Visitors

IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA UHAMIAJI HABARI BLOGU KARIBU KWENYE BLOG RASMI YA IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA TUNAKULETEA MATUKIO YANAYOTOKEA KILA SIKU KATIKA IDARA YA UHAMIAJI TAFADHALI TUNAOMBA TUFUATILIE PIA KATIKA MITANDAO YETU YA KIJAMII

09 Februari 2018

Fahamu kuhusu Uhamiaji Mtandao na Pasipoti ya Kielektroniki.

Uhamiaji Mtandao ni Nini?
Uhamiaji Mtandao (e-Immigration) ni muunganiko wa Mifumo mbalimbali ambayo imesanifiwa kufanya kazi kwa pamoja na kutoa taarifa kwa watumiaji na wadau wa huduma za kiuhamiaji. 

Lengo la Uhamiaji Mtandao
Lengo kuu la Uhamiaji Mtandao ni Kuimarisha Ulinzi na Usalama wa Nchi yetu, Kudhibiti ukusanyaji wa maduhuli ya serikali na kuimarisha utoaji wa huduma za kiuhamiaji kwa raia na wageni wanaoingia na kuishi hapa nchini kwa madhumuni mbalimbali.

Mfumo wa Uhamiaji Mtandao, utawezesha;

Idara ya Uhamiaji kutoa viza kielektroniki (e-Visa); ambapo mgeni ataweza kuwasilisha ombi lake na kupata majibu kwa njia ya kielektroniki. Mfumo huo pia utasaidia Serikali kupata taarifa sahihi za malipo ya viza na kuchagiza ukuaji wa Sekta ya Utalii nchini.

Mfumo wa Udhibiti na Usimamizi wa Mipaka Kielektroni (e-Border Management), Mfumo utasaidia kudhibiti na kuwezesha uingiaji na utokaji wa raia na wageni nchini, Sambamba na hilo, Mfumo utasaidia kuchuja wageni wasiotakiwa kuingia nchini na hivyo kuimarisha ulinzi hususan katika maeneo ya mipakani na kuzuia ongezeko la wahamiaji haramu nchini.

Mfumo wa utoaji wa Vibali vya Ukaazi Kielektroniki (e-Residence Permit), Mfumo huu utasaidia kuboresha usimamizi wa utoaji vibali kwani mwombaji atawasilisha maombi yake kwa njia ya kielektroniki. Hii itasaidia kukuza Sekta ya Uwekezaji nchini kwa maendeleo ya uchumi wa Nchi yetu.

Mfumo wa Utoaji wa Pasipoti kielektroniki (e-Passport); Mfumo huu ambao ndio wa kwanza katika utekelezaji wa Mradi wa Uhamiaji Mtandao, utawawezesha waombaji wa huduma ya Pasipoti kuwasilisha maombi yao kwa njia ya kielektroniki (Online Passport Application) kutoka mahali popote walipo, na kuweza kufuatilia (Track) maombi hayo kielektroniki.


Pasipoti hii mpya ya Kielektroniki imesheheni sifa zifuatazo:

1.  Imewekwa Kifaa maalum chenye uwezo wa kutunza taarifa za mmiliki wa pasipoti “Micro-Chip” na hivyo kufanya suala la utunzaji wa Usalama za Pasipoti hizi kuwa wa hali ya juu
2.  Vile vile uwepo wa “Micro-Chip” katika Pasipoti ya kielektroniki, kunaifanya pasipoti hii kuwa ngumu kuibiwa au kutumiwa na wahalifu au watu wanaojaribu kuficha utambulisho

3.  Vile vile uwepo wa “Micro Chip” katika pasipoti ya kielektroniki, kunaifanya pasipoti ya hii kuwa ngumu kuibiwa au kutumiwa na wahalifu au watu wanaojaribu kuficha utambulisho wao kwa kutumia pasipoti zisizo zao.

4.    Pasipoti hiyo ina viwango vilivyopendekezwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia Usafiri wa Anga (ICAO).

5.    Pasipoti inatumia mfumo bora wa Utunzaji wa taarifa za mmiliki wa Pasipoti kielektroniki, ambao hurahisisha utunzaji wa taarifa za mhusika, na kuondoaa urasimu wa ufuatiliaji wa kumbukumbu za mmiliki pale anapotaka huduma nyengine

6. Pasipoti hiyo ina uwezo wa kutunza kumbukumbu za kibailojia (Biometric features)

 Faida za Pasipoti Mpya ya Kielektroniki
Pasipoti hii mpya ina uwezo wa kuhifadhiwa katika Simu ya Kisasa (Smart Phone) na hivyo kumuwezesha mwenye nayo kupata msaada wa Hati ya Dharura katika Ubalozi wowote wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, pale anapopotelewa na pasipoti hiyo awapo nje ya nchi ili aweze kurudi nyumbani.

Aidha, Pasipoti mpya ya Tanzania ya Kielektroniki ina muonekano unaofanana na pasipoti za nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na faida zake ni nyingi;-

(i)      Utambulisho wa pamoja wa raia wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanapokuwa nchi za nje na hivyo kurahisisha kupata msaada wa huduma za kikonsula (consular services) inapobidi. Kwa mfano, kupata msaada wa kurejeshwa nchini kupitia balozi za nchi wanachama wakati wa dharura, ikiwa sehemu husika haina ubalozi wa Tanzania.

(ii)          Raia wa nchi wanachama kutambuana wanapokuwa nje ya nchi na hivyo kujenga umoja wa kikanda kwa ngazi ya raia, wanapokuwa nje, kwani ni rahisi kupata msaada kwa jirani kuliko mtu wa mbali.


Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akiweka saini yake kwenye kifaa cha kusaini cha kielektoniki kabla y akupatiwa pasipoti yake ya kielektroniki.

Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akionesha pasipoti yake baada ya kukabidhiwa na Mheshimiwa waziri wa Mambo ya ndani ya nchi Dkt. Mwigulu Mchemba.

Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu akionesha pasipoti yake ya kielektroniki wakati wa uzinduzi wa pasipoti hizo kwenye Ofisi za Uhamiaji Makao Makuu, Kurasini jijini Dar es salaam.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni