu hivyo anapongeza juhudi za serikali katika kuthibiti wahamiaji haramu nchini.

Ibada ya kuwaombea marehemu iliendeshwa na viongozi wa dini kutoka madhehebu ya kikristo na kiislamu, ambapo Kanisa la KKKT iliwakilishwa na na Mchungaji Warehema Chamshana, Kanisa la Waadventista Wasabato alikuwepo Mwinjilisti Elitumaini Mchomvu na kwa upande wa Waislamu aliyewaombea marehemu ni Maalim Juma bin Salum wa wa Msikiti wa Masjid Sayyidna Bilal Rabbah katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga

Ikumbukwe kwamba, mnamo tarehe 22 Oktoba mwaka jana, waethipoia hao waliokotwa kando ya bahari ya Hindi nje kidogo ya jiji la Tanga wakiwa wamekufa. Baada ya uchunguzi wa kina, Idara ya Uhamiaji mkoani Tanga ilibaini kuwa walikuwa raia wa Ethiopia waliokuwa wakisafirishwa kwa njia ya haramu kuelekea Afrika ya Kusini