Visitors

IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA UHAMIAJI HABARI BLOGU KARIBU KWENYE BLOG RASMI YA IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA TUNAKULETEA MATUKIO YANAYOTOKEA KILA SIKU KATIKA IDARA YA UHAMIAJI TAFADHALI TUNAOMBA TUFUATILIE PIA KATIKA MITANDAO YETU YA KIJAMII

28 Septemba 2019

NAIBU KATIBU MKUU RAMADHAN KAILIMA ATEMBELEA OFISI YA UHAMIAJI MAKAO MAKUU

Naibu Katibu Mkuu Ramadhani Kailima na Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala wakifurahia jambo na wananchi ambao wapo kwenye foleni ya kusubiria huduma ya kupewa pasipoti kwa dharura.

Mkuu wa Kitengo cha Tehama Kamishna Msaidizi Mwandamizi Mohamed Awesu akimwonyesha Naibu Katibu Mkuu namna mfumo wa Tehama wa e-Immigration unavyofanya kazi nchi nzima


Naibu Katibu Mkuu Ramadhani Kailima akiangalia pasipoti ya kieletroniki baada ya kuchapishwa alipotembelea chumba cha Passport Printing, Uhaimiaji Makao Makuu.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ramadhani Kailima akingalia jinsi pasipoti inavyokaguliwa katika mfumo kwenye hatua ya mwisho kabla ya kutolewa ili itumike

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Ramadhani Kailima
ametembelea Ofisi ya Uhamiaji Makao Makuu Dar es Salaam na kujionea namna  Idara hiyo ilivyojipanga kuwahudumia Wananchi.


 Akiwa Ofisini hapo, Naibu Katibu Mkuu huyo alipata fursa ya kukagua Mfumo wa utoaji wa huduma ya Pasipoti.


 Maeneo aliyotembelea na kukagua ni Kaunta ya kupokelea maombi, Chumba maalum cha kuchukulia alama za vidole kielektroniki, Ofisi ya Uhakiki na Udhinishaji wa maombi hayo pamoja na Ofisi ya Uchapishaji wa Pasipoti (Passports' Printing Room).
 Naibu Katibu Mkuu huyo pia amekagua Kitengo cha Utoaji wa Pasipoti kwa haraka/dharura kwa Wananchi wenye mahitaji maalum.


 Kabla ya kuhitimisha Ziara yake, Naibu Katibu Mkuu Kailima alipata fursa ya kuzungumza na Wananchi na raia wa kigeni walifika Ofisini hapo kwa ajili ya kupatiwa huduma mbalimbali za kiuhamiaji.


 Aidha, Naibu Katibu Mkuu Kailima amemuagiza Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Peter Makakala kuanzisha utoaji wa huduma za Pasipoti kwa haraka (express).
 "Nimelezwa kuwa kwa sasa Waombaji wa Pasipoti wanapatiwa kwa muda siku  ..., Hivyo  anzisheni Mfumo wa utoaji wa Pasipoti kwa haraka (express) na Wananchi watakao hitaji huduma hiyo wachangie kiasi kidogo cha fedha na kupatiwa Pasipoti zao kwa muda wa siku moja", alizungumza Kailima.


 Aliongeza kuwa wapo baadhi ya Wananchi hawapendi kutumia muda wao mwingi kwenye foleni wakati wanaweza kulipia kiasi kidogo cha fedha ili kupata huduma kwa haraka.
  Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Peter Makakala
alimwahidi Naibu Katibu Mkuu huyo kutekeleza maelekezo aliyoyatoa katika ziara hiyo.
 Dkt. Makakala ameongeza kuwa Idara ya Uhamiaji imejiimarisha vyema kutekeleza Mradi wa Uhamiaji Mtandao kwa lengo la kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi na wageni.
 Kupitia Mfumo huo, Jumla ya Pasipoti 187,787 na hati za dharura za safari (Emergency Traveling Documents - ETDs) 255,534 zimetolewa kwa Watanzania.


 Dkt. Makakala ameongeza kuwa Idara ya Uhamiaji inatekeleza vyema dhana kuimarisha sekta za Utalii na Uwekezaji Nchini. Kupitia Mfumo huu, Idara imetoa Vibali vya Ukaazi 6,848 kwa Wageni waliongia na kuishi Nchini kwa madhumuni mbalimbali ikiwemo Uwekezaji.
  Pia Idara ya Uhamiaji imetoa viza 152,377 kwa Wageni walioingia nchini kwa madhumuni mbalimbali ikiwemo Utalii na Matembezi.


 Mfumo wa Uhamiaji Mtandao unaohusisha Utoaji wa huduma za kielektroniki za Pasipoti, Viza, Vibali vya Ukaazi pamoja na Usimamizi na Udhibiti wa Mipaka umezinduliwa mnao Januari 31, 2018 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.


19 Septemba 2019

WAHITIMU UHAMIAJI WATAKIWA KUFANYA KAZI KWA WELEDI NA KUZINGATIA SHERIA


Wahitimu wa mafunzo ya Uongozi ya Maafisa Uhamiaji wametakiwa kutumia elimu waliyoipata  kufanya kazi kwa bidii, weledi na kwa kuzingatia sheria ili kuboresha huduma za kiuhamiaji  kwa wageni na wananchi kwa ujumla.

Hayo yamezungumzwa na Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Peter Makakala wakati akifunga Mafunzo ya Maafisa Uhamiaji Daraja la Pili yaliyofanyika katika Chuo cha Magereza cha Gereza Kuu Kingolwira - Morogoro mwanzoni mwa wiki hii. 
Dkt. Makakala amewataka wahitimu hao kuzingatia dhana ya uwajibikaji hivyo kutumia elimu waliyoipata kupitia mafunzo hayo kufanya kazi kwa uadilifu na bidii ili kuboresha huduma kwa wageni na raia wa Tanzania.

“Mafunzo mliyopata yawe chachu na kuongeza hamasa katika kutoa huduma iliyotukuka kwa wageni na kuifanya Tanzania kuwa sehemu salama ya uwekezaji bila kuweka vikwazo zinavyo kwamisha uwekezaji nchini”, alisisitiza Dkt. Makakala. 

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Magereza cha Gereza Kuu Kingolwira - Morogoro, Kamishna Msaidizi wa Magereza, Lazaro Nyanga (ACP) amewapongeza wahitimu hao kwa kuonesha nidhamu kwa kipindi chote cha mafunzo na amewata kuendeleza uadilifu huo watakapokuwa kwenye vituo vyao vya kazi.

“Wamekuwa wakijitolea na kufanya kazi kwa bidii na kushiriki katika shughuli za kijamii na wakati mwingine kujitolea kutatua changamoto mbalimbali zinazokikabili chuo chetu ikiwa ni pamoja na kutumia nguvu kazi kwa ajili ya ujenzi wa miundo mbinu ya chuo chetu. Hivyo naomba nichukue fursa hii kuwashukuru, kuwapongeza na kuwataka waendelee kuwa na moyo huo kwa wakati wote watakapokuwa kazini ili kuchangia jitihada za Serikali kwa mambo mbalimbali katika sehemu zao za kazi”, aliongeza Kamishna Msaidizi wa Magereza Nyanga.

Akizungumza na Uhamiaji Media Mmoja wa Wahitimu hao Mkaguzi Msaidizi wa Uhamiaji, Vedasto Rwekiza Venant amesema kuwa mafunzo hayo yamekuwa chachu kwao na kuahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote waliyopewa na Viongozi wakati wa kufunga mafunzo hayo.

Ikumbukwe kwamba Mafunzo haya yanafanyika kutokana na Marekebisho ya Sheria ya Uhamiaji Na. 8 ya Mwaka 2015 (The Immigration Ammendment Act, 2015).

Kupitia marekebisho hayo yameiingiza Idara ya Uhamiaji katika Tume ya Polisi, Uhamiaji na Magereza hatua ambayo kimsingi yamechangia uwepo wa mabadiliko katika kuajiri, upandishwaji wa vyeo, utoaji wa stahili na mafunzo mbalimbali.

Tayari Idara ya Uhamiaji imetoa mafunzo kwa Maafisa na Askari 642 hadi sasa, kwa kozi maalum za kijeshi za kupandishwa vyeo (Promotion Course) katika Shule ya Polisi Moshi na Chuo cha Magereza cha Gereza Kuu Kingolwira - Morogoro. Awamu ya kwanza kwa kipindi cha Mwezi Aprili na Juni 2017, jumla ya Maafisa na Askari 222 wamehitimu. Awamu ya Pili imehusisha Maafisa na Askari 362 kwa mafunzo yaliyofanyika kati ya Mwezi Februari na Julai, 2018. 

Sherehe hizo za ufungaji wa mafunzo hayo zimehudhuliwa na Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar, Johari Masoud Sururu (CI-Znz), Kamishna wa Uhamiaji, Utawala na Fedha Edward Peter Chogero (CI-A&F), Kamishna wa TRITA, Maurice Kitinusa (CI-TRITA), Kamaishna wa Magereza, Huduma za Urekebishaji, Tusikile Mwaisabela (CP), Viongozi wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa Morogoro, Wananchi wa Morogoro, Waaalikwa pamoja na na Waandishi wa habari.16 Septemba 2019

DKT MAKAKALA KUFUNGA MAFUNZO YA UONGOZI YA MAAFISA UHAMIAJIKamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Peter Makakala kesho Jumanne tarehe 17 Septemba, 2019 anatarajia kufunga Mafunzo ya Uongozi ya awamu ya nne kwa Maafisa 54 wa ngazi ya Wakaguzi Wasaidizi wa Uhamiaji ambao wamehitimu mafunzo hayo.


Akitoa taarifa hiyo Mjini Morogoro, Msemaji Mkuu wa Idara ya Uhamiaji, Mrakibu Mwandamizi Alhaji Ally Mtanda amesema kuwa Mafunzo hayo yatafungwa na Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Peter Makakala katika Chuo cha Magereza cha Gereza Kuu Kingolwira – Morogoro.


Sherehe hizo za ufungaji wa mafunzo hayo zitahudhuriwa na Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar, Johari Masoud Sururu  (CI-Znz), Kamishna wa Uhamiaji,  Utawala na Fedha Edward Peter Chogero (CI - A&F), Kamishna wa TRITA, Maurice Kitinusa  (CI - TRITA), Afisa Uhamiaji Mkoa Morogoro, Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji Angela Mathew Shija (ACI) pamoja na Wakuu wa  Vitengo mbalimbali kutoka Ofisi ya Uhamiaji Makao Makuu.