Idara ya Uhamiaji
Tanzania kwa kipindi cha Januari 2018 mpaka Disemba 2019 imetoa zaidi ya
pasipoti mpya za kielekroniki 230,000 kwa raia wa Tanzania.
Hayo yamesemwa mapema
leo hii na Msemaji Mkuu wa Idara ya Uhamiaji Tanzania Mrakibu Mwandamizi wa
Uhamiaji, Alhaj Ally Mtanda wakati akiongea na waandishi wa habari katika Ofisi
za Uhamiaji Kurasini, Jijini - Dar es salaam.
“Tulitoa
miaka miwili kwamba itakapofika tarehe 31 Januari 2020 tutasitisha matumizi ya
huduma za pasipoti za zamani yaani (MRP) tulianza huduma hii ya utoaji pasipoti
mpya za kielekroniki kwa ofisi za makao
makuu ya Uhamiaji Tanzania bara na Afisi Kuu ya Uhamiaji Zanzibar, lakini mpaka
sasa huduma hii tumeisogeza katika Mikoa yote hapa nchini na katika Balozi zetu
zote za nje ya nchi ili kuwasaidia Watanzania kubadilisha pasipoti zao, kupata
Pasipoti mpya na huduma nyingine za kiuhamiaji
kwa urahisi kwa kutumia njia ya mtandao” alisema Mtanda.
Kwa ujumla kumekuwa
na mwitikio mkubwa kwa Wananchi kujitokeza kubadilisha pasipoti zao pamoja na waombaji
wapya wa pasipoti za kielektroniki, ambapo takwimu zinaonesha kwa kipindi cha tarehe
31 Januari 2018 hadi 31 Disemba 2019 takribani Watanzania 239,946 waliweza
kukidhi vigezo vya kupatiwa pasipoti, kwa mujibu wa sheria ya Pasipoti na hati
za safari Sura ya 42 ya Mwaka 2002 na Kanuni zake za Mwaka 2004.
Mchanganuo wa
Pasipoti zilizotolewa kwa kipindi hiki ni kama ifuatavyo, pasipoti za kawaida
yaani (Ordinary Passport) 237,813 zimetolewa kwa wananchi, pasipoti za utumishi
(Service Passport) kwa viongozi waandamizi wa serikali idadi 459 na pasipoti za
kidiplomasia (Diplomatic Passport) ambazo wanapewa viongozi wanye hadhi ya
kidiplomasia wakiwemo mawaziri, mabalozi
na wabunge idadi ni 1672 na
pasipoti maalumu za kidiplomasia zilizotolewa kwa viongozi wa juu wa Serikali 05
hivyo kuleta idadi ya jumla ya pasipoti 239,946.
Ikumbukwe kuwa zoezi
la ubadilishaji wa pasipoti za zamani (MRP) kuelekea pasipoti mpya za
kielektroniki lilizinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 31 Januari mwaka 2018, katika Ofisi za
iliyokuwa Makao Makuu ya Uhamiaji, kurasini, Jijini Dar es Salaam, ili kuendelea
kukidhi utoaji wa huduma za kiuhamiaji kwa viwango vya kimataifa.
Aidha gharama zote za
upatikanaji wa pasipoti hii mpya ya kusafiria ya kielekroniki ni Tsh. 150,000
tu kwa watanzania waishio hapa nchini na kwa waishio nje ya nchi gharama yake
ni dola za kimarekani 90 (USD) tu.
HABARI NA MATUKIO
Msemaji Mkuu wa Idara ya Uhamiaji Tanzania Mrakibu Mwandamizi Alhaj Ally Mtanda |
Mteja akipatiwa pasipoti yake katika ofisi za Uhamiaji Kurasini Dar es salaam mara baada ya kumaliza hatua zote za uombaji |
Mmoja wa wateja waliofika katika ofisi za uhamiaji kurasini jijini Dar es salaam akifurahia pasipoti mpya ya kielekroniki kulia kwake ni Msemaji wa Idara ya Uhamiaji Tanzania Mrakibu Mwandamizi wa Uhamiaji SSI Alhaj Ally Mtanda |
Mteja akionesha pasipoti yake mpya ya kielekroniki mara baada ya kumaliza hatua zote na kuipata |
Uchukuaji wa Alama za vidole ikiwa ni hatua muhimu za kupata pasipoti mpya ya kielekroniki |
Picha zote na Kitengo cha Uhusiano Uhamiaji Makao Makuu |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni