Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala |
Kamishna Jenerali wa
Uhamiaji Dkt. Anna Peter Makakala ameyasema hayo mapema leo hii alipofanya
ziara ya kikazi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA)
ikiwa na lengo la kujionea namna watumishi wa Idara ya Uhamiaji wanavyochukua
hatua za kujikinga dhidi ya maradhi ya Ugonjwa hatari wa Covid19 unaosababishwa
na virusi vya Corona.
Dkt. Makakala
ameupongeza uongozi wa Uwanja huo kwa kushirikiana vyema na Uhamiaji katika
kuhakikisha ulinzi na usalama wa eneo hilo, lakini pia kwa namna walivyojipanga
kujikinga na maambukizi ya maradhi ya ugonjwa wa Covid19 wakati wa utoaji
huduma za kiuhamiaji zinazoendelea kutolewa katika uwanja huo.
Aidha ameeleza kwamba,
vyombo vyote vya ulinzi na usalama viko macho katika kuhakikisha mipaka yote ya
nchi inalindwa ipasavyo katika kipindi hiki ambacho watu wengine wanaweza
kutumia kama faida ya kuhatarisha usalama wa Taifa.
“Wapo watu wanaweza
kutumia janga hili la ugonjwa wa Covid19 kuhatarisha usalama wa nchi
yetu, hivyo ni muhimu kuendelea kuwa makini katika kuilinda nchi yetu na
kuendeleza ulinzi madhubuti wa mipaka yetu kwa nguvu zetu zote, Alisema.
Mbali na hilo
Kamishna Jenerali Dkt. Makakala ametoa wito kwa Maafisa Uhamiaji Mikoa yote na
Wafawidhi wa vituo vyote vya Uhamiaji nchini kuhakikisha wanafuata taratibu
zote zinazotolewa na wataalamu wa afya katika kujikinga na maradhi hayo, na pia
kuhakikisha huduma za vifaa kinga zinakuwepo muda wote katika sehemu zote za
kutolea huduma za kiuhamiaji kwa faida ya sasa na baadae.
Kwa
upande wake Afisa Uhamiaji Mfawidhi wa Kituo cha Uwanja wa ndege wa Kimataifa (JNIA),
Naibu Kamishna wa Uhamiaji (DCI) Fredrick Kiondo amemshukuru Kamishna Jenerali
wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala kwa kuwapatia vifaa kinga mapema tu ugonjwa huo ulipoanza
kuibuka na sasa vifaa hivyo vinasaidia sana Maafisa, Askari, na wananchi kwa ujumla wanaoenda kupata huduma za kiuhamiaji kujikinga
na maambukizi yanayoweza kujitokeza.
Akitoa taarifa ya
mwenendo wa uingiaji wa abiria kwa sasa katika uwanja huo, DCI Kiondo alieleza
kwamba kwa sasa kiwango cha kupokea ndege kimeshuka sana, ambapo hapo awali walikuwa
wana uwezo wa kupokea na kuhudumia ndege karibu 19 kwa siku lakini toka ugonjwa
huu umeshika kasi idadi hiyo imeporomoka kwa kasi sana na kufikia ndege moja tu.
Ndege hiyo huweza kutua mara mbili au tatu kwa wiki na huja na abiria
wachache sana wengi wao wakiwa ni watanzania wanaorudi nyumbani na wakifika tu
wanapimwa na wataalamu wa afya kisha wanapata huduma za kiuhamiaji na baadae huchukuliwa na magari maalumu ya serikali kwa ajili ya kuwapeleka karantini ya siku 14 kwa ungalizi na vipimo zaidi kama maagizoya serikali yanavyoelekeza.
HABARI PICHA NA MATUKIO
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala akinawa mikono mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa (JNIA Terminal III) Katika ziara yake ya kikazi |
Eneo linalotumiwa na wateja mbalimbali wanaowasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa (JNIA) kunawa mikono ikiwa ni juhudi za kujikinga na maambukizi ya Corona |
Maofisa Uhamiaji wa kituo cha JNIA Wakijiandaa kumpokea Kamishna Jenerali wa Uhamiaji (Kushoto) ni Msemaji Mkuu wa Uhamiaji Mrakibu Paul Mselle |
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala akipokea maelezo ya huduma zinavyotelewa katika kiwanja hicho kutoka kwa Mfawidhi wa Kituo hicho Naibu Kamishna wa Uhamiaji (DCI) Fredrick Kiondo |
Baadhi ya kaunta zinazotoa huduma za kiuhamiaji |
|
Muonekano wa nje wa Jengo la Abiria Terminal III Katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa JNIA (Picha zote na Kitengo cha Uhusiano Uhamiaji Makao Makuu) |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni