Visitors

IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA UHAMIAJI HABARI BLOGU KARIBU KWENYE BLOG RASMI YA IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA TUNAKULETEA MATUKIO YANAYOTOKEA KILA SIKU KATIKA IDARA YA UHAMIAJI TAFADHALI TUNAOMBA TUFUATILIE PIA KATIKA MITANDAO YETU YA KIJAMII

31 Agosti 2019

IDARA YA UHAMIAJI YATAKIWA KUJIIMARISHA KATIKA KUVUTIA WAWEKEZAJI NCHINI








Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe Kangi Lugola ameitaka Idara ya Uhamiaji kuimarisha uwekezaji nchini. Wito huo umetolewa leo Mjini Moshi wakati akifungua Mkutano wa Maafisa Uhamiaji Waandamizi  unao lenga kujadili na kutathmini utendaji kazi wa Idara ya Uhamiaji.

Akizungumza na Maafisa hao, Waziri Lugola amesisitiza kuwa nchi yetu inazo fursa nyingi za kiuchumi na Utalii hivyo kuwavutia wageni na wawekezaji wengi kuiingia na kuwekeza nchini.

“Katika utendaji kazi wake,Idara ya uhamiaji ndio kioo/taswira ya nchi yetu hivyo  tufanye kazi kwa weledi na kuweka mazingira bora ya uwekezaji na kuwahudumia wageni kwa ukarimu, lugha za staha na msiwe kikwazo cha uwekezaji na utalii nchini” alisema Waziri Lugola.

Aidha, Waziri Lugola amemuagiza Kamishna Jenerali wa Uhamiaji kusimamia kikamilifu Ukusanyaji wa Maduhuli ya Serikali na kudhibiti mianya inayopelekea upotevu wa maduhuli.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjro, Mhe. Anna Mghwira ametoa wito kwa Idara ya Uhamiaji kushiriki kikamilifu katika zoezi la uandikishaji na utoaji wa Vitambulisho vya Taifa (NIDA).

“Mkoa wa Kilimanjaro una idadi kubwa ya Wahamiaji haramu kutokana na jiografia yake pamoja na kuwepo kwa fursa mbalimbali za uwekezaji na utalii. Ili kukabiliana na changamoto hii, Idara iimarishe udhibiti wa mipaka ya nchi yetu ikiwa ni sambamba na kuwatambua Watanzania na raia wa kigeni wanaoishi na kufanya kazi nchini”, aliongeza Mhe. Mghwira.

Mhe. Mghwira ameitaka pia Idara ya Uhamiaji kujenga mahusiano na Wananchi ili kupata taarifa za haraka na sahihi kutoka kwa wananchi hao.

“Nitoe wito kwa Idara ya Uhamiaji kubuni mbinu na mikakati kwa Maafisa wake kushuka chini kwa Wananchi ili kuwa karibu zaidi na jamii na Watanzania kwa ujumla. Kwa kufanya hivyo Wananchi watajua haki zao ikiwa pamoja na kufahamu vielelezo vinavyotakiwa katika kupata huduma za Idara ikiwamo Pasipoti sanjali na kutoa taarifa juu ya uwepo wa wahamiaji haramu katika maeneo yao  amesisitiza Mhe. Mghwira.

Awali akimkaribisha Mhe. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi katika Mkutano huo, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Peter Makakala amesema kuwa Idara imezindua mpango mkakati wa kudhibiti Uhamiaji nchini. Mpango huo unalenga kuwatambua na kuwaorodhesha wahamiaji wote nchini na zoezi hilo litafanyika nchi nzima kwa kuanzia Mkoa wa Dar es Salaam.

Katika utekelezaji wake, mpango huo utahusisha Viongozi wa Serikali za Mitaa au Vijiji (MEO/VEO), Maafisa Watendaji wa Kata (WEO) na kuratibiwa na Idara ya Uhamiaji. Kupitia Mpango huo Idara itaimarisha udhibiti na usimamizi wa mipaka yetu, kuimarisha ulinzi na Usalama na pia kulipatia ufumbuzi suala la Wahamiaji Walowezi. 

30 Agosti 2019

WAZIRI LUGOLA KUFUNGUA MKUTANO WA MAAFISA UHAMIAJI WAANDAMIZI


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mheshimiwa Kangi Lugola kesho Jumamosi tarehe 31 Agosti anatarajiwa kufungua mkutano wa Maafisa Uhamiaji Waandamizi kutoka mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar.  

Akitoa taarifa hiyo mjini Moshi leo, Msemaji Mkuu wa Idara ya Uhamiaji Mrakibu Mwandamizi Alhaji Ally Mtanda amesema kuwa mkutano huo wa siku mbili chini ya Uenyekiti wa Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Peter Makakala utafanyika katika Chuo cha Kikanda cha Uhamiaji (TRITA) mjini Moshi una lenga kujadili na kutathmini utendaji kazi wa idara pamoja na kukumbushana masuala mbalimbali hususan Sheria, Kanuni na Taratibu ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na raia wa kigeni.

“Mkutano huu utahudhuriwa na Makamishna wa Uhamiaji, Maafisa Uhamiaji Mikoa yote Tanzania na Zanzibar, Wakuu wa Vitengo pamoja na Wafawidhi wa Vituo vya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume (AAKIA), Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), Namanga, Tunduma na Bandari ya Zanzibar.” Aliongeza Alhaji Mtanda.