Visitors

IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA UHAMIAJI HABARI BLOGU KARIBU KWENYE BLOG RASMI YA IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA TUNAKULETEA MATUKIO YANAYOTOKEA KILA SIKU KATIKA IDARA YA UHAMIAJI TAFADHALI TUNAOMBA TUFUATILIE PIA KATIKA MITANDAO YETU YA KIJAMII

24 Februari 2018

UHAMIAJI YASHIRIKI USAFI NA KUTOA ZAWADI KWA WANAFUNZI KATIKA SHULE YA MSINGI MATUMAINI JIJINI DAR ES SALAAM.

Idara ya Uhamiaji imeshiriki zoezi la kufanya usafi katika shule ya msingi Matumaini iliyoko Kurasini jijini Dar es salaam. Shule hiyo inayomilikiwa na Jeshi la Wokovu inasomesha wanafunzi wenye mahitaji maalum toka Mikoa mbalimbali nchini na hata nje ya nchi.

Akiongea kwa niaba ya Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Kamishna wa Utawala na Fedha, Edward Peter Chogero ambaye ndiye aliyeongoza Maafisa, Askari na Watumishi wa kada nyingine wa Idara hiyo, alisema zoezi hilo ni mwendelezo wa utekelezaji wa agizo la Serikali la kufanya usafi katika kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi. 

Aidha, Idara ya Uhamiaji ilitoa zawadi mbalimbali kwa wanafunzi wa shule hiyo walio na mahitaji maalum ikiwa ni sehemu ya kuwafariji na kuwaonesha upendo ili wajisikie ni sawa na watu wengine katika jamii.

Akiongea kwa niaba ya Uongozi, Luteni Thomas Sinana ambaye ni Mkurugenzi wa Shule hiyo aliishukuru na kuipongeza Idara ya Uhamiaji kwa moyo wa upendo waliouonesha kwa wanafunzi hao wenye mahitaji maalum, kwa kushiriki kwao katika kufanya usafi katika maeneo mbalimbali ya shule hiyo pamoja na kutoa zawadi mbali mbali kwa watoto hao.

Luteni Sinana alisema “kituo kina mahitaji mengi japo kuwa tunashirikiana na Serikali kutoa elimu kwa vijana hawa kuanzia darasa la kwanza mpaka la saba ila watoto wote waliopo hapa wana mahitaji maalumu kutokana na ulemavu wao hivyo tunapopata vifaa kama hivi vinatusaidia sana kwenye kituo chetu” .

Mwisho watoto hao walipata nafasi ya kuonyesha vipaji vyao mbalimbali ikiwa ni pamoja na kazi za mikono wanazotengeza wenyewe, kuimba, kucheza na kuigiza.


Kamishna wa Uhamiaji (Utawala na Fedha) Edward Chogero akikabidhi zawadi kwa Kiranja Mkuu wa Shule ya Matumaini Ernest Thomas mara baada ya zoezi la kufanya usafi kumalizika shuleni hapo.

Maafisa Uhamiaji wakifanya usafi katika Shule ya Msingi Matumaini leo Jumamosi Februari 24, 2018
Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Matumaini wakifuatilia tukio la kukabidhiwa zawadi

Kamishna wa Uhamiaji (Utawala na Fedha) akiwa na Mkurugenzi wa Shule ya Matumaini Luteni Thomas Sinana

Kikundi cha Sanaa cha Shule ya Msingi Matumaini kikitumbuiza wakati wa zoezi la utoaji zawadi shuleni hapo
Wanafunzi wa Shule ya Msingi Matumaini wakitoa burudani kwa Maafisa Uhamiaji waliofika shuleni hapo kwa ajili ya kushiriki usafi na kutoa zawadi

Wanafunzi wakisoma vipeperushi vyenye kuelezea maana ya Uhamiaji Mtandao

Kamishna Edward Chogero akiangalia vitu mbalimbali vinavyotengezwa na wanafunzi wa shule ya msingi Matumaini

Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Matumaini ambaye pia ndiye kaka Mkuu wa shule hiyo akitoa shukrani kwa niaba ya wanafunzi wenzake mara baada ya kukabidhiwa zawadi hizo.

Maafisa Uhamiaji wakiwasalimia wanafunzi wa Shule ya Matumaini 21 Februari 2018

Watuhumiwa wa Uhamiaji Haramu 48 wakamatwa Kampala International University (KIU) Tawi la Dar Es Salaam.

Idara ya Uhamiaji kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu ilifanya ukaguzi wa kushtukiza katika chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala na kufanikiwa kuwakamata Watuhumiwa 48, siku ya Jumanne ya tarehe 20 Februari 2018.


Watuhumiwa hao ni Wahadhiri, Wanafunzi na Wafanyakazi wa kada mbalimbali. Pia katika tukio hilo wamekamatwa Watanzania (9) kwa kosa la kuwahifadhi na kutokutoa ushirikiano kwa Maafisa Uhamiaji kinyume na sheria ya Uhamiaji.

Msemaji Mkuu wa Idara Uhamiaji Mrakibu wa Uhamiaji Ally Mtanda alifafanua kuwa Watuhumiwa waliokamatwa kwa mchanganuo wa uraia wao ni kama ifuatavyo, Uganda (30), Nigeria (5), Kenya (3) na Congo D.R (1).

Tukio hili ni muendelezo wa doria na misako inayofanywa na Idara kwa lengo la kuwasaka na kuwakamata Wahamiaji haramu ambapo awali walikamatwa Watuhumiwa wengine raia wa Nigeria (5) kwa kosa la kuishi nchini bila Vibali vya Ukaazi na kujishughulisha na biashara haramu ya madawa ya kulevya na raia watatu (3) wa Tanzania kwa kushirikiana na Wanaijeria hao.

Baada ya kuhojiwa ilibainika kuwa mmoja wa watuhumiwa raia wa Nigeria ni mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala tawi la Dar Es Salaam kilichopo Gongolamboto.

Watuhumiwa wote wanaendelea kuhojiwa na mara baada ya kukamilika kwa taratibu zote watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.


Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Peter Makakala akiongea na waandishi wa Habari mara baada ya timu yake kuwakamata wahamiaji haramu zaidi ya 40 katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala.

Kaimu Kamishna wa Udhibiti na Usimamizi wa Mipaka  Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji Hosea Kagimbo akiwa na Mheshimiwa Waziri wa Elimu Prof. Ndaliachako wakikagua vibali vya watumishi raia wa kigeni katika Chuo cha Kimataifa cha Kampala kilichopo Gongolamboto jijini Dar es salaam siku ya Jumanne tarehe 20 Februari 2018.

Kamishna Jenerali wa Uhamiaji pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Elimu wakijibu maswali ya Waandishi wa Habari katika chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala.
Baadhi ya Watuhumiwa wakiwa ndani ndani ya  Basi la Idara ya Uhamiaji tayari kwa kupelekwa kwenye ofisi za Uhamiaji kwa mahojiano zaidi.14 Februari 2018

TAARIFA KWA UMMA

KAMISHNA JENERALI WA UHAMIAJI ANAPENDA KUUTANGAZIA UMMA KUWA, WAFUATAO HAPA CHINI SI WAFANYAKAZI KATIKA IDARA YA UHAMIAJI.

BAADA YA TANGAZO HILI, IDARA YA UHAMIAJI HAITAHUSIKA AMA KUTAMBUA HUDUMA YOYOTE ITAKAYOTOLEWA NA WATAJWA HAPA CHINI.  13 Februari 2018

Mwaka mmoja kuongoza Idara ya Uhamiaji

Mwaka Mmoja wa Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Peter Makakala kuongoza Idara ya Uhamiaji , Mengi amefanya katika kuboresha utendaji kazi wa Idara hii nyeti nchini.


10 Februari 2018

Kamishna Jenerali wa Uhamiaji akagua vituo vya mpakani mkoani Kilimanjaro

Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala  amefanya ziara ya siku moja katika vituo vya mpakani mkoa wa Kilimanjaro ikiwa na lengo kukagua utendaji kazi wa maafisa na askari wa Uhamiaji katika vituo hivyo.

Akiwa kituo cha Holili alikagua mpaka na kuongea na watumishi wa Idara ya Uhamiaji kituoni hapo na kuwasisitiza kufanya kazi kwa weledi na juhudi pia kujiepusha na vitendo vya rushwa. Pia aliwataka kuzidisha doria na ukaguzi maeneo ya mipakani ili kudhibiti uingiaji wa wahamiaji haramu.

Katika kituo cha Tarakea, Kamishna Jenerali alikagua mpaka na utendaji kazi katika kituo hicho na baadaye kuongea na watumishi  wa uhamiaji na vyombo vingine vya serikali vinavyofanya kazi katika mpaka huo na kuwataka kuwa na ushirikiano katika kutekeleza majukumu yao mpakani hapo.

Pia Kamishna Jenerali alisisitiza watumishi wa uhamiaji kufanya kazi kwa weledi na kufuata sheria za nchi pia kujiepusha na vitendo vya rushwa, pia aliwataka kuongeza kasi ya kufanya doria maeneo yanayodhaniwa kuwa ni vipenyo vya wahamiaji haramu kuingia nchini.

Akiwa katika mpaka wa Rongai, Kamishna Jenerali aliongea na wananchi na kuwataka kutoa ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na usalama katika ulinzi wa mpaka huo na kuwasisisitiza kutoa taarifa za wahamiaji haramu badala ya kukaa kimya na kuangalia tu kwani wananchi waishio mipakani wanalo jukumu kubwa katika ulinzi wa mipaka katika maeneo wanayoishi,

Akiwa mjini Moshi, Kamishna Jenerali alifungua mafunzo ya Ukaguzi wa nyaraka na kujenga uwezo  kwa maafisa  wa vyombo ya ulinzi na usalama katika masula ya Ugaidi yaliyoanza tarehe 8 Februari 2018 katika Chuo cha Uhamiaji cha Kikanda (TRITA) mjini Moshi.

Kamishna Jenerali wa Uhamiaji akipata maelezo kutoka kwa Mfawidhi wa Kituo cha Uhamiaji katika mpaka wa Tarakea
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji akisalimiana na Maafisa na Askari wa Uhamiaji katika kituo cha Uhamiaji Holili wakati wa ziara yake katika kituo hicho
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa Mafunzo ya Ukaguzi wa Nyaraka kwa Maafisa kutoka vyombo vya ulinzi na usalama hapa nchini katika chuo cha Uhamiaji cha Kikanda (TRITA) mjni Moshi.
Mkuu wa Chuo cha Kikanda cha Uhamiaji (TRITA) Kamishna wa Uhamiaji Kitinusa akimsikiliza Kamishna Jenerali wa Uhamiaji kabla ya kuanza kwa mafunzo ya Ukaguzi wa Nyaraka kwa Maafisa kutoka Vyombo vya Ulinzi na Usalama

Picha ya pamoja kati ya Kamishna Jenerali wa Uhamiaji (mwenye koti jekundu katikati) na Washiriki wa Mafunzo ya Usalama wa Nyaraka na Kujenga uwezo katika Masuala ya Usalama juu ya Ugaidi katika Chuo cha Kikanda cha Uhamiaji (TRITA) mjini Mosji Mkoani Kilimanjaro siku ya tarehe 8 Februari 2018

Msemaji wa Idara ya Uhamiaji (katikati), Afisa Uhusiano wa Chuo cha Uhamiaji cha Kikanda, na Mfawidhi wa Kitengo cha Mafunzo katika Idara ya Uhamiaji Mrakibu Msaidizi wa Uhamiaji Ignatius Mgana wakati wa ziara ya Kamishna Jenerali wa Uhamiaji katika vituo vya mpakani katika mkoa wa Kilimanjaro
Msemaji wa Idara Mrakibu wa Uhamiaji Ally Mtanda akiwa na Afisa Uhusiano wa Chuo cha Uhamiaji cha Kikanda (TRITA) Mkaguzi wa Uhamiaji Leslie Mbotta

09 Februari 2018

Fahamu kuhusu Uhamiaji Mtandao na Pasipoti ya Kielektroniki.

Uhamiaji Mtandao ni Nini?
Uhamiaji Mtandao (e-Immigration) ni muunganiko wa Mifumo mbalimbali ambayo imesanifiwa kufanya kazi kwa pamoja na kutoa taarifa kwa watumiaji na wadau wa huduma za kiuhamiaji. 

Lengo la Uhamiaji Mtandao
Lengo kuu la Uhamiaji Mtandao ni Kuimarisha Ulinzi na Usalama wa Nchi yetu, Kudhibiti ukusanyaji wa maduhuli ya serikali na kuimarisha utoaji wa huduma za kiuhamiaji kwa raia na wageni wanaoingia na kuishi hapa nchini kwa madhumuni mbalimbali.

Mfumo wa Uhamiaji Mtandao, utawezesha;

Idara ya Uhamiaji kutoa viza kielektroniki (e-Visa); ambapo mgeni ataweza kuwasilisha ombi lake na kupata majibu kwa njia ya kielektroniki. Mfumo huo pia utasaidia Serikali kupata taarifa sahihi za malipo ya viza na kuchagiza ukuaji wa Sekta ya Utalii nchini.

Mfumo wa Udhibiti na Usimamizi wa Mipaka Kielektroni (e-Border Management), Mfumo utasaidia kudhibiti na kuwezesha uingiaji na utokaji wa raia na wageni nchini, Sambamba na hilo, Mfumo utasaidia kuchuja wageni wasiotakiwa kuingia nchini na hivyo kuimarisha ulinzi hususan katika maeneo ya mipakani na kuzuia ongezeko la wahamiaji haramu nchini.

Mfumo wa utoaji wa Vibali vya Ukaazi Kielektroniki (e-Residence Permit), Mfumo huu utasaidia kuboresha usimamizi wa utoaji vibali kwani mwombaji atawasilisha maombi yake kwa njia ya kielektroniki. Hii itasaidia kukuza Sekta ya Uwekezaji nchini kwa maendeleo ya uchumi wa Nchi yetu.

Mfumo wa Utoaji wa Pasipoti kielektroniki (e-Passport); Mfumo huu ambao ndio wa kwanza katika utekelezaji wa Mradi wa Uhamiaji Mtandao, utawawezesha waombaji wa huduma ya Pasipoti kuwasilisha maombi yao kwa njia ya kielektroniki (Online Passport Application) kutoka mahali popote walipo, na kuweza kufuatilia (Track) maombi hayo kielektroniki.


Pasipoti hii mpya ya Kielektroniki imesheheni sifa zifuatazo:

1.  Imewekwa Kifaa maalum chenye uwezo wa kutunza taarifa za mmiliki wa pasipoti “Micro-Chip” na hivyo kufanya suala la utunzaji wa Usalama za Pasipoti hizi kuwa wa hali ya juu
2.  Vile vile uwepo wa “Micro-Chip” katika Pasipoti ya kielektroniki, kunaifanya pasipoti hii kuwa ngumu kuibiwa au kutumiwa na wahalifu au watu wanaojaribu kuficha utambulisho

3.  Vile vile uwepo wa “Micro Chip” katika pasipoti ya kielektroniki, kunaifanya pasipoti ya hii kuwa ngumu kuibiwa au kutumiwa na wahalifu au watu wanaojaribu kuficha utambulisho wao kwa kutumia pasipoti zisizo zao.

4.    Pasipoti hiyo ina viwango vilivyopendekezwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia Usafiri wa Anga (ICAO).

5.    Pasipoti inatumia mfumo bora wa Utunzaji wa taarifa za mmiliki wa Pasipoti kielektroniki, ambao hurahisisha utunzaji wa taarifa za mhusika, na kuondoaa urasimu wa ufuatiliaji wa kumbukumbu za mmiliki pale anapotaka huduma nyengine

6. Pasipoti hiyo ina uwezo wa kutunza kumbukumbu za kibailojia (Biometric features)

 Faida za Pasipoti Mpya ya Kielektroniki
Pasipoti hii mpya ina uwezo wa kuhifadhiwa katika Simu ya Kisasa (Smart Phone) na hivyo kumuwezesha mwenye nayo kupata msaada wa Hati ya Dharura katika Ubalozi wowote wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, pale anapopotelewa na pasipoti hiyo awapo nje ya nchi ili aweze kurudi nyumbani.

Aidha, Pasipoti mpya ya Tanzania ya Kielektroniki ina muonekano unaofanana na pasipoti za nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na faida zake ni nyingi;-

(i)      Utambulisho wa pamoja wa raia wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanapokuwa nchi za nje na hivyo kurahisisha kupata msaada wa huduma za kikonsula (consular services) inapobidi. Kwa mfano, kupata msaada wa kurejeshwa nchini kupitia balozi za nchi wanachama wakati wa dharura, ikiwa sehemu husika haina ubalozi wa Tanzania.

(ii)          Raia wa nchi wanachama kutambuana wanapokuwa nje ya nchi na hivyo kujenga umoja wa kikanda kwa ngazi ya raia, wanapokuwa nje, kwani ni rahisi kupata msaada kwa jirani kuliko mtu wa mbali.


Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akiweka saini yake kwenye kifaa cha kusaini cha kielektoniki kabla y akupatiwa pasipoti yake ya kielektroniki.

Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akionesha pasipoti yake baada ya kukabidhiwa na Mheshimiwa waziri wa Mambo ya ndani ya nchi Dkt. Mwigulu Mchemba.

Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu akionesha pasipoti yake ya kielektroniki wakati wa uzinduzi wa pasipoti hizo kwenye Ofisi za Uhamiaji Makao Makuu, Kurasini jijini Dar es salaam.


07 Februari 2018

HATUA ZA UJAZAJI FOMU YA MAOMBI YA PASIPOTI KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI (MTANDAO).


HATUA ZA UJAZAJI FOMU YA MAOMBI YA PASIPOTI KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI (MTANDAO).

1.   INGIA KATIKA TOVUTI YA IDARA: www.immigration.go.tz KISHA NENDA KATIKA KITUFE CHA e-SERVICES
2.   CHAGUA PASSPORT APPLICATION FORM;
3.   CHAGUA OMBI JIPYA;
4.   TIKI KIBOKSI KUKUBALIANA NA MAELEKEZO;
5.   JAZA TAARIFA ZAKO KWA UKAMILIFU UKIFUATA MAELEKEZO NA MPANGILIO (FORMAT) KATIKA KILA KIPENGELE;
NB:
BAADA YA MWOMBAJI KUKAMILISHA KUJAZA TAARIFA ZAKE, ATAFAHAMISHWA YA KWAMBA USAJILI UMEKAMILIKA NA KUPATIWA NAMBA YA OMBI, AMBAYO NI MUHIMU AIANDIKE PEMBENI NA KUIHIFADHI KWA KUMBUKUMBU ZA BAADAE. KISHA ATAPEWA NAMBA YA KUMBUKUMBU YA MALIPO (CONTROL NUMBER) NA KUTAKIWA KWENDA KULIPIA MALIPO YA AWALI (ADVANCE FEE) YA TSH 20,000.

BAADA YA KUKAMILISHA USAJILI, NA KUPATIWA NAMBA YA OMBI NA NAMBA YA KUMBUKUMBU (CONTROL NUMBER), UKURASA UTAONEKANA KAMA IFUATAVYO:
INGIA KWENYE MENU YA M-PESA/TIGOPESA (*150*00#/*150*01#)
1. Bonyeza Namba 4 (Lipa kwa M-Pesa) - VODA
2. Bonyeza Namba 4 (Kulipia Bili) - TIGO
Kisha Weka/Ingiza Namba ya Kampuni
3. Ingiza Namba (888999)
4. Ingiza kumbukumbu Namba(Ingiza Control Number inayoanzia na 99109…….)
5. Ingiza kiasi (kama ulivyo elekezwa Mfano: 20,000 nk.)
6. Utapata Maelezo kuwa unalipa pesa NMB
7. Ingiza Namba ya Siri
8. Hakiki
9. Utapata Meseji toka M-Pesa/Tigopesa kama muamala umekubalika;

Utapata meseji kutoka kwenye mfumo Namba 15200
kama muamala umekubalika;

10.       Mteja atatakiwa kurudi katika OMBI LINALOENDELEA:
11.       Kisha ataingiza NAMBA YA OMBI/SIMU na NAMBA YA RISITI

Na hapo ataweza kupakua Fomu yake ya Maombi
Ataiwasilisha Fomu hiyo katika Ofisi ya Uhamiaji Makao makuu au Afisi Kuu Zanzibar
1.  Jaza fomu ya malipo ya kielectroniki;
    2. Fuata maelekezo kama yanavyojieleza kwenye fomu;
    3. Utapata meseji toka benki;
           Utapata meseji toka kwenye mfumo Namba 15200  
     kama muamala umekubalika.

05 Februari 2018

Wanasiasa, Wafanyabiashara na Watu Maarufu wafika Uhamiaji kujipatia pasipoti za kielektroniki

Baada ya Idara ya Uhamiaji kuanza rasmi kutoa pasipoti za kielektroniki, Baadhi ya Wafanyabiashara na wanasiasa wakubwa nchini wameanza kufika Makao Makuu ya Uhamiaji kupata pasipoti hizo. Miongoni mwa waliofika kujipatia pasipoti ni Wafanyabiashara maarufu nchini Mzee Reginald Mengi akiwa na mkewe pamoja na Mzee Said Salim Bakhresa. 

Kwa upande wa wanasiasa, Waziri Mkuu Mstaafu Mh. Edward Lowassa alifungua pazia kwa wanasiasa waliofika Uhamiaji Makao makuu kujipatia pasipoti hizo za kisasa zenye usalama wa hali ya juu.

Akiongea mara baada ya kupatiwa pasipoti yake, Mzee Mengi alisema amefurahishwa na mabadiliko makubwa ya kiutendaji ambapo amefanya maombi na kupatiwa pasi ndani ya siku moja kitu ambacho awali hakikuwepo.

''Hii ni hatua kubwa sana kwa kweli, Uhamiaji mmejitahidi mno, mimi na mke wangu tumefanya maombi leo na kupata pasipoti zetu, hongereni sana kwa hili" alisema Mzee Mengi ambaye aliambatana na Mkewe Bi. Jacqueline.

Naye Mheshimiwa Lowassa alisifu juhudi zinazofanywa na Idara  ya Uhamiaji kwenye dhana ya Uhamiaji Mtandao ambapo ampongeza Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala kwa juhudi zake za kuifanaya Idara ya Uhamiaji kwenda sambamba na tekinolojia.


01 Februari 2018

TAARIFA KWA UMMATAARIFA KWA UMMA:

UFAFANUZI JUU YA “UZUSHI” UNAOENEA KWENYE TOVUTI NA MITANDAO YA KIJAMII KUHUSU IDARA YA UHAMIAJI KUTANGAZA NAFASI ZA KAZI.
Katika siku za hivi karibuni, kumekuwepo na uvumi unaoenezwa kupitia baadhi ya tovuti na mitandao ya kijamii kuhusu kutangazwa kwa nafasi za ajira na Idara ya Uhamiaji kwa ngazi ya Mkaguzi Msaidizi, Koplo na Konstebo. Tunaamini uvumi huo unaenezwa na watu au kikundi cha watu kwa nia ya kujipatia maslahi yao binafsi au kwa malengo wanayoyafahamu wao.

Kufuatia kuwepo kwa taarifa hizo, Idara ya Uhamiaji inapenda kutoa ufafanuzi ufuatao:
  1. Idara ya Uhamiaji haijatangaza nafasi zozote za ajira katika kipindi cha hivi karibuni, hivyo tunawaomba wananchi wasirubuniwe au kushawishiwa na mtu yoyote kutoa kitu chochote ili waweze kusaidiwa kupata kazi Idara ya Uhamiaji.
  2. Taarifa za kutangazwa nafasi za kazi zilizotolewa kupitia blogu husika na Mitandao ya kijamii si za kweli, bali ni uzushi uliofanywa na watu au kikundi cha watu kwa malengo wanayoyajua wao.

  1. Idara ya Uhamiaji, kama Taasisi ya Serikali hutangaza nafasi za ajira  kwa uwazi kupitia Magazeti, Televisheni na Tovuti yake ambayo niwww.immigration.go.tz

  1. Idara inalaani na kukemea vikali watu au kikundi cha watu kinachotoa taarifa za upotoshaji kuhusu Idara kutangaza nafasi za kazi kama ambavyo imeripotiwa kwenye baadhi ya tovuti na mitandao ya kijamii.

Imetolewa na;
KITENGO CHA UHUSIANO,
MAKAO MAKUU, DAR ES SALAAM.
TAREHE: 01 FEBRUARI, 2018