Idara ya Uhamiaji nchini imepokea ugeni kutoka chuo cha Ulinzi wa Taifa NDC kwa ajili ya ziara ya kupatiwa mafunzo ya namna Idara ya Uhamiaji inavyofanya shughuli zake katika ulinzi wa Taifa na maendeleo ya kiuchumi.
Ziara hiyo ya mafunzo imefanyika katika Ofisi ya Uhamiaji makao makuu Dodoma huku ikiongozwa na Mkuu wa chuo hicho Meja Jenerali Ibrahim Michael Mhona na kupokelewa na Kaimu Kamishna Jenerali wa uhamiaji nchini, anayeongoza Divisheni ya Uraia na Pasipoti Kamishna Gerald Kihinga ambae alimwakilisha Kamishna Jenerali wa Uhamiaji nchini (CGI) Dkt. Anna Peter Makakala.
Zaidi ya washiriki 60 walipatiwa mafunzo hayo huku wengi wakitoea katika vyombo vya ulinzi na usalama nchini, viongozi waandamizi kutoka katika taasisi za serikali na wengine kutoka nchi washiriki hususani kutoka katika nchi ya Bangladesh, Burundi, Uganda, Kenya, Malawi, Zambia na Nigeria.
Katika mafunzo hayo, mada mbalimbali ziliweza kuwasilishwa na maafisa kutoka Idara ya uhamiaji Mrakibu Mathew Ikomba kutoka kitengo cha utawala na uratibu, Mrakibu Msaidizi Azizi Kirondomara kutoka kitengo cha uhusiano uhamiaji makao makuu pamoja na Kamishna wa Uhamiaji Utawala na Fedha (CI) Edward Chogero na Kamishna wa Uhamiaji Divisheni ya Visa Vibali vya ukaazi na Pasi (CI) Marry Palmer ndc.
Maofisa hao walifundisha masuala ya Pasipoti, Visa za Kielektroniki, Uraia pamoja na mifumo inayotumika katika utoaji wa pasipoti na visa za kieletroniki sanjari na masuala ya ulinzi wa mipaka na udhibiti wa wahamiaji haramu.
Aidha, washiriki wa ziara hiyo walipata fursa ya kuuliza maswali na kujibiwa ipasavyo sanjari na kutembelea na kujionea maendeleo ya ujenzi wa jengo jipya la ofisi za makao makuu ya Idara ya Uhamiaji lililopo Jijini Dodoma.
Kwa upande wao washiriki walimpongeza Kamishna Jenerali wa Uhamiaji nchini Dkt. Anna Makakala kwa mafunzo waliyoyapata na kuongeza kuwa, mafunzo hayo yatawajengea uwezo wa kufanya kazi kwa ufanisi na weledi mkubwa hususani katika kuwahudumia Watanzania, Afrika na Dunia kwa Ujumla.
Idara ya Uhamiaji inafanya kazi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu katika utendaji wake na inasimamiwa na sheria ya Uhamiaji sura ya 54 Rejeo la mwaka 2016, sheria ya Uraia Tanzania sura ya 357 Rejeo la 2002, sheria ya Tanzania ya Pasipoti na hati za kusafiria sura ya 42 ya mwaka 2002 pamoja na kanuni zake.
Majukumu ya msingi ya Idara ya Uhamiaji ni kusimamia na kudhibiti uingiaji na utokaji wa watu nchini, kutoa hati na vibali vya ukaazi kwa raia wa kigeni waliokidhi matakwa ya sheria ya kuishi hapa nchini kwa madhumuni mbalimbali, kutoa huduma za pasipoti na hati nyingine za safari kwa raia wa Tanzania, kuratibu maombi ya wageni wanaoomba uraia wa Tanzania, Kufanya misako na doria kubaini wageni wanaoishi nchini kinyume cha sheria pamoja na kuendesha kesi za makosa ya ki-uhamiaji.
HABARI PICHA NA MATUKIO
Mkuu wa chuo cha Ulinzi wa Taifa NDC Meja Jenerali Ibrahim Michael Mhona akisaini kitabu cha wageni katika ofisi ya Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Makao Makuu Jijini Dodoma |
Kaimu Kamishna Jenerali wa Uhamiaji CI Gerald Kihinga akiongea na washiriki kutoka chuo cha ulinzi wa Taifa NDC |
Kamishna wa Utawala na Fedha Edward Chogero akifafanua jambo kwa washiriki kutoka chuo cha ulinzi wa Taifa NDC |
Baadhi ya washiriki kutoka nchi mbalimbali wakipata elimu ya Uhamiaji katika ofisi za Uhamiaji Makao Makuu |
(Picha zote na Kitengo cha Uhusiano Uhamiaji Makao Makuu) |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni