Visitors

IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA UHAMIAJI HABARI BLOGU KARIBU KWENYE BLOG RASMI YA IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA TUNAKULETEA MATUKIO YANAYOTOKEA KILA SIKU KATIKA IDARA YA UHAMIAJI TAFADHALI TUNAOMBA TUFUATILIE PIA KATIKA MITANDAO YETU YA KIJAMII

20 Aprili 2020

Kinara wa Usafirishaji Wahamiaji Haramu Akamatwa Kyela.

Mbeya, Tanzania.
Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Mbeya Imefanikiwa Kumkamata mtuhumiwa wa usafirishaji wa wahamiaji haramu Bwana Paul Edward Kawilo, alimaarufu Mwakaniemba Mtanzania mwenye umri wa miaka 36 mkazi wa Kasumulu Wilaya ya Kyela Mkoani Mbeya.

Mtuhumiwa alikamatwa tarehe 16 Aprili ambapo anatuhumiwa kwa makosa ya kusafirisha wahamiaji haramu ambao idadi yao ni 06 raia wa  Ethiopia, raia  hao walipitishwa katika vipenyo vya Mpaka wa Isongole uliopo Wilayani Ileje Mkoani Songwe unaotenganisha nchi ya Tanzania na Malawi, kwa kutumia usafiri wa pikipiki (Bodaboda) zenye namba za usajili wa Tanzania ambazo nazo zinashikiliwa na Uhamiaji.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya Habari Afisa Uhamiaji Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACI) Msafiri Alan Shomari alieleza kwamba Mtuhumiwa alikamatwa na Afisa Uhamiaji akishirikiana vyema na askari wa Jeshi la Magereza na wananchi katika eneo la Busare Wilaya ya Kyela Mkoani Mbeya,  hata hivyo mtuhumiwa  amerudishwa Mkoani Songwe kwa ajili ya kupelekwa mahakamani Kujibu shitaka lake.

Afisa uhamiaji Mkoa wa Mbeya ametoa wito Kwa wananchi kutojihusisha na biashara hiyo kwani ni hatari kwa usalama wa nchi na mipaka yetu na hivyo amewahimiza kufanya shughuli nyingine halali zinazoweza kuwaingizia vipato.

Aidha kwa kushirikiana na Ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Songwe SACI Shomari amesema mtuhumiwa ananendelea kufanyiwa mahojiano ya kina kwa lengo la kubaini mtandao wa usafirishaji wa wahamiaji haramu ili kusambaratisha kabisa mtandao huo katika Mikoa hiyo ya kusini.
HABARI PICHA
Afisa Uhamiaji Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACI) Msafiri Alan Shomari  (kulia) akimuonesha Mtuhumiwa wa usafirishaji  wahamiji Haramu (Picha na Ofisi ya Uhusiano Uhamiaji Mkoa wa Mbeya).


 (Pikipiki  zilizokuwa zinatumika kusafirishia wahamiaji haramu Picha na Ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Songwe)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni