Visitors

IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA UHAMIAJI HABARI BLOGU KARIBU KWENYE BLOG RASMI YA IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA TUNAKULETEA MATUKIO YANAYOTOKEA KILA SIKU KATIKA IDARA YA UHAMIAJI TAFADHALI TUNAOMBA TUFUATILIE PIA KATIKA MITANDAO YETU YA KIJAMII

31 Januari 2020

TAARIFA KWA UMMA: MWISHO WA MATUMIZI YA PASIPOTI YA ZAMANI (MRP)


Oparesheni Maalumu ya Uhamiaji Mkoa wa Mara yazaa Matunda

Mara, Tanzania
Afisa Uhamiaji Mkoa wa Mara Naibu Kamishna Albert Rwelamila
Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Mara inaendesha Oparesheni Maalum ya kudhibiti Wahamiaji haramu kwa kukagua viwanda, mashule, taasisi za dini, migodi, hoteli na nyumba za kulala wageni na kufanikiwa kukamata Jumla ya wageni 109, ambao wamekutwa na makosa mbalimbali ya kiuhamiaji kama vile kufanya kazi bila vibali, kuingia nchini kinyume cha taratibu na wengine kuzidisha muda wa ruhusa zao walizopewa kwenye vituo vya kuingia nchini (entry point).

Akizungumza  na Waandishi wa Habari Ofisini kwake Afisa Uhamiaji Mkoa wa Mara Naibu Kamishna (DCI) Albert Rwelamila alisema lengo la Operesheni hiyo ni utekelezaji wa  mkakati wa Idara ya Uhamiaji wa kudhibiti Uhamiaji usio zingatia sheria ambao ulizinduliwa mwezi septemba mwaka 2019.

Hadi kufikia  leo Uhamiaji Mkoa wa Mara imekamata wahamiaji hao haramu wakiwemo wenye utata wa uraia, ambao wanaotoka katika nchi mbalimbali  za Uganda, Kenya, Rwanda, Armenia, Urusi, Korea, Australia, Afrika Kusini, Nigeria, Uingereza Ethiopia, China, Congo, Senegal, India, na Indonesia.

Aidha Naibu Kamishna Rwelamila aliongeza kuwa wamekamata pia raia wengine wa kigeni ambao wamejiandikisha katika daftari la wapiga kura na wengine vitambulisho vya taifa, ambapo idara imefanikiwa kuzuia kwa muda nyaraka hizo kwa uchunguzi zaidi zikiwa idadi nyaraka 24.

Jumla ya Kesi saba zimefikishwa katika mahakama ya wilaya ya Musoma, kwa makosa ya kuingia na kuishi nchini  kinyume cha sheria  ya Uhamiaj ya  Sura ya 54 Rejeo la Mwaka 2016 na Kanuni zake,  ambapo  watuhumiwa watano walikutwa na hatia  na kuhukumiwa kwenda jela miaka mitatu au  kulipa faini ya Tsh 500,000/=, watatu wamelipa faini na kuondoshwa nchini, watuhumiwa wawili wanatumikia kifungo pamoja na watuhumiwa wengine wawili kesi zao bado zinendelea mahakamani.

“Operesheni hii bado inaendelea na tunawataadharisha wageni kufuata uraratibu wa kuingia na kuishi nchini pamoja na kutii sheria bila shuruti” aliongeza Naibu Kamishna Rwelamira

Sanjari na hilo Afisa Uhamiaji Mkoa wa Mara ametoa wito kwa Wageni wanapoingia nchini, wanatakiwa  kuwa na Pasipoti halisi ya kusafiria kutoka katika  nchi yake au hati yoyote ya kusafiria, apate ruhusa, kulingana na dhumuni la safari yake na pia  apite katika kituo rasmi cha  kuingilia nchini.

Ikiwa mgeni anataka kuja kufanya kazi hapa nchini anatakiwa kuomba kibali cha kazi kutoka katika Wizara ya Kazi Ajira na walemavu na baadae kuomba kibali cha ukaazi ambacho kinatolewa na Idara ya Uhamiaji.

Operesheni hiyo, maalumu ilipewa baraka na Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Peter Makakala, katika Mkoa wa Mara ikiwa na lengo la kuthibiti wahamiaji haramu ambao wanaweza kuhatarisha Usalama wa Taifa letu na inaendelea kufanyika kwa ufanisi mkubwa baada ya kuongezewa nguvu ya Askari wapya walioajiriwa hivi karibuni na kusambazwa katika Wilaya zote za Mkoa wa Mara  ambazo ni Bunda, Musoma, Tarime, Serengeti, Rorya na Butiama.

HABARI PICHA NA MATUKIO

Afisa Uhamiaji Mkoa wa Mara Naibu Kamishna Albert Rwelamila (kulia) akionesha baadhi ya Vitambulisho vya Taifa na Kadi za mpiga kura zilizokuwa zinatumika na watu wasiokuwa raia wa Tanzania kushoto kwake ni Naibu kamishna wa Uhamiaji Pima Salehe ambae ndiye Naibu Afisa Uhamiaji Mkoa wa Mara
Afisa Uhamiaji Mkoa wa Mara Naibu Kamishna Albert Rwelamila (kulia) akionesha baadhi ya Vyeti vya kuzaliwa vilivyopatikana kinyume na sheria.

(Picha zote na Ofisi ya Uhusiano Uhamiaji Mkoa wa Mara)

30 Januari 2020

UHAMIAJI Iringa Kinara wa Kukamata Wahamiaji Haramu


Iringa, Tanzania

Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Iringa kwa mara nyingine imekamata wahamiaji haramu (07) raia wa Ethiopia mapema leo hii asubuhi baada ya kutelekezwa na kiongozi wao.

Akiongea na waandishi wa habari Ofisini kwake, Afisa Uhamiaji Mkoa wa Iringa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhamiaji (SACI) Agnes Michael Luziga alisema, watuhumiwa wote wamekamatwa eneo la Igumbilo lililopo karibia na Kituo Kikuu cha mabasi Iringa na Kikosi Maalumu cha doria cha Askari wa Uhamiaji wakati wakitekeleza majukumu yao ya kila siku.

Baada ya kuhojiwa imebainika kuwa watuhumiwa hao walikuwa wametelekezwa na wenyeji wao na walikuwa wanapita katika njia za panya maeneo ya nje kidogo ya Manispaa ya Iringa na walikuwa wanaelekea nchini Afrika ya Kusini kupitia Malawi, aliongeza Kamishna Msaidizi Mwandamizi Luziga.

Watuhumiwa wote wanatarajiwa kufikishwa Mahakamani kwa kosa la kuingia nchini kinyume cha Sheria ya Uhamiaji Sura 54, Rejeo la Mwaka 2016 pamoja na Kanuni zake.

Aidha, Idara ya Uhamiaji inatoa wito kwa watu wasiowadilifu na wanaojihushisha na biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu kuacha mara moja.

Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Iringa inaendelea kufanya doria na oparesheni mbalimbali kwa lengo la kuwabaini na kuwakamata watuhumiwa wote wanaoishi nchini kinyume cha Sheria na kuwafikisha Mahakamani na hatimaye kuwaondosha nchini.

Ikumbukwe kuwa ndani ya mwezi mmoja tu wa Januari 2020 Uhamiaji Mkoa wa Iringa imefanikiwa kukamata wahamiaji haramu zaidi ya mara tatu mfululizo.
HABARI PICHA NA MATUKIO
Afisa Uhamiaji Mkoa wa Iringa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhamiaji (SACI) Agnes Michael Luziga
Afisa Uhamiaji Mkoa wa Iringa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhamiaji (SACI) Agnes Michael Luziga (Kulia) akiwa na Afisa Uhamiaji Msaidizi Mkoa Kamishna Msaidizi (ACI) Peter Joseph Kimario 
Watuhumiwa waliokamatwa








(Picha zote na Ofisi ya Uhusiano Mkoa wa Iringa)

28 Januari 2020

UHAMIAJI Mtwara Yamshukuru CGI Kwa Kuongezewa Askari Wapya 20

Mtwara, Tanzania
Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Mtwara imetoa shukrani zake za dhati kwa Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Peter Makakala kwa kuongezewa nguvu ya askari wapya 20.

Jumla ya askari wapya 20 waliripoti Mkoani Mtwara mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka jana 2019 Mara baada ya kumaliza mafunzo ya Uhamiaji katika Chuo cha Uongozi cha Jeshi la Kujenga Taifa JKT-Kimbiji Kilichopo Wilaya ya Kigamboni Jijijini Dar es salaam.

Akitoa Taarifa ya utendaji kazi ya Mkoa, wakati wa ziara ya Kamishna wa Uhamiaji anayesimamia Chuo cha Uhamiaji cha Kikanda (TRITA) Maurice Kitinusa, Afisa Uhamiaji Mkoa wa Mtwara Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji James Mwanjotile alisema mara baada ya kupata mgao huo aligawa askari hao kwa kila wilaya na vituo vyote vya uhamiaji mkoani hapo kulingana na mahitaji ya sehemu husika.

“Ujio huu wa askari wapya afande umesaidia sana kuongeza ufanisi mkubwa katika utendaji wa shughuli mbalimbali ndani ya Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Mtwara, na kwa muda mfupi tu tunaona matunda yake ambapo vitendo vingi vya uhalifu wa Kiuhamiaji vinadhibitiwa ipasavyo, alisema Mwanjotile.

Sanjari na hilo amevishukuru vyombo vingine vya ulinzi na usalama kwa ushirikiano wanaoutoa katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya kiuhamiaji ndani ya mkoa wa mtwara  bila kuwasahau wananchi wa mkoa huo ambao wamekuwa msaada mkubwa wa kutoa taarifa za wahamiaji haramu na kusaidia kudhibiti vitendo hivyo.

Ikumbukwe kuwa mafanikio yote hayo yanatokana na Juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano chini ya  Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. John Pombe Magufuli ambae ndie aliyetoa kibali cha Kuajiri Jumla ya Askari wapya 400 waliomaliza mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa JKT, Oparesheni Kikwete na Oparesheni Magufuli Kujitolea na baadae kujiunga na Mafunzo ya Idara ya Uhamiaji, tayari askari hao wametawanywa nchi nzima Tanzania bara na Zanzibar tayari kwa kulitumikia Taifa lao kwa utii, uzalendo weledi na uhodari.


  HABARI PICHA NA MATUKIO
Kamishna wa Uhamiaji aneyesimamia Chuo cha Uhamiaji cha Kikanda (TRITA) Maurice Kitinusa akisalimiana na Maofisa askari na Watumishi wa Umma Mkoani Mtwara wakati wa ziara yake hivi karibuni
Kamishna wa Uhamiaji aneyesimamia Chuo cha Uhamiaji cha Kikanda (TRITA) Maurice Kitinusa akisalimiana na Maofisa askari na Watumishi wa Umma Mkoani Mtwara wakati wa ziara yake hivi karibuni



Kamishna wa Uhamiaji aneyesimamia Chuo cha Uhamiaji cha Kikanda (TRITA) Maurice Kitinusa akisaini kitabu cha wageni Mkoani Mtwara wakati wa ziara yake hivi karibuni.
Picha na Ofisi ya Uhusiano Uhamiaji Mtwara
Askari wapya wa Idara ya Uhamiaji Tanzania
Askari wapya wa Idara ya Uhamiaji Tanzania
Picha na Maktaba Kutoka Kitengo cha Uhusiano Makao Makuu yan Uhamiaji

27 Januari 2020

Kamishna Kitinusa Apeleka Ujumbe wa CGI Mtwara na Kumshukuru Rais Magufuli kwa Kuajiri Askari wapya 400.


Mtwara, Tanzania
Kamishna wa Uhamiaji anayesimamia Chuo cha Uhamiaji cha Kikanda (TRITA) Maurice David Kitinusa mapema wikii hii amefanya ziara ya siku mbili katika Mkoa wa Mtwara na wilaya zake huku akibeba ujumbe wa Kamishana Jenarali wa Uhamiaji Dkt. Anna Peter Makakala.

Akiongea na Maafisa, Askari na Watumishi wa Idara ya Uhamiaji Mkoani hapo alisema Kamishna Jenerali wa Uhamiaji anamshukuru Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuridhia kuajiri askari wapya 400 waliohitimu mafunzo yao mwezi Disemba mwaka jana 2019  katika Chuo cha Uongozi chaJeshi la Kujenga Taifa-Kimbiji kilichopo wilaya ya Kigamboni Jijini  Dar es salaam, na tayari  walishapangiwa vituo mbalimbali vya kazi nchi nzima na wanachapa kazi ipasavyo.

Mbali na idadi hiyo kuongezeka bado tuna uhitaji mkubwa wa watumishi ndani ya idara yetu kwani malengo ni kufikia askari elfu ishirini (20,000).

Hivyo kutokana na upungufu huo kamishina Jenerali amewataka watumishi wote waliopo kufanya kazi kwa bidii, weledi, uzalendo utii na uhodari wa hali ya juu wakati changamoto hiyo ikiendelea kutatuliwa kama ilivyooneshwa nia na Rais Magufuli.

Aidha ameendelea kusisitiza Utoaji wa huduma bora na ukusanyaji wa maduhuli ya serikali na kuhakikisha Idara inatimiza malengo yake ya kukusanya maduhuli kwa ajili ya maendeleo na uchumi wa Taifa.
Katika ujumbe huo kamishna Jenerali wa Uhamiaji amewaasa Maafisa, Askari, na Watumishi wote ndani ya Idara ya Uhamiaji kujiepusha na rushwa na kufanya kazi kwa weledi zaidi.

Kutokana na tatizo la wahamiaji haramu ndani ya nchi, Kamishina Jenerali amewataka askari na watumishi wengine wa Idara ya Uhamiaji kuhakikisha wanakabiliana na tatizo hilo kwa kuendesha Oparesheni maalumu, akifafanua ujumbe huo Kamishna Maurice Kitunusa ametoa agizo la kufanyika kwa Oparesheni maalumu ya kuwabaini wahamiaji haramu waliopo ndani ya nchi na kuwachukulia hatua ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani.

Pia amesisitiza kutumia vyombo vya habari nchini yaani T.V, redio, magazeti na mitandao ya kijamii ili kuuhabarisha umma juu ya kinachoendelea katika oparesheni hiyo na Kuendelea kutoa elimu kwa umma juu ya madhara ya kuruhusu wahamiaji haramu katika nchi yetu ambapo ni hatari kwa usalama wa Taifa na Dunia kwa ujumla.

Kamishna Kitunusa aliwasili Mkoani Mtwara akitokea Mkoa wa Lindi na Kupokelewa na Mwenyeji wake Afisa Uhamiaji Mkoa wa Mtwara Kamishna Msaidizi James A. Mwanjotile huku akikagua maendeleo ya ujenzi wa Jengo Jipya la Ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Mtwara na baadae kutembelea daraja la umoja linalotenganisha Wilaya ya Nanyumbu na Nchi ya Msumbiji.


HABARI PICHA NA MATUKIO
Kamishna wa Uhamiaji anayesimamia Chuo cha Uhamiaji cha Kikanda (TRITA) Maurice David Kitinusa akiwasilikatika Ofisi za Uhamiaji Mkoani Mtwara
Kamishna wa Uhamiaji anayesimamia Chuo cha Uhamiaji cha Kikanda (TRITA) Maurice David Kitinusa (katikati) akiwa katika ofisi ya Afisa Uhamiaji Mkoa wa Mtwara tayari kwa kupokea taarifa ya Uhamiaji Mkoa kutoka kwa Mwenyeji wake Afisa Uhamiaji Mkoa wa Mtwara Kamishna Msaidizi James A. Mwanjotile 

Kamishna wa Uhamiaji anayesimamia Chuo cha Uhamiaji cha Kikanda (TRITA) Maurice David Kitinusa akisalimiana na Maofisa na Askari wa Ofisi ya Uhamiji Wilaya ya Masasi

Pichani Ujenzi wa Jengo Jipya la Ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Mtwara ukiendelea.



Kamishna Kitinusa alipotembelea daraja la umoja linalotenganisha Wilaya ya Nanyumbu na Nchi ya Msumbiji.
Daraja la umoja linalotenganisha Nchi ya Tanzania na Msumbiji katika  Wilaya ya  Nanyumbu.



Picha zote na Ofisi ya Uhusiano Uhamiaji Mkoa wa Mtwara
Baadhi ya Askari wa Uhamiaji Wakimsikiliza kwa makini Kamishana Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Peter Makakala (Hayupo Pichani) alipowatembelea na kukagua maendeleo yao siku chache kabla ya sherehe ya kumaliza mafunzo yao ya Uhamiaji katika Chuo cha Uongozi wa Kijeshi JKT- Kimbiji.

22 Januari 2020

Uhamiaji Iringa yakamata tena Wahamiaji Haramu


Iringa, Tanzania
Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Iringa inawashikilia Watuhumiwa  (09) kwa makosa ya kiuhamiaji ambapo (07) ni  raia wa Ethiopia, (01) raia wa Kenya mwenye asili ya Somalia na  (01) raia wa Tanzania ambae ni dereva.

Akizungumza na Waandishi wa habari mapema wiki hii, Afisa Uhamiaji Mkoa wa Iringa - Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhamiaji, Agnes Michael Luziga  alisema, watuhumiwa  hao wamekamatwa  eneo la Mtera getini na Askari wa Uhamiaji waliokuwa kwenye doria ya kawaida.  

Watuhumiwa hawa wamekamatwa kwa kosa la kuingia nchini kinyume cha Sheria ya Uhamiaji Sura ya 54 (Immigration Act Cap 54 RE 2016) pamoja na kanuni zake na watuhumiwa wote wanatarajiwa kufikishwa Mahakamani baada ya upelelezi wa tuhuma zao kukamilika, aliongeza Kamishna Msaidizi Mwandamizi Luziga.

Baada ya kuhojiwa na kukaguliwa ilibainika kuwa watuhumiwa hao walikuwa na  pasipoti za kughushi  za Kenya na Ethiopia zikiwa na  vibali vya kughushi na wameingia nchini kupitia njia za panya wakitokea nchini Kenya wakipita kuelekea  nchini Afrika Kusini.

Watuhumiwa hao walitumia gari binafsi aina ya Noah lenye namba za usajili T656 DNP lililokuwa likiendeshwa na dereva raia wa Tanzania Mosses Apendavyo Mbwambo, Watuhumiwa wengine ni Isse Aliye Abdi, Hussein Hirsi Ali, Hassan Maalim Adan, Jama Abdulmalik Yuune, Hussein Siyad Ali,  Mohhamed Hassan Tikki, Ali Muktar Abdulkadir na Osman Mohamed Ali.

Aidha, Idara ya Uhamiaji inatoa  wito  kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri pamoja na madereva kuaacha mara moja tabia na  tamaa za kujishughulisha na  biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu kwani ni kinyume na sheria za nchi na hatari kwa usalama wa nchi yetu.

HABARI PICHA NA MATUKIO

Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhamiaji Agnes Michael Luziga Afisa Uhamiaji Mkoa wa Iringa  


Watuhumiwa wa Makosa ya Kiuhamiaji waliokamatwa Iringa



Gari aina ya Noah lililotumika kusafirishia wahamiaji Haramu


Wahamiaji haramu wakifikishwa katika kituo cha polisi Iringa
(Picha zote na Ofisi ya Uhusiano - Uhamiaji Iringa)

20 Januari 2020

IOM na Uhamiaji Tanzania zatoa elimu Wananchi waishio Mpakani mwa Tanzan...

IOM na Uhamiaji Tanzania zashirikiana kuendesha Mafunzo Mpakani mwa Tanzania na Kenya.


Shirika la Umoja wa Mataifa la Wahamaji (IOM) kwa kushirikiana na Idara ya Uhamiaji wameendesha mafunzo ya elimu kwa umma mapema mwezi huu kuhusu masuala ya uhamiaji mipakani katika kijiji cha Jasini kilichopo katika kata ya Mayomboni, Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga.

IOM Tanzania inatekeleza miradi mingi hapa Afrika hususani nchini Tanzania na sasa wakishirikiana na Idara ya Uhamiaji Tanzania wanatekeleza mradi huu wa kampeni ya utoaji elimu kwa umma kuhusu masuala ya kiuhamiaji mipakani ikiwa na lengo kuu la kutatua changamoto wanazokutana nazo wananchi waishio mipakani na kuwajengea uwezo ili kuwa na uhusiano mzuri wa kuwezesha ulinzi na usalama na hatimae kupambana na uhalifu unaotokea mipakani.

Akifungua rasmi mafunzo hayo ya kuwajengea uwezo wawakilishi wa wananchi, Mkuu wa Wilaya ya Mkinga Yona Maki amelishukuru Shirika la Umoja wa Mataifa la Wahamaji (IOM) na Idara ya Uhamiaji Tanzania kwa kuwaletea fursa hiyo ya mafunzo kwa wananchi wake ili kusaidia kupunguza vitendo vya kihalifu vinavyotokea katika mpaka wa Kenya na Tanzania.

Vitendo hivyo vya kihalifu vinasababishwa na kutokuwa na elimu sahihi ya jinsi ya kuishi mipakani na namna ya kuwabaini wahamiaji haramu ambao wanaweza kuhatarisha usalama wa Taifa na wananchi kwa ujumla.

“Tunapoishi mipakani kuna shughuli nyingi zinafanyika, wengine mnasafirisha magendo, wengine mnasafirisha wahamiaji haramu ili kujipatia fedha, lakini leo wamekuja wataalamu wetu na wanatufundisha madhara ya kufanya shughuli haramu kama hizo ni kosa la jinai hivyo yazingatieni sana mafunzo haya kwa faida ya kizazi cha sasa na baadae” alisema Bwana Maki.

Aidha ameendelea kuishukuru serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuiwezesha Idara ya Uhamiaji kuendelea kutekeleza majukumu yake ipasavyo ikiwa ni pamoja na utoaji elimu kwa umma na wanavyoshirikiana kwa karibu na shirika hili la IOM jambo ambalo limesaidia sana kupungua kwa vitendo vya kihalifu katika mipaka ya nchi yetu hasa katika Mkoa wa Tanga.

“IOM na Idara ya Uhamiaji Wamekuwa ni wadau wetu wakubwa sana kwani wameendelea kutuletea mafunzo kama haya kwa zaidi ya mara tatu sasa wanafika katika maeneo yetu ya Wilaya ya Mkinga na kutupa elimu hii muhimu sana” alisema.

Kwa upande wake Afisa Uhusiano kutoka Idara ya Uhamiaji Makao Makuu Mrakibu Msaidizi, Azizi Kirondomara akitambulisha mada zilizofundishwa alisema washiriki wamefundishwa aina za uhalifu unaovuka mipaka, usafirishaji haramu wa binadamu, usafirishaji kimagendo, ugaidi usafirishaji silaha haramu, uingizaji bidhaa feki, utakatishaji fedha, madawa ya kulevya, uhalifu wa kimtandao, na taratibu za kuingia nchini.

Aidha amebainisha madhara yanayoweza kutokea endapo wahamiaji haramu watapenya na kuingia hapa nchini, ambapo hupelekea kuhatarisha usalama wa Taifa, kuongeza mzigo serikali katika utoaji wa huduma za jamii, kuongezeka kwa vitendo vya kihalifu, kupungua kwa nafasi za ajira, kuchochea migogoro baina ya wafugaji na wakullima na pia wahamiaji holela kushiriki katika chaguzi mbalimbali za serikali.

Afisa uhamiaji mfawidhi wa kituo cha uhamiaji Horohoro, Mrakibu Singwa Mokiwa alibainisha kwamba wasafirishaji wakubwa wa wahamiaji haramu katika wilaya ya Mkinga ni madereva Bodaboda ambao hutumia vipenyo ikiwemo eneo la kijiji cha Jasini hivyo elimu hiyo imefika wakati muafaka ambapo itawasaidia madereva hao kutimiza wajibu wao bila kuvunja sheria na kuilinda nchi yao dhidi ya wahamiaji haramu.

Mrakibu Mokiwa ametoa wito kwa wananchi kwamba mlinzi namba moja wa mipaka ni mwananchi mwenyewe hivyo wananchi wanatakiwa kuwa na uzalendo na nchi yao kwa kuwafichua wahamiaji haramu ikiwemo kutoa taarifa kwa mamlaka husika.

Washiriki wa Mafunzo hayo waliotoka katika makundi mbalimbali ya kijamii walikuwa na matarajio ya kujua sheria za kuishi mipakani, kujua muhusika wa kwanza wa uhamiaji haramu, jinsi ya kumtambua mhamiaji haramu na madhara ya kupitisha wahamiaji haramu katika mipaka ya nchi yetu.

Yote hayo yalipatiwa ufumbuzi na wakufunzi Mrakibu Msaidizi wa Uhamiaji Azizi Kirondomara kutoka Kitengo cha Uhusiano Uhamiaji Makao Makuu, Bi Lucy Mseke Afisa Mradi Msaidizi IOM Tanzania na Bwana David Lukiri Kutoka Shirika la umoja wa mataifa la Wahamaji IOM.

HABARI PICHA NA MATUKIO

Yona Maki Mkuu wa Wilaya Mkinga
Washiriki wa mafunzo ya Uhamiaji wakifuatilia kwa makini mafunzo yanayoendeshwa na IOM na Idara ya Uhamiaji katika kijiji cha Jasini Wilayani Mkinga Mkoani Tanga
Afisa Uhamiaji Mfawidhi wa Kituo cha Uhamiaji Horohoro Mrakibu Singwa Mokiwa akiongea na washiriki wa mafunzo ya uhamiaji (Hawapo Pichani) katika kijiji cha Jasini kilichopo Wilayani Mkinga Mkoani Tanga mpakani mwa Tanzania na Kenya
Baadhi ya washiriki waliohudhuria Mafunzo wakiwa katika Picha ya pamoja na Viongozi wa IOM na Idara ya Uhamiaji
Mrakibu Msaidizi wa Uhamiaji Azizi Kirondomara kutoka Kitengo cha Uhusiano Uhamiaji Makao Makuu akiwasilisha moja ya mada ya madhara ya uhamiaji haramu nchini 
Lucy Mseke Afisa Mradi Msaidizi IOM Tanzania akieleza lengo la mafunzo




David Lukiri Mmoja wa wakufunzi kutoka IOM akiwafundisha washiriki mbinu za kupambana na uhamiaji haramu katika maeneo ya mipakani





Lucy Mseke kutoka IOM akifundisha moja ya mada za uhamiaji mpakani








Washiriki wakifuatilia kwa makini mada zinzofundishwa



(Picha zote na Kitengo cha Uhusiano Uhamiaji Makao Makuu)