Visitors

IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA UHAMIAJI HABARI BLOGU KARIBU KWENYE BLOG RASMI YA IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA TUNAKULETEA MATUKIO YANAYOTOKEA KILA SIKU KATIKA IDARA YA UHAMIAJI TAFADHALI TUNAOMBA TUFUATILIE PIA KATIKA MITANDAO YETU YA KIJAMII

25 Juni 2021

KAMISHNA JENERALI WA UHAMIAJI, DKT. A.P. MAKAKALA, AFUNGUA WARSHA KUHUSU USALAMA WA MIPAKA KWA NJIA YA MTANDAO




Kamishna  Jenerali wa Uhamiaji DKT. A. P. Makakala mapema wiki hii afungua warsha kuhusu Usalama wa Mipaka, warsha hiyo inayoendeshwa katika Chuo cha Uhamiaji cha Kikanda (TRITA) Moshi, ilifunguliwa na Kamishna Jenerali kwa njia ya mtandao akiwa Zanzibar.

 
Katika hotuba yake Dkt. Makakala alifahamisha kuwa usalama wa mipaka lazima upewe kipaumbele hasa kwa kuzingatia maendeleo ya sayansi na teknolojia ambayo yanachangia uhalifu unaovuka mipaka (Transnational Organized Crimes) duniani kote.

Dkt. Makakala aliwataka washiriki wa warsha hiyo kuwa makini na kuzingatia mafunzo watakayopatiwa ili waweze kuwafundisha wenzao ambao hawakupata fursa ya kushiriki mafunzo hayo pamoja na kuwataka kutumia mbinu mpya walizofundishwa katika marsha hiyo katika kudhibiti Uhalifu unaovuka mipaka.

Maafisa 32 walioshiriki katika warsha hiyo kutoka vituo mbali mbali vya kuingilia na kutokea watu nchini kutoka Tanzania Bara na Zanzibar walijifunza ukaguzi wa nyaraka, mienendo na mabadiliko ya mbinu za kudhibiti ugaidi, dawa za kulevya, umuhimu wa intelijensia katika kusimamia ulinzi na usalama wa mipaka pamoja na matumizi ya mifumo mbalimbali ya Uhamiaji.


 

MATUKIO KATIKA PICHA: ZIARA YA NAIBU WAZIRI MAMBO YA NDANI YA NCHI UHAMIAJI

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Khamis Hamza Khamis amefanya ziara kutembelea ofisi za Uhamiaji Makao Makuu pamoja na kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo Uhamiaji Makao Makuu jijini Dodoma siku ya Alhamis tarehe 24 Juni, 2021.

Mhe. Khamis akiwa Uhamiaji Makao Makuu eneo la Uzunguni, alipata wasaa wa kuongea na Maafisa, Askari na Watumishi wa Uhamiaji Makao Makuu na kuwataka kuchapa kazi kwa weledi, kujiepusha na vitendo vya rushwa na kuzingatia sheria za nchi katika kuwahudumia raia wa Tanzania na Wageni.

Awali, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Peter Makalala akisoma taarifa ya Utendaji kazi wa Idara ya Uhamiaji alisema kwamba anaishukuru serikali kwa kuwapandisha vyeo maafisa, askari na watumishi wa kada ya kiraia zaidi ya 1000.

Naibu waziri baadae alielekea eneo linapojengwa jengo la Uhamiaji Makao Makuu na kukagua hatua zilizofikiwa katika ujenzi huo na kuwataka wakandarasi kuharakisha ujenzi huo ikibidi kufanya kazi usiku na mchana ili kabla ya kuisha mwaka huu basi jengo hilo lianze kutumika.

Hii ni mara ya kwanza kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Mhe. Khamis Hamza Khamis kutembelea idara ya Uhamiaji toka ateuliwe kuwa naibu waziri mwishoni mwa mwaka jana na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ambapo mabadiliko yaliyofanya na Rais wa sasa Mhe. Samia Suluhu hassan hayakuathiri wizara ya mambo ya ndani.


Dkt. Anna Makakala akisoma taarifa ya Utendaji kazi wa Idara ya Uhamiaji mbele ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Mhe. Khamis Hamza Khamis

Baadhi ya Maafisa, Askari na watumishi wa Idara ya Uhamiaji wakimsikiliza Mhe. Khamis wakati akiongea nao nje ya jengo ya ofisi za Makao Makuu ya Uhamiaji Dodoma


Naibu Waziri Mhe. Khamis Hamza Khamis akiandika katika kumbukumbu zake wakati akiskiliza taarifa kutoka kwa Dkt. Makakala





Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Khamis Hamza Khamis akiongea na Maafisa, Askari na Watumishi wa Idara ya Uhamiaji Dodoma

Picha ya Pamoja: Naibu Waziri pamoja na Viongozi waandamizi wa Idara ya Uhamiaji, kushoto ni Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala na kulia kwa waziri ni Kamishna wa Uhamiaji (Pasipoti na Uraia) Gerald Kihinga.



Kamishna wa Uhamiaji (Utawala na Fedha) Hamza Ismail Shaabani akitoa taarifa ya maendeleo wa jengo la Uhamiaji Makao Makuu jijini Dodoma








 

11 Juni 2021

KAMISHNA WA UHAMIAJI ZANZIBAR AWATAKA WANANCHI KUFICHUA WAHAMIAJI WASIOFUATA SHERIA






Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar Johari Masoud Sururu mapema wiki hii atembelea vipenyo mbali mbali katika Mkoa wa Kusini na Kaskazini Pemba ili kujionea mazingira halisi pamoja na kutoa elimu kwa Wananchi juu ya umuhimu wakushirikiana na Idara ya Uhamiaji katika kutoa taarifa kwa Wahamiaji wasiofuata sheria za Uhamiaji.

Akizungumza na Wananchi wanaoishi pembezoni mwa vipenyo vya mto wa kuwa na Mkia wa ng’ombe huko Kaskazini Pemba aliwataka wananchi kushiriki katika kuimarisha ulinzi kwenye vipenyo kwa kutoa taarifa kwa Idara ya Uhamiaji kuhusu chombo chochote kinachokusudia au kuonekana katika eneo hilo ili taratibu za kisheria ziweze kuchukuliwa.

Kamishna Sururu aliwafahamisha Wananchi hao athari za Uhamiaji haramu ikiwa ni pamoja na kuhatarisha usalama wa nchi na Serikali kukosa mapato yatokanayo na malipo ya visa.

Aidha Wananchi walitaka kupatiwa elimu zaidi ya Uhamiaji ili wawe na uwezo wa kuwabaini Wahamiaji Haramu katika maeneo yao. Wananchi hao waliahidi kutoa mashirikiano na Idara ya Uhamiaji.

Nae Sheha wa Shehia ya Gando Maalim Karim Mangunja alibainisha kuwa hakuna vyombo vya kigeni vinavyoingia katika vipenyo hivyo hata hivyo aliahidi pale ikitokea chombo chochote ikitakachotiliwa shaka ataijuilisha Idara ya Uhamiaji.