Visitors

IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA UHAMIAJI HABARI BLOGU KARIBU KWENYE BLOG RASMI YA IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA TUNAKULETEA MATUKIO YANAYOTOKEA KILA SIKU KATIKA IDARA YA UHAMIAJI TAFADHALI TUNAOMBA TUFUATILIE PIA KATIKA MITANDAO YETU YA KIJAMII

26 Novemba 2019

RAIS MAGUFULI AWEKA JIWE LA MSINGI KATIKA JENGO LA OFISI YA UHAMIAJI MAKAO MAKUU DODOMA
Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt John Pombe Joseph Magufuli ameweka jiwe la Msingi katika ujenzi wa Mradi wa Jengo la Uhamiaji Makao Makuu Dodoma.

Akizungumza katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi, Mhe. Rais alisema amefurahishwa na kiwango cha ubora wa jengo hilo na kuongeza kuwa, mara baada ya kukamilika ujenzi huo, Jengo hilo la Uhamiaji litaboresha mandhari ya jiji la Dodoma.

Hata hivyo, Mhe. Rais alimtaka Mshauri Mwelekezi katika Mradi huo Prof. Evaristo Liwa kwa kushirikiana na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni kupitia upya gharama za Mradi huo na kuhakikisha gharama hizo zinashuka kutoka bilioni 30 hadi kufikia chini ya bilioni 20.

Aidha, Mhe. Rais alitumia fursa hiyo kumpongeza Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Peter Makakala kwa kazi nzuri inayofanywa na Idara hiyo hasa katika udhibiti wa Wahamiaji Haramu kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama.

Kwa upande mwingine, Mhe. Rais aliwataka Makamanda na Watumishi wa Idara ya Uhamiaji kuchapa kazi kazi kwa uadilifu na kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zinazowaongoza katika utekelezaji wa majukumu yao.

Akielezea maendeleo ya Mradi huo, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt Makakala alisema, ujenzi wa Jengo hilo umefikia asilimia 20 na kuongeza kuwa kasi ya ujenzi ni nzuri. Aidha, Dkt. Makakala alimshukuru Mhe. Rais kwa misaada mbalimbali ambayo amekuwa akiitoa kwa Idara ya Uhamiaji katika kipindi cha miaka minne tangu aingie madarakani, ikiwemo kiasi cha shilingi bilioni kumi kwa ajili ya kuanza ujenzi wa jengo hilo la Uhamiaji Makao Makuu Dodoma, ambazo alizitoa wakati wa Uzinduzi wa Mradi wa Uhamiaji Mtandao mwezi Januari, mwaka 2018.


Mradi wa Ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Uhamiaji Makao Makuu upo katika eneo la National Capital City jijini Dodoma, likiwa ni eneo lenye ukubwa wa mita za mraba 13,260. Mradi huo unatekelezwa na Kampuni ya Suma JKT chini ya Mshauri Mwelekezi kutoka Chuo Kikuu Ardhi. Mradi huo ulianza kutekelezwa tarehe 27 Mei, 2019 na unatarajia kukamilika ifikapo tarehe 27 Novemba, 2020.

21 Novemba 2019

MKUTANO WA WAKUU WA IDARA ZA UHAMIAJI NA KAZI WA TANZANIA NA UGANDA WAFANYIKA JIJINI DAR ES SALAAM

Kamishna wa Uhamiaji (Vibali na Pasi), Mary Palmer akiongea wakati wa mkutano huo.

Kamishna Palmer akimkabidhi zawadi Mkurugenzi Mkuu wa Uraia na Masuala ya Uhamiaji wa Uganda Meja Jenerali Apollo Kassita-Gowa mara bada ya mkutano huo.


Mkurugenzi Mkuu wa Uraia na Masuala ya Uhamiaji wa Uganda Meja Jenerali Apollo Kassita-Gowa akimkabidhi zawadi Kamishna wa Uhamiaji Mary Palmer (ndc) ambaye pia ndiye aliyeongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo.Kamishna  wa Uhamiaji Mary Palmer (ndc), anayesimamia Divisheni ya Vibali, Pasi na Visa, aliongoza ujumbe wa Idara ya Uhamiaji Tanzania katika Mkutano wa Wakuu wa Idara za Uhamiaji na Kazi za Tanzania na Uganda uliofanyika Makao Makuu ya Uhamiaji jijini Dar es salaam.

Lengo la mkutano huo ni kuzikutanisha nchi za Tanzania na  Uganda ili kujadili na kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali hususan  za kiuhamiaji zilizopo baina ya nchi hizo.

Katika Mkutano huo, Kamishna Palmer alimuwakilisha Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt Anna Peter Makakala, ambaye yuko nje ya Ofisi kwa majukumu mengine ya kikazi. Aidha, ujumbe kutoka Uganda uliongozwa na Meja Jenerali Apollo Kasiita-Gowa, ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Uraia na Masuala ya Kiuhamiaji nchini Uganda.

Akizungumza wakati wa mkutano huo Kamishna Palmer alisema, ushirikiano baina ya nchi hizo mbili ni muhimu sana katika kuimarisha udhibiti wa masuala mbalimbali ya kiuhamiaji. Pia aliongeza kusema kuwa mkutano huo utasaidia kuongeza kasi ya kuondoa vikwazo vya safari baina ya raia wa nchi za Tanzania na Uganda.

Kwa upande wake Meja Jenerali Apollo Kasiita -Gowa akieleza umuhimu wa mkutano huo alisema, sio tu utakuwa ni chachu katika kuongeza mtangamano na mshikamano baina ya wananchi wa pande zote mbili bali pia utasaidia katika kurahisisha taratibu za kiuhamiaji baina ya raia wa nchi mbii hizo, pamojana kuimamarisha udhibiti wa uhalifu unaovuka mipaka (Transanational Crimes).


Mkutano huo ni mwendelezo wa Mkutano wa tatu wa Wakuu wa Idara za Uhamiaji na Kazi baina ya nchi za Tanzania na Uganda uliofanyika jijini Kampala, Uganda mwezi Novemba mwaka jana.

18 Novemba 2019

Mbaroni kwa kujifanya Afisa Uhamiaji
Afisa Uhamiaji ‘Feki’ Bushiri Ally Nassoro  mwenye  umri wa miaka 19 leo tarehe 18 Novemba 2019, amekamatwa na Maafisa Uhamiaji kwa tuhuma za kuwatapeli na kuwalaghai wateja wanaokuja kupata huduma za Kiuhamiaji katika ofisi ya Uhamiaji Makao Makuu Kurasini jijini Dar es salaam.

Katika mahojiano ya awali, Afisa huyo Feki  pia aligundulika  kudanganya kama Afisa Usalama wa Taifa. Kijana huyo tapeli ambaye anadai ameanza kulaghai wateja tangu mwaka 2017 bado anaendelea kushikiliwa na kuhojiwa kwa uchunguzi zaidi.

05 Novemba 2019

UHAMIAJI YAWAPIGA MSASA MABALOZI WATEULE

Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt Anna Peter Makakala leo ameongoza Ujumbe wa Mabalozi kumi na mbili katika Mafunzo ya huduma mbalimbali za kiuhamiaji zinazotolewa katika Balozi za Tanzania Nje ya Nchi. Mabalozi hao wameteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli hivi karibuni.


Katika mafunzo hayo, mada mbalimbali ziliweza kuwasilishwa na Maafisa kutoka Idara ya uhamiaji hususan Pasipoti, Visa za kielektroniki, Huduma za kibalozi (Consular Services) pamoja na Mifumo inayotumika katika utoaji wa Pasipoti na visa za kieletroniki.


Aidha, Waheshimiwa mabalozi walipata fursa ya kutembelea na kujionea namna mifumo mbalimbali ya Uhamiaji inavyofanya kazi na kuonyesha kufurahishwa na jinsi mifumo hiyo inavyorahisisha utoaji wa huduma za uhamiaji kwa haraka na kwa ufanisi mkubwa.


Kwa upande wake Balozi wa Tanzania Nchini Kuwait, Mheshimiwa Aisha S. Amour kwa niaba ya mabalozi wenzake alimshukuru na Kumpongeza Kamishna Jenerali wa Uhamiaji kwa mafunzo waliyoyapata. Pia ameongeza kuwa, mafunzo hayo yatawajengea uwezo wa kufanya kazi kwa ufanisi hususani katika kuwahudumia Watanzania waishio nje ya nchi na wageni wanaoingia  hapa nchini kwa madhumuni mbalimbali ikiwemo utalii, matembezi, Biashara na uwekezaji.


Baadhi ya waheshimiwa Mabalozi  waliohudhuria mafunzo hayo ni pamoja na Maj Gen, Gaudence Milanzi, Mohamed A. Mtonga, H.A Kattanga, Aisha S. Amour, Prof. Emmanuel D. Mbennah, Ali J.Mwadini, Dkt. Jilly E. Maleko pamoja na Dkt. Modestus F. Kipilimba.