Mkuu wa Mkoa wa Rukwa
Mh. Joachim Leonard Wangabo akiambatana na Afisa Uhamiaji Mkoa, Naibu Kamishna
wa Uhamiaji DCI Elizeus Mushongi na Mganga Mkuu wa Mkoa, wamefanya ziara ya ukaguzi wa vipenyo haramu katika Wilaya ya
Nkasi Mkoani humo, ikiwa ni utekelezaji wa kupambana na kudhibiti maambukizi ya
Ugonjwa wa COVID-19 unaosababishwa na Virusi vya Corona.
Katika ziara hiyo
elimu ya sheria za Uhamiaji na jinsi ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa
COVID-19 ilitolewa katika vituo vya Kabwe, Kirando na Wampembe kwa kuongea na
Watendaji wa Kata na vijiji, madiwani, wenyeviti wa vijiji na vitongoji.
Ziara hiyo ilihitimishwa
Jumapili ya pasaka kwa kusali na kuongea na waumini wa Kanisa Katoliki Parokia
ya Namanyere, wilayani Nkasi, ambapo pia walipata fursa ya kutoa elimu kwa
waumini.
Mhe. Wangabo alitoa
wito kwa wananchi wa Mkoa huo kuhakikisha wanafuata ushauri unaotolewa na
wataalamu wa Afya na kutopokea wageni wanaoweza kuingia nchini kinyume na
sheria, sanjari na kuhakikisha boti zote zinazoingia katika mwambao mwa ziwa
Tanganyika kupitia katika vituo vilivyo rasmi, ili kufanyiwa vipimo hali
itakayopunguza maambukizi virusi vya Corona.
Akitoa taarifa fupi ya ziara hiyo Afisa Uhamiaji
Mkoa wa Rukwa DCI Mushongi alieleza kwamba takribani watu 45 waliotoka nje ya
nchi kupitia mpaka wa mwambao wa Ziwa Tanganyika wamewekwa karantini Mkoani
humo baada ya kumaliza taratibu za kiuhamiaji, ambapo Kirando katika ziwa
Tanganyika ina idadi ya watu 22, Kabwe 17, Kasesya 03, na Sumbawanga Mjini 03.
Zoezi hilo la kuwaweka
karantini wageni na raia wa Tanzania wanaoingia hapa nchini kupitia mipaka
mbalimbali ni utekelezaji wa maelekezo ya serikali kwa wananchi na wageni
wanaongia nchini kujitenga kwa siku 14
kwa kujitegemea.
Raia hao na wageni
walioingia nchini hivi karibuni mpaka sasa wako chini ya uangalizi wa wataalamu
wa Afya kwa ajili ya kuafanyiwa vipimo kuhusu hali zao za kiafya.
Aidha katika idadi
hiyo ya waliowekwa karantini watanzania ni 40, raia wa Congo 04 na raia 01
mwenye asili ya Omani.
Jeshi la Uhamiaji chini
ya Kamishna Jenerali Dkt. Anna Makala linaendelea kuwa hodari na shupavu
katika kutimiza majukumu yake ya msingi katika kulinda mipaka ya nchi na
kuendesha doria za mara kwa mara katika mipaka yote na kudhibiti vipenyo
vinavyosadikika kupitisha wahamiaji haramu ili kulinda Amani na Usalama wa nchi
yetu.
HABARI PICHA NA MATUKIO
Naibu Kamishna wa Uhamiaji Elizeus Mushongi akitoa elimu ya sheria za uhamiaji kwa Watendaji wa Kata na vijiji, madiwani, wenyeviti wa vijiji na vitongoji (hawapo pichani) |
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (katikati) akiwa na Naibu Kamishna wa Uhamiaji Mkoa (kushoto), katika ibada ya pasaka iliyofanyika katika kanisa Katoliki Parokia ya Namanyere |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni