Wakuu wa nchi
wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki mwezi Novemba 2013, waliamuru kila
nchi mwanachama ianze mchakato wa kutoa pasipoti mpya ya Afrika Mashariki.
Tarehe 02 machi 2016 Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na waheshimiwa
marais wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kilele cha
mkutano wao uliofanyika Arusha Tanzania, walikubaliana rasmi kuanza kutoa
pasipoti za kielekroniki (EA-eppt) ifikapo Januari 2017.
Idara ya Uhamiaji
Tanzania bila kuchelewa ilitekeleza kwa vitendo agizo hilo na kuwa nchi ya kwanza
kuanzisha pasipoti mpya zote za kielekroniki katika nchi wanachama wa Jumuiya
ya Afrika Mashariki.
Mnamo Januari 31,
2018 Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John
Pombe Magufuli alizindua rasmi mfumo wa utoaji huduma za uhamiaji mtandao (e-Immigration)
na hivyo kuifanya Tanzania kuanza nchi ya kwanza kutoa aina zote nne za Pasipoti
mpya ya kielektroniki yaani pasipoti ya kawaida, utumishi, kidiplomasia na
pasipoti Maalumu za Kidiplomasia kwa wakati mmoja.
Pasipoti hii ya
kisasa imekidhi viwango vya ubora vya kimataifa vinavyopendekezwa na shirika la
umoja wa mataifa linalosimamia usafiri wa anga (International civil aviation
organization-ICAO).
Machi, 2019 pasipoti
mpya ya Kielektroniki ya Tanzania iliibuka kidedea na kupata tuzo ya ubora
katika viwango vya kimataifa vya usalama na kuwa pasipoti bora katika ukanda wa
Ulaya, Mashariki ya Kati, na Afrika (Europe, Middle East and Afrika - EMEA)
Katika kipengele cha
utambulisho (National Identity) pasipoti hii imesanifiwa kwa kuzingatia
utamaduni wa Kitanzania na maliasili tulizonazo ambazo ni fahari ya nchi yetu.
Michoro iliyopo
katika pasipoti hiyo ni pamoja na wanyama, majengo ya kihistoria, matukio ya
kitaifa na nukuu za hamasa za hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere.
Kuhusu eneo la
usalama, Pasipoti hii ina kifaa maalumu chenye uwezo wa kutunza taarifa za
mmiliki wa pasipoti “Micro Chip” na hivyo kufanya suala la utunzaji wa usalama wa
pasipoti hizi kuwa wa hali ya juu zaidi.
Pasipoti hii ina
uwezo wa kutunza kumbukumbu za kibailojia (Biometric features) na alama za
usalama ambazo si rahisi kwa mtu yeyeote kuzibaini hivyo kuwa vigumu kughushiwa
na wahalifu au watu wanaojaribu kuficha utambulisho wao kwa kutumia pasipoti
zisizo kuwa zao.
Faida za pasipoti ya
kielektroniki (e-Passport) ni utambulisho wa pamoja wa raia wa nchi wanachama
wa EA wanapokuwa nje na hivyo kurahisisha kupata msaada wa huduma za kikonsula
(Consular Services) mfano kupata msaada wa kurejeshwa nchini kupitia balozi za
nchi wanachama wakati wa dharula ikiwa sehemu husika haina ubalozi wa Tanzania.
Mbali na hilo pia
husaidia wanachama kutambuana wanapokuwa nje ya nchi hivyo kujenga umoja na
ushirikiano sanjari na kurahisisha utambuzi na utunzaji wa kumbukumbu za raia
wa Afrika Mashariki.
Ikumbukwe kuwa
utekelezaji wa mradi wa utoaji pasipoti mpya za kielektroniki ulifanyika kwa
muda mfupi sana kwa ufadhiri wa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.
Idara ya Uhamiaji
Tanzania kwa kipindi cha Januari 2018 mpaka Disemba 2019 imetoa zaidi ya
pasipoti mpya za kielekroniki 230,000 kwa raia wa Tanzania waliokidhi vigezo
vya kupatiwa pasipoti hizo kwa mujibu wa sheria ya pasipoti ya Tanzania ya
mwaka 2002 sura ya 42 na kanuni zake za mwaka 2004.
“Tulitoa
miaka miwili kwamba itakapofika tarehe 31 Januari 2020 basi tutasitisha
matumizi ya huduma za pasipoti za zamani yaani (MRP) tulianza huduma hii ya utoaji
pasipoti mpya za kielekroniki kwa ofisi za iliyokuwa makao makuu ya Uhamiaji
Tanzania iliyopo Kurasini Jijijini Dar es salaam na Afisi kuu ya Uhamiaji
Zanzibar, lakini mpaka sasa huduma hii tumeisogeza katika mikoa 29 Tanzania
bara hivyo kuleta idadi ya vituo 31vya kutolea huduma hiyo, Katika
balozi zetu pia za nje ya nchi ili kuwasaidia watanzania kubadilisha pasipoti
zao, kupata Pasipoti mpya na kupata huduma za kiuhamiaji kwa urahisi ikiwemo
kutumia njia ya uhamiaji mtandao takribani Balozi 44 zimefungwa mfumo huo”
alisema SSI Alhaj Ally Mtanda Msemaji Mkuu wa Idara ya Uhamiaji Tanzania.
Kwa ujumla kumekuwa
na mwitikio mkubwa kwa wananchi katika kuja kubadilisha pasipoti zao na wengine
kufanya maombi ya pasipoti mpya, ambapo takwimu zinaonesha kwa kipindi cha
tarehe 31 Januari 2018 hadi 31 Disemba 2019 mwaka jana takribani Watanzania
239,946 waliweza kukidhi vigezo vya kupatiwa pasipoti mpya ya kielektroniki kwa
mujibu wa sheria.
Mchanganuo wa
Pasipoti zilizotolewa kwa kipindi hiki ni kama ifuatavyo, pasipoti za kawaida
yaani (Ordinary Passport) 237,813 zimetolewa kwa wananchi, pasipoti za utumishi
(Service Passport) kwa viongozi waandamizi wa serikali idadi 459 na pasipoti za
kidiplomasia (Diplomatic Passport) ambazo wanapewa viongozi wa juu wa nchi
wakiwemo mawaziri, mabalozi na wabunge idadi ni 1672 na pasipoti maalumu za
kidiplomasia 05 hivyo kuleta idadi ya jumla ya pasipoti 239,946.
Idara ya Uhamiaji
inasisitiza na kukumbusha mwisho wa kutumia pasipoti ya zamani yaani (MRP) ni
31 Januari mwaka huu 2020, ewemwananchi epuka usumbufu usiokuwa wa lazima wahi mapema kubadili pasipoti yako.
Aidha gharama zote za upatikanaji wa pasipoti hii mpya ya kusafiria ya kielekroniki ni Tsh.150,000 tu kwa watanzania waishio hapa nchini na kwa waishio nje ya nchi gharama yake ni dola za kimarekani 90 (USD)tu.
HABARI PICHA
Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli akitia saini pasipoti yake mpya ya kielekroniki wakati wa uzinduzi wa utoaji wa pasipoti hizo mpya kwa raia wa Tanzania |
Mke wa Rais wa Tanzania Mama Janeth Mgufuli nae akipata huduma ya pasipoti mpya ya kielektroniki na hapa anachuku alama za vidole kama hatua moja wapo ya kukamilisha tartibu za upatikanaji wa Pasipoti hiyo |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni