Shirika la Umoja wa Mataifa
la Wahamaji (IOM) kwa kushirikiana na Idara ya Uhamiaji wameendesha mafunzo ya
elimu kwa umma mapema mwezi huu kuhusu masuala ya uhamiaji mipakani katika
kijiji cha Jasini kilichopo katika kata ya Mayomboni, Wilaya ya Mkinga Mkoani
Tanga.
IOM Tanzania
inatekeleza miradi mingi hapa Afrika hususani nchini Tanzania na sasa wakishirikiana
na Idara ya Uhamiaji Tanzania wanatekeleza mradi huu wa kampeni ya utoaji elimu
kwa umma kuhusu masuala ya kiuhamiaji mipakani ikiwa na lengo kuu la kutatua
changamoto wanazokutana nazo wananchi waishio mipakani na kuwajengea uwezo ili
kuwa na uhusiano mzuri wa kuwezesha ulinzi na usalama na hatimae kupambana na
uhalifu unaotokea mipakani.
Akifungua rasmi
mafunzo hayo ya kuwajengea uwezo wawakilishi wa wananchi, Mkuu wa Wilaya ya
Mkinga Yona Maki amelishukuru Shirika la Umoja wa Mataifa la Wahamaji (IOM)
na Idara ya Uhamiaji Tanzania kwa kuwaletea fursa hiyo ya mafunzo kwa wananchi
wake ili kusaidia kupunguza vitendo vya kihalifu vinavyotokea katika mpaka wa
Kenya na Tanzania.
Vitendo hivyo vya
kihalifu vinasababishwa na kutokuwa na elimu sahihi ya jinsi ya kuishi mipakani
na namna ya kuwabaini wahamiaji haramu ambao wanaweza kuhatarisha usalama wa
Taifa na wananchi kwa ujumla.
“Tunapoishi mipakani
kuna shughuli nyingi zinafanyika, wengine mnasafirisha magendo, wengine
mnasafirisha wahamiaji haramu ili kujipatia fedha, lakini leo wamekuja
wataalamu wetu na wanatufundisha madhara ya kufanya shughuli haramu kama hizo
ni kosa la jinai hivyo yazingatieni sana mafunzo haya kwa faida ya kizazi cha
sasa na baadae” alisema Bwana Maki.
Aidha ameendelea
kuishukuru serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa
kuiwezesha Idara ya Uhamiaji kuendelea kutekeleza majukumu yake ipasavyo ikiwa
ni pamoja na utoaji elimu kwa umma na wanavyoshirikiana kwa karibu na shirika
hili la IOM jambo ambalo limesaidia sana kupungua kwa vitendo vya kihalifu
katika mipaka ya nchi yetu hasa katika Mkoa wa Tanga.
“IOM na Idara ya
Uhamiaji Wamekuwa ni wadau wetu wakubwa sana kwani wameendelea kutuletea
mafunzo kama haya kwa zaidi ya mara tatu sasa wanafika katika maeneo yetu ya
Wilaya ya Mkinga na kutupa elimu hii muhimu sana” alisema.
Kwa upande wake Afisa
Uhusiano kutoka Idara ya Uhamiaji Makao Makuu Mrakibu Msaidizi, Azizi
Kirondomara akitambulisha mada zilizofundishwa alisema washiriki wamefundishwa
aina za uhalifu unaovuka mipaka, usafirishaji haramu wa binadamu, usafirishaji
kimagendo, ugaidi usafirishaji silaha haramu, uingizaji bidhaa feki, utakatishaji
fedha, madawa ya kulevya, uhalifu wa kimtandao, na taratibu za kuingia nchini.
Aidha amebainisha
madhara yanayoweza kutokea endapo wahamiaji haramu watapenya na kuingia hapa
nchini, ambapo hupelekea kuhatarisha usalama wa Taifa, kuongeza mzigo serikali
katika utoaji wa huduma za jamii, kuongezeka kwa vitendo vya kihalifu, kupungua
kwa nafasi za ajira, kuchochea migogoro baina ya wafugaji na wakullima na pia
wahamiaji holela kushiriki katika chaguzi mbalimbali za serikali.
Afisa uhamiaji
mfawidhi wa kituo cha uhamiaji Horohoro, Mrakibu Singwa Mokiwa alibainisha
kwamba wasafirishaji wakubwa wa wahamiaji haramu katika wilaya ya Mkinga ni
madereva Bodaboda ambao hutumia vipenyo ikiwemo eneo la kijiji cha Jasini hivyo
elimu hiyo imefika wakati muafaka ambapo itawasaidia madereva hao kutimiza
wajibu wao bila kuvunja sheria na kuilinda nchi yao dhidi ya wahamiaji haramu.
Mrakibu Mokiwa ametoa
wito kwa wananchi kwamba mlinzi namba moja wa mipaka ni mwananchi mwenyewe
hivyo wananchi wanatakiwa kuwa na uzalendo na nchi yao kwa kuwafichua wahamiaji
haramu ikiwemo kutoa taarifa kwa mamlaka husika.
Washiriki wa Mafunzo
hayo waliotoka katika makundi mbalimbali ya kijamii walikuwa na matarajio ya
kujua sheria za kuishi mipakani, kujua muhusika wa kwanza wa uhamiaji haramu,
jinsi ya kumtambua mhamiaji haramu na madhara ya kupitisha wahamiaji haramu
katika mipaka ya nchi yetu.
Yote hayo yalipatiwa ufumbuzi na wakufunzi Mrakibu Msaidizi wa Uhamiaji Azizi Kirondomara kutoka Kitengo cha Uhusiano Uhamiaji Makao Makuu, Bi Lucy Mseke Afisa Mradi Msaidizi IOM Tanzania na Bwana David Lukiri Kutoka Shirika la umoja wa mataifa la Wahamaji IOM.
HABARI PICHA NA MATUKIO
Yona Maki Mkuu wa Wilaya Mkinga |
Washiriki wa mafunzo ya Uhamiaji wakifuatilia kwa makini mafunzo yanayoendeshwa na IOM na Idara ya Uhamiaji katika kijiji cha Jasini Wilayani Mkinga Mkoani Tanga |
Afisa Uhamiaji Mfawidhi wa Kituo cha Uhamiaji Horohoro Mrakibu Singwa Mokiwa akiongea na washiriki wa mafunzo ya uhamiaji (Hawapo Pichani) katika kijiji cha Jasini kilichopo Wilayani Mkinga Mkoani Tanga mpakani mwa Tanzania na Kenya |
Baadhi ya washiriki waliohudhuria Mafunzo wakiwa katika Picha ya pamoja na Viongozi wa IOM na Idara ya Uhamiaji |
Mrakibu Msaidizi wa Uhamiaji Azizi Kirondomara kutoka Kitengo cha Uhusiano Uhamiaji Makao Makuu akiwasilisha moja ya mada ya madhara ya uhamiaji haramu nchini |
Lucy Mseke Afisa Mradi Msaidizi IOM Tanzania akieleza lengo la mafunzo |
David Lukiri Mmoja wa wakufunzi kutoka IOM akiwafundisha washiriki mbinu za kupambana na uhamiaji haramu katika maeneo ya mipakani |
Lucy Mseke kutoka IOM akifundisha moja ya mada za uhamiaji mpakani |
Washiriki wakifuatilia kwa makini mada zinzofundishwa |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni