Idara ya Uhamiaji Mkoa
wa Arusha imeimarisha Udhibiti wa uingiaji wa Watu Nchini ili kujilinda na
Maambukizi ya ugonjwa wa Corona.
Wakitekeleza Maelekezo ya Serikali kupitia Waziri wa Afya
kwamba watu wote wanaoingia nchini kuwekwa Karantini kwa muda wa siku 14 kwa
gharama zao, Idara ya Uhamiaji Mkoani Arusha tayari imewakamata raia wa Tanzania
131 ambao wamerejea nchini wakitokea nchini Kenya kwa kupita katika vipenye
visivyo rasmi (njia za panya) katika Maeneo ya Namanga, zoezi ambalo linafanywa
na Idara ya Uhamiaji kwa ushirikiano na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama
pamoja na Wataalam wa Wizara ya Afya.
Akizungumzia namna Idara
ya Uhamiaji ilivyojipanga Kuthibiti Mipaka, Afisa Uhamiaji Mkoa wa Arusha Naibu
Kamishna wa Uhamiaji Abdallah Towo amethibitisha kukamatwa kwa raia hao wa
Tanzania, pamoja na raia 3 wa Kenya ambao tayari wamerudishwa nchini kwao.
Akifafanua zaidi,
Kamanda Towo ameeleza kuwa Watanzania
wote 131 wamewekwa Karantini katika ya
Shule ya Sekondari Namanga na kwenye Hotel maalum zilizotengwa kwa ajili
ya shughuli hiyo.
Taarifa yake inaongeza
kuwa, Idara ya Uhamiaji inazishikilia jumla ya pikipiki 2 (Moja yenye usajili
wa Kenya na nyingine Tanzania) ambazo zimetumiwa na baadhi yao kuingia nchini.
Ameendelea kueleza kuwa
baada ya kuwahoji washikiliwa hao ilibainika kuwa kati yao ni raia 11 tu ndio
walikuwa na Hati za Dharura za Kusafiria za Tanzania. Aidha, wengine
wamechana/kuzitupa hati zao wakati walipokuwa wanavuka Mpaka ili kukwepa
kutambuliwa kwa urahisi na kukwepa kuwekwa karantini.
Akihitimisha taarifa
yake, Kamanda Towo amesisitiza kuwa Watu hao wote wamewekwa Karantini kwa muda
wa Siku 14 kwa gharama zao kama ilivyoamriwa na Mamlaka zinazosimamia Ulinzi na
Usalama Mkoani Arusha.
Aidha, Idara ya Uhamiaji
inatoa wito kwa Watanzania na Wageni wote wanaoingia nchini kupita kwenye
Mipaka ambayo imeanishwa kisheria, kwani kutumia njia za panya ni kosa kwa Mujibu
wa Sheria ya Uhamiaji Sura 54, Rejeo la Mwaka 2016.
Pia Idara inatoa wito
kwa wananchi wanaoishi maeneo ya mipakani kushirikiana na serikali katika
kipindi hiki kwa kutoa taarifa za watu wanaoingia nchini bila kufuata taratibu
ili waweze kuchukuliwa hatua na kuwekwa karantini ili kuepuka kusambaa kwa
virusi vya corona bila kujua chanzo chake.
Afisa Uhamiaji Mkoa wa Arusha Naibu Kamishna wa Uhamiaji Abdallah Towo |
Pikipiki zilizokamatwa zikihusishwa na uvushaji wa watu katika njia zisizo rasmi katika eneo la Namanga mkoani Arusha |
Baadhi ya raia wa Tanzania waliokamatwa na Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Arusha wakiwa ndani ya ofisi ya Kituo cha Uhamiaji Namanga. |
Baadhi ya raia wa Tanzania waliokamatwa na Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Arusha wakiwa ndani ya ofisi ya Kituo cha Uhamiaji Namanga. |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni