Visitors

IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA UHAMIAJI HABARI BLOGU KARIBU KWENYE BLOG RASMI YA IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA TUNAKULETEA MATUKIO YANAYOTOKEA KILA SIKU KATIKA IDARA YA UHAMIAJI TAFADHALI TUNAOMBA TUFUATILIE PIA KATIKA MITANDAO YETU YA KIJAMII

19 Septemba 2019

WAHITIMU UHAMIAJI WATAKIWA KUFANYA KAZI KWA WELEDI NA KUZINGATIA SHERIA


Wahitimu wa mafunzo ya Uongozi ya Maafisa Uhamiaji wametakiwa kutumia elimu waliyoipata  kufanya kazi kwa bidii, weledi na kwa kuzingatia sheria ili kuboresha huduma za kiuhamiaji  kwa wageni na wananchi kwa ujumla.

Hayo yamezungumzwa na Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Peter Makakala wakati akifunga Mafunzo ya Maafisa Uhamiaji Daraja la Pili yaliyofanyika katika Chuo cha Magereza cha Gereza Kuu Kingolwira - Morogoro mwanzoni mwa wiki hii. 
Dkt. Makakala amewataka wahitimu hao kuzingatia dhana ya uwajibikaji hivyo kutumia elimu waliyoipata kupitia mafunzo hayo kufanya kazi kwa uadilifu na bidii ili kuboresha huduma kwa wageni na raia wa Tanzania.

“Mafunzo mliyopata yawe chachu na kuongeza hamasa katika kutoa huduma iliyotukuka kwa wageni na kuifanya Tanzania kuwa sehemu salama ya uwekezaji bila kuweka vikwazo zinavyo kwamisha uwekezaji nchini”, alisisitiza Dkt. Makakala. 

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Magereza cha Gereza Kuu Kingolwira - Morogoro, Kamishna Msaidizi wa Magereza, Lazaro Nyanga (ACP) amewapongeza wahitimu hao kwa kuonesha nidhamu kwa kipindi chote cha mafunzo na amewata kuendeleza uadilifu huo watakapokuwa kwenye vituo vyao vya kazi.

“Wamekuwa wakijitolea na kufanya kazi kwa bidii na kushiriki katika shughuli za kijamii na wakati mwingine kujitolea kutatua changamoto mbalimbali zinazokikabili chuo chetu ikiwa ni pamoja na kutumia nguvu kazi kwa ajili ya ujenzi wa miundo mbinu ya chuo chetu. Hivyo naomba nichukue fursa hii kuwashukuru, kuwapongeza na kuwataka waendelee kuwa na moyo huo kwa wakati wote watakapokuwa kazini ili kuchangia jitihada za Serikali kwa mambo mbalimbali katika sehemu zao za kazi”, aliongeza Kamishna Msaidizi wa Magereza Nyanga.

Akizungumza na Uhamiaji Media Mmoja wa Wahitimu hao Mkaguzi Msaidizi wa Uhamiaji, Vedasto Rwekiza Venant amesema kuwa mafunzo hayo yamekuwa chachu kwao na kuahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote waliyopewa na Viongozi wakati wa kufunga mafunzo hayo.

Ikumbukwe kwamba Mafunzo haya yanafanyika kutokana na Marekebisho ya Sheria ya Uhamiaji Na. 8 ya Mwaka 2015 (The Immigration Ammendment Act, 2015).

Kupitia marekebisho hayo yameiingiza Idara ya Uhamiaji katika Tume ya Polisi, Uhamiaji na Magereza hatua ambayo kimsingi yamechangia uwepo wa mabadiliko katika kuajiri, upandishwaji wa vyeo, utoaji wa stahili na mafunzo mbalimbali.

Tayari Idara ya Uhamiaji imetoa mafunzo kwa Maafisa na Askari 642 hadi sasa, kwa kozi maalum za kijeshi za kupandishwa vyeo (Promotion Course) katika Shule ya Polisi Moshi na Chuo cha Magereza cha Gereza Kuu Kingolwira - Morogoro. Awamu ya kwanza kwa kipindi cha Mwezi Aprili na Juni 2017, jumla ya Maafisa na Askari 222 wamehitimu. Awamu ya Pili imehusisha Maafisa na Askari 362 kwa mafunzo yaliyofanyika kati ya Mwezi Februari na Julai, 2018. 

Sherehe hizo za ufungaji wa mafunzo hayo zimehudhuliwa na Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar, Johari Masoud Sururu (CI-Znz), Kamishna wa Uhamiaji, Utawala na Fedha Edward Peter Chogero (CI-A&F), Kamishna wa TRITA, Maurice Kitinusa (CI-TRITA), Kamaishna wa Magereza, Huduma za Urekebishaji, Tusikile Mwaisabela (CP), Viongozi wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa Morogoro, Wananchi wa Morogoro, Waaalikwa pamoja na na Waandishi wa habari.Hakuna maoni:

Chapisha Maoni