Mhe. Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt John Pombe Joseph Magufuli
ameweka jiwe la Msingi katika ujenzi wa Mradi wa Jengo la Uhamiaji Makao Makuu
Dodoma.
Akizungumza katika hafla ya
uwekaji wa jiwe la msingi, Mhe. Rais alisema amefurahishwa na kiwango cha ubora
wa jengo hilo na kuongeza kuwa, mara baada ya kukamilika ujenzi huo, Jengo hilo
la Uhamiaji litaboresha mandhari ya jiji la Dodoma.
Hata hivyo, Mhe. Rais
alimtaka Mshauri Mwelekezi katika Mradi huo Prof. Evaristo Liwa kwa
kushirikiana na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni
kupitia upya gharama za Mradi huo na kuhakikisha gharama hizo zinashuka kutoka
bilioni 30 hadi kufikia chini ya bilioni 20.
Aidha, Mhe. Rais alitumia
fursa hiyo kumpongeza Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Peter Makakala
kwa kazi nzuri inayofanywa na Idara hiyo hasa katika udhibiti wa Wahamiaji
Haramu kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama.
Kwa upande mwingine, Mhe.
Rais aliwataka Makamanda na Watumishi wa Idara ya Uhamiaji kuchapa kazi kazi
kwa uadilifu na kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zinazowaongoza katika
utekelezaji wa majukumu yao.
Akielezea maendeleo ya Mradi
huo, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt Makakala alisema, ujenzi wa Jengo hilo
umefikia asilimia 20 na kuongeza kuwa kasi ya ujenzi ni nzuri. Aidha, Dkt.
Makakala alimshukuru Mhe. Rais kwa misaada mbalimbali ambayo amekuwa akiitoa
kwa Idara ya Uhamiaji katika kipindi cha miaka minne tangu aingie madarakani,
ikiwemo kiasi cha shilingi bilioni kumi kwa ajili ya kuanza ujenzi wa jengo
hilo la Uhamiaji Makao Makuu Dodoma, ambazo alizitoa wakati wa Uzinduzi wa
Mradi wa Uhamiaji Mtandao mwezi Januari, mwaka 2018.
Mradi wa Ujenzi wa Jengo la
Ofisi ya Uhamiaji Makao Makuu upo katika eneo la National Capital City jijini
Dodoma, likiwa ni eneo lenye ukubwa wa mita za mraba 13,260. Mradi huo
unatekelezwa na Kampuni ya Suma JKT chini ya Mshauri Mwelekezi kutoka Chuo
Kikuu Ardhi. Mradi huo ulianza kutekelezwa tarehe 27 Mei, 2019 na unatarajia
kukamilika ifikapo tarehe 27 Novemba, 2020.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni