Visitors

IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA UHAMIAJI HABARI BLOGU KARIBU KWENYE BLOG RASMI YA IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA TUNAKULETEA MATUKIO YANAYOTOKEA KILA SIKU KATIKA IDARA YA UHAMIAJI TAFADHALI TUNAOMBA TUFUATILIE PIA KATIKA MITANDAO YETU YA KIJAMII

20 Aprili 2020

Kinara wa Usafirishaji Wahamiaji Haramu Akamatwa Kyela.

Mbeya, Tanzania.
Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Mbeya Imefanikiwa Kumkamata mtuhumiwa wa usafirishaji wa wahamiaji haramu Bwana Paul Edward Kawilo, alimaarufu Mwakaniemba Mtanzania mwenye umri wa miaka 36 mkazi wa Kasumulu Wilaya ya Kyela Mkoani Mbeya.

Mtuhumiwa alikamatwa tarehe 16 Aprili ambapo anatuhumiwa kwa makosa ya kusafirisha wahamiaji haramu ambao idadi yao ni 06 raia wa  Ethiopia, raia  hao walipitishwa katika vipenyo vya Mpaka wa Isongole uliopo Wilayani Ileje Mkoani Songwe unaotenganisha nchi ya Tanzania na Malawi, kwa kutumia usafiri wa pikipiki (Bodaboda) zenye namba za usajili wa Tanzania ambazo nazo zinashikiliwa na Uhamiaji.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya Habari Afisa Uhamiaji Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACI) Msafiri Alan Shomari alieleza kwamba Mtuhumiwa alikamatwa na Afisa Uhamiaji akishirikiana vyema na askari wa Jeshi la Magereza na wananchi katika eneo la Busare Wilaya ya Kyela Mkoani Mbeya,  hata hivyo mtuhumiwa  amerudishwa Mkoani Songwe kwa ajili ya kupelekwa mahakamani Kujibu shitaka lake.

Afisa uhamiaji Mkoa wa Mbeya ametoa wito Kwa wananchi kutojihusisha na biashara hiyo kwani ni hatari kwa usalama wa nchi na mipaka yetu na hivyo amewahimiza kufanya shughuli nyingine halali zinazoweza kuwaingizia vipato.

Aidha kwa kushirikiana na Ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Songwe SACI Shomari amesema mtuhumiwa ananendelea kufanyiwa mahojiano ya kina kwa lengo la kubaini mtandao wa usafirishaji wa wahamiaji haramu ili kusambaratisha kabisa mtandao huo katika Mikoa hiyo ya kusini.
HABARI PICHA
Afisa Uhamiaji Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACI) Msafiri Alan Shomari  (kulia) akimuonesha Mtuhumiwa wa usafirishaji  wahamiji Haramu (Picha na Ofisi ya Uhusiano Uhamiaji Mkoa wa Mbeya).


 (Pikipiki  zilizokuwa zinatumika kusafirishia wahamiaji haramu Picha na Ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Songwe)


15 Aprili 2020

#COVID-19 Uhamiaji Rukwa Kupambana na Vipenyo Haramu Kudhibiti Corona

Rukwa, Tanzania
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Leonard Wangabo akiambatana na Afisa Uhamiaji Mkoa, Naibu Kamishna wa Uhamiaji DCI Elizeus Mushongi na Mganga Mkuu wa Mkoa, wamefanya ziara ya  ukaguzi wa vipenyo haramu katika Wilaya ya Nkasi Mkoani humo, ikiwa ni utekelezaji wa kupambana na kudhibiti maambukizi ya Ugonjwa wa COVID-19 unaosababishwa na Virusi vya Corona.

Katika ziara hiyo elimu ya sheria za Uhamiaji na jinsi ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19 ilitolewa katika vituo vya Kabwe, Kirando na Wampembe kwa kuongea na Watendaji wa Kata na vijiji, madiwani, wenyeviti wa vijiji na vitongoji.

Ziara hiyo ilihitimishwa Jumapili ya pasaka kwa kusali na kuongea na waumini wa Kanisa Katoliki Parokia ya Namanyere, wilayani Nkasi, ambapo pia walipata fursa ya kutoa elimu kwa waumini.

Mhe. Wangabo alitoa wito kwa wananchi wa Mkoa huo kuhakikisha wanafuata ushauri unaotolewa na wataalamu wa Afya na kutopokea wageni wanaoweza kuingia nchini kinyume na sheria, sanjari na kuhakikisha boti zote zinazoingia katika mwambao mwa ziwa Tanganyika kupitia katika vituo vilivyo rasmi, ili kufanyiwa vipimo hali itakayopunguza maambukizi virusi vya Corona.

Akitoa taarifa fupi ya ziara hiyo Afisa Uhamiaji Mkoa wa Rukwa DCI Mushongi alieleza kwamba takribani watu 45 waliotoka nje ya nchi kupitia mpaka wa mwambao wa Ziwa Tanganyika wamewekwa karantini Mkoani humo baada ya kumaliza taratibu za kiuhamiaji, ambapo Kirando katika ziwa Tanganyika ina idadi ya watu 22, Kabwe 17, Kasesya 03, na Sumbawanga Mjini 03.

Zoezi hilo la kuwaweka karantini wageni na raia wa Tanzania wanaoingia hapa nchini kupitia mipaka mbalimbali ni utekelezaji wa maelekezo ya serikali kwa wananchi na wageni wanaongia  nchini kujitenga kwa siku 14 kwa kujitegemea.
Raia hao na wageni walioingia nchini hivi karibuni mpaka sasa wako chini ya uangalizi wa wataalamu wa Afya kwa ajili ya kuafanyiwa vipimo kuhusu hali zao za kiafya.

Aidha katika idadi hiyo ya waliowekwa karantini watanzania ni 40, raia wa Congo 04 na raia 01 mwenye asili ya Omani.

Jeshi la Uhamiaji chini ya Kamishna Jenerali Dkt. Anna Makala linaendelea kuwa hodari na shupavu katika kutimiza majukumu yake ya msingi katika kulinda mipaka ya nchi na kuendesha doria za mara kwa mara katika mipaka yote na kudhibiti vipenyo vinavyosadikika kupitisha wahamiaji haramu ili kulinda Amani na Usalama wa nchi yetu.

HABARI PICHA NA MATUKIO
Naibu Kamishna wa Uhamiaji Elizeus Mushongi akitoa elimu ya sheria za uhamiaji kwa Watendaji wa Kata na vijiji, madiwani, wenyeviti wa vijiji na vitongoji (hawapo pichani)

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (katikati) akiwa na Naibu Kamishna wa Uhamiaji Mkoa (kushoto),  katika ibada ya pasaka iliyofanyika katika kanisa Katoliki Parokia ya Namanyere

13 Aprili 2020

Uhamiaji Mkoa wa Mara yapokea Kontena kutoka Barrick North Mara

Mara, Tanzania
Katika kuendeleza jitihada za kuunga mkono serikali katika ulinzi na usalama hapa nchini Mgodi wa Barrick North Mara Mkoani Mara umetoa kontena moja (tupu) kwa Idara ya Uhamiaji   wilayani Butiama Mkoani Mara litakalotumika kama Ofisi ndogo katika Kizuizi cha Kirumi ikiwa na lengo la kurahisisha utendaji kazi katika kizuizi hicho.

Akiongea wakati akipokea kontena hilo Afisa uhamiaji Mkoa wa Mara Naibu Kamishna wa Uhamiaji DCI Albert Rwelamila aliwapongeza wakurugenzi wa Barrick North Mara kwa kutoa kontena hilo kwani litasaidia  katika utendaji kazi wa kawaida na kufanya doria za ulinzi imara katika Mipaka ya nchi ili kuendelea kudumisha hali ya amani na usalama wa wananchi na mali zao .

Awali Kizuizi hicho hakikuwa na ofisi au sehemu ya Kutosha  kujikinga na jua au mvua kwa askari wakati wa utekelezaji wa majukmu yao, hivyo kontena hilo limefika wakati muafaka hasa katika kipindi hiki cha kupambana na wahamiaji haramu wanaojaribu kujipenyeza kuingia nchini bila kufuata utaratibu kutokana na ugonjwa wa COVID -19 Unaosababishwa na virusi vya Corona.

Aidha DCI Rwelamila akiwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Tarime na Rorya ACP William Mkondya waliweza kuongea na askari waliopo katika kizuizi hicho cha Kirumi kwenye barabara ya Sirari-Musoma- Mwanza, walipofanya ziara ya kukagua utendaji kazi katika vituo mbalimbali vya mipaka na vizuizi Mkoani Mara.

Katika ziara hiyo  walitoa  wito na maelekezo kwa Maafisa na askari wa vituo hivyo juu ya  kushirikiana kwa vyombo vyote vya ulinzi na usalama katika udhibiti wa uingiaji wa wageni nchini kinyume na sheria hasa wakati huu wa juhudi za kupambana na kudhibiti kuenea kwa maambuki ya virusi vya Corona.


HABARI PICHA NA MATUKIO
DCI Albert Rwelamila Afisa Uhamiaji Mkoa Mara (aliyevaa Barakoa Kulia) akikagua utendaji kazi wa madaktari wanaopima abiria katika kizuizi cha Kirumi  juu ya maambukizi ya covid 19 Kabla ya Kukutana na Huduma za Kiuhamiaji

 DCI Albert Rwelamila Afisa Uhamiaji Mkoa Mara akiwa na Kamanda Kanda Maalumu ACP William Mkondya wakiongea na askari katika kizuizi cha Kirumi kwenye barabara ya Sirari-Musoma- Mwanza 


Picha ya Pamoja DCI Rwelamila, (Katikati waliosimama) kushoto kwake ni ACI Othuman Makame, Mrakibu Msaidizi Adam Tebuye akifuatiwa na Mhasibu David Sanga, Kulia kwa DCI Rwelamila  ni Maafisa Uhamiaji na Waliochuchumaa ni Wadau walioleta kontena kutoka - Barrick North Mara

Afisa Uhamiaji Mkoa aliyevaa T-shirt nyeupe akitoa maelekezo kwa Maafisa wa Uhamiaji juu ya matumizi ya kontena lililopokelewa katika kizuizi cha Kirumi (Picha zote na Ofisi ya Uhusiano Uhamiaji Mkoa wa Mara). 

11 Aprili 2020

PASAKA NJEMA


#COVID-19TZ: UHAMIAJI KAGERA YATEKELEZA AGIZO LA KAMISHNA JENERALI DKT. MAKAKALA KUTHIBITI UINGIAJI HOLELA WA WATU NCHINI.

Idara ya Uhamiaji Mkoani Kagera imeanzisha progamu za Elimu kwa Umma na Ukaguzi (Doria na Misako) kwa lengo la kuimarisha udhibiti wa uingiaji wa watu nchini.

Akizungumzia Mikakati hiyo Afisa Uhamiaji Mkoa wa Kagera, Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji Upendo  Buteng’e amesema Idara ya Uhamiaji kwa ushirikiano na Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama Mkoani humo, wamefanya ukaguzi kwa vipenyo (Panya Road) ambavyo vinatumiwa na Watanzania na raia wa kigeni kuingia nchini kinyemela.

Kijiografia, Mkoa wa Kagera unapakana na Nchi za Burundi, Rwanda, Uganda pamoja na Uwanda Mkubwa wa Ziwa Victoria ambao unapakana na Kenya.

Kutokana na muingiliano mkubwa wa watu na uwepo wa vipenyo vingi, Uhamiaji Mkoa wa Kagera wameanzisha program maalum za Ukaguzi (Doria na Misako) na Elimu kwa Umma kwa kuwashirikisha moja kwa moja Wananchi, Madereva wa Magari ya Usafirishaji mizigo na Viongozi wa Serikali za Vijiji na Mitaa hususan maeneo ya mipakani kuacha kuwapokea Watanzania na wageni wanaoingia nchini kupitia kwenye maneo yao.

Zoezi hili limeanza tarehe 31/03/2020 ambalo litaendelea kwa muda wa siku 30 linahusisha pia ukaguzi wa vipenyo na mialo iliyopo katika Wilaya za Bukoba,  Missenyi, Kyerwa na Ngara.

Pamoja na udhibiti wa uingiaji wa watu nchini pia wananchi wametakiwa kuchukua tahadhari zote za kujikinga na ugonjwa wa Corona kwa kufuata maelekezo yanayotolewa na Serikali kupitia Wizara ya Afya ikiwa pamoja na kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni pamoja na vitakasa mikono na Barakoa wakati wote.

Aidha, Idara ya Uhamiaji inawataka Madereva wa magari makubwa ya mizigo kuacha kubeba abiria kwenye magari yao, endapo watabainika kufanya hivyo hawataruhusiwa kuendelea na safari zao na badala yake watawekwa Karantini kwa muda wa siku 14 kwa gharama zao wenyewe. Tofauti na ilivyo sasa kwamba wanaendelea na safari zao baada ya kufanyiwa vipimo na kuonekana wako salama.

Wakati huo huo Wananchi wengine wametakiwa kutofanya safari zozote ambazo siyo za lazima kwasababu Nchi jirani wamezika watu kuingia katika Nchi zao.

Hata hivyo Idara ya Uhamiaji inatoa wito kwa wananchi wasiokuwa na  safari za lazima waahirishe safari zao hadi hapo hali itakapokuwa sawia.

Ikumbukwe kuwa zoezi linafanywa ikiwa ni Utekelezaji wa Agizo la Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Makakala alilotoa hivi karibuni alipokagua kituo cha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwl. Julius Nyerere (JNIA) ambapo kwa Mkoani Kagera linafanywa kwa ushiriano na Vyombo vya Ulinzi na Usalama Mkoa pamoja na Wilaya za Bukoba, Missenyi, Kyerwa na Ngara na Wataalam kutoka Wizara ya Afya

Afisa Uhamiaji Mkoa wa Kagera, Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji Pendo  Buteng’e akitoa taarifa ya utekelezaji wa agizo la Kamishna Jenerali wa Uhamiaji katika Ofisi ya Uhamiaji Mkoa Kagera mjini Bukoba 

Kituo cha Uhamiaji Mutukula kilichopo mpakani mwa Tanzania na Uganda kinachohudumia raia na wageni wanaokwenda nchi za Uganda, Sudani Kusini na DRC

Afisa Uhamiaji Mkoa wa Kagera, Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji Pendo  Buteng’e akiwa wilayani Kyerwa katika utekelezaji wa agizo la kumarisha doria na misako mkoani Kagera. 

Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Kagera, wakiongea na wananchi walipotembelea kijiji cha mpakani cha Rubafu.

Ukaguzi wa 'njia za panya' katika kijiji cha mpakani cha Kakoni wilayani Kyerwa uliofanywa na Idara ya Uhamiaji mkoa wa Kagera kwa ushirikiano na vyombo vingine vya dola mkoani humo.


10 Aprili 2020

#CORONAVIRUS: UHAMIAJI MKOA WA ARUSHA YAIMARISHA UDHIBITI WA MIPAKA NA VIPENYO KWA WATU WANAOINGIA NCHINI.


Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Arusha imeimarisha Udhibiti wa uingiaji wa Watu Nchini ili kujilinda na Maambukizi ya ugonjwa wa  Corona.

Wakitekeleza  Maelekezo ya Serikali kupitia Waziri wa Afya kwamba watu wote wanaoingia nchini kuwekwa Karantini kwa muda wa siku 14 kwa gharama zao, Idara ya Uhamiaji Mkoani Arusha tayari imewakamata raia wa Tanzania 131 ambao wamerejea nchini wakitokea nchini Kenya kwa kupita katika vipenye visivyo rasmi (njia za panya) katika Maeneo ya Namanga, zoezi ambalo linafanywa na Idara ya Uhamiaji kwa ushirikiano na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama pamoja na Wataalam wa Wizara ya  Afya.

Akizungumzia namna Idara ya Uhamiaji ilivyojipanga Kuthibiti Mipaka, Afisa Uhamiaji Mkoa wa Arusha Naibu Kamishna wa Uhamiaji Abdallah Towo amethibitisha kukamatwa kwa raia hao wa Tanzania, pamoja na raia 3 wa Kenya ambao tayari wamerudishwa nchini kwao.

Akifafanua zaidi, Kamanda Towo ameeleza kuwa  Watanzania wote 131 wamewekwa Karantini katika ya  Shule ya Sekondari Namanga na kwenye Hotel maalum zilizotengwa kwa ajili ya shughuli hiyo.

Taarifa yake inaongeza kuwa, Idara ya Uhamiaji inazishikilia jumla ya pikipiki 2 (Moja yenye usajili wa Kenya na nyingine Tanzania) ambazo zimetumiwa na baadhi yao kuingia nchini.

Ameendelea kueleza kuwa baada ya kuwahoji washikiliwa hao ilibainika kuwa kati yao ni raia 11 tu ndio walikuwa na Hati za Dharura za Kusafiria za Tanzania. Aidha, wengine wamechana/kuzitupa hati zao wakati walipokuwa wanavuka Mpaka ili kukwepa kutambuliwa kwa urahisi na kukwepa kuwekwa karantini.

Akihitimisha taarifa yake, Kamanda Towo amesisitiza kuwa Watu hao wote wamewekwa Karantini kwa muda wa Siku 14 kwa gharama zao kama ilivyoamriwa na Mamlaka zinazosimamia Ulinzi na Usalama Mkoani Arusha.

Aidha, Idara ya Uhamiaji inatoa wito kwa Watanzania na Wageni wote wanaoingia nchini kupita kwenye Mipaka ambayo imeanishwa kisheria, kwani kutumia njia za panya ni kosa kwa Mujibu wa Sheria ya Uhamiaji Sura 54, Rejeo la Mwaka 2016.

Pia Idara inatoa wito kwa wananchi wanaoishi maeneo ya mipakani kushirikiana na serikali katika kipindi hiki kwa kutoa taarifa za watu wanaoingia nchini bila kufuata taratibu ili waweze kuchukuliwa hatua na kuwekwa karantini ili kuepuka kusambaa kwa virusi vya corona bila kujua chanzo chake.


Afisa Uhamiaji Mkoa wa Arusha Naibu Kamishna wa Uhamiaji Abdallah Towo 


Pikipiki zilizokamatwa zikihusishwa na uvushaji wa watu katika njia zisizo rasmi katika eneo la Namanga mkoani Arusha

Baadhi ya raia wa Tanzania waliokamatwa na Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Arusha wakiwa ndani ya ofisi ya Kituo cha Uhamiaji Namanga.

Baadhi ya raia wa Tanzania waliokamatwa na Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Arusha wakiwa ndani ya ofisi ya Kituo cha Uhamiaji Namanga.

09 Aprili 2020

Muendelezo wa Ziara ya Utambulisho wa Msemaji Mkuu wa Idara ya Uhamiaji katika kituo cha Azam TV

Msemaji Mkuu wa Idara ya Uhamiaji Tanzania na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano Mrakibu wa Uhamiaji, Paul John Mselle mapema wiki hii ameendelea na ziara ya utambulisho katika vyombo mbalimbali vya habari.

Ambapo wiki hii ametambulishwa rasmi katika studio za Azam TV na U FM zilizopo Tabata Jijini Dar es Salaam na kufanya mazungumzo na Uongozi wa Uhai Productions na Watangazaji wa Habari wa Azam TV na U fm Redio.

Tukio hilo liliratibiwa na aliyekuwa Msemaji Mkuu wa Idara ya Uhamiaji Mrakibu Mwandamizi, Alhaj Ally Mohamed Mtanda ambaye amehamishiwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na kuongozwa Bi. Timzo Kalugira mtangazaji wa Azam. 

HABARI PICHA NA MATUKIO
Mkurugenzi wa Habari Azam Tv Bi. Jane Shirima (katikati) akiwapokea Msemaji Mkuu wa Uhamiaji Tanzani na Aliyekuwa Msemaji wakati wa ziara ya Utambulisho katika studio za Azam Tv mapema wiki hii
 Msemaji Mkuu wa Idara ya Uhamiaji Tanzania na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano Mrakibu wa Uhamiaji, Paul John Mselle (Kulia) akifanya mazungumzo na Mtangazaji wa Azam Tv Baraka Mpenja 
Bi. Timzo Kalugira Mtangazaji wa Azam Tv wa kwanza (kushoto) akitoa maelezo juu ya utayarishaji na uandaaji wa vipindi unavyofanyika katika studio za Azam Tv


Baadhi ya Waandishi wa Habari wa Azam Tv Wakiwa katika Majukumu yao ya Kawaida


 

Ndani ya Studio za 107.3 U fm Dar es salaam

(Picha zote na Kitengo cha Uhusiano Uhamiaji Makao Makuu)

06 Aprili 2020

CGI Dkt. Anna Makakala Awakumbusha Maafisa, Askari na Watumishi wa Uhamiaji Kuchukua Tahadhari Dhidi ya Corona

Dar es Salaam, Tanzania
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Peter Makakala ameyasema hayo mapema leo hii alipofanya ziara ya kikazi  katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) ikiwa na lengo la kujionea namna watumishi wa Idara ya Uhamiaji wanavyochukua hatua za kujikinga dhidi ya maradhi ya Ugonjwa hatari wa Covid19 unaosababishwa na virusi vya Corona.

Dkt. Makakala ameupongeza uongozi wa Uwanja huo kwa kushirikiana vyema na Uhamiaji katika kuhakikisha ulinzi na usalama wa eneo hilo, lakini pia kwa namna walivyojipanga kujikinga na maambukizi ya maradhi ya ugonjwa wa Covid19 wakati wa utoaji huduma za kiuhamiaji zinazoendelea kutolewa katika uwanja huo.

Aidha ameeleza kwamba, vyombo vyote vya ulinzi na usalama viko macho katika kuhakikisha mipaka yote ya nchi inalindwa ipasavyo katika kipindi hiki ambacho watu wengine wanaweza kutumia kama faida ya kuhatarisha usalama wa Taifa.

“Wapo watu wanaweza kutumia janga hili la ugonjwa wa Covid19 kuhatarisha usalama wa nchi yetu, hivyo ni muhimu kuendelea kuwa makini katika kuilinda nchi yetu na kuendeleza ulinzi madhubuti wa mipaka yetu kwa nguvu zetu zote, Alisema.

Mbali na hilo Kamishna Jenerali Dkt. Makakala ametoa wito kwa Maafisa Uhamiaji Mikoa yote na Wafawidhi wa vituo vyote vya Uhamiaji nchini kuhakikisha wanafuata taratibu zote zinazotolewa na wataalamu wa afya katika kujikinga na maradhi hayo, na pia kuhakikisha huduma za vifaa kinga zinakuwepo muda wote katika sehemu zote za kutolea huduma za kiuhamiaji kwa faida ya sasa na baadae.  
Kwa upande wake Afisa Uhamiaji Mfawidhi wa Kituo cha Uwanja wa ndege wa Kimataifa (JNIA), Naibu Kamishna wa Uhamiaji (DCI) Fredrick Kiondo amemshukuru Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala kwa kuwapatia vifaa kinga mapema tu ugonjwa huo ulipoanza kuibuka na sasa vifaa hivyo vinasaidia sana Maafisa, Askari, na wananchi kwa ujumla wanaoenda kupata huduma za kiuhamiaji kujikinga na maambukizi yanayoweza kujitokeza.

Akitoa taarifa ya mwenendo wa uingiaji wa abiria kwa sasa katika uwanja huo, DCI Kiondo alieleza kwamba kwa sasa kiwango cha kupokea ndege kimeshuka sana, ambapo hapo awali walikuwa wana uwezo wa kupokea na kuhudumia ndege karibu 19 kwa siku lakini toka ugonjwa huu umeshika kasi idadi hiyo imeporomoka kwa kasi sana na kufikia ndege moja tu.

Ndege hiyo huweza kutua mara mbili au tatu kwa wiki na huja na abiria wachache sana wengi wao wakiwa ni watanzania wanaorudi nyumbani na wakifika tu wanapimwa na wataalamu wa afya kisha wanapata huduma za kiuhamiaji na baadae huchukuliwa na magari maalumu ya serikali kwa ajili ya kuwapeleka karantini ya siku 14 kwa ungalizi na vipimo zaidi kama maagizoya serikali yanavyoelekeza.

HABARI PICHA NA MATUKIO

Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala akinawa mikono mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa (JNIA Terminal III) Katika ziara yake ya kikazi


Kamishna wa Uhamiaji Divisheni ya Vibali vya Ukaazi na Pasi Mary Palmer (Ndc) akinawa Mikono mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa (JNIA) katika ziara ya Kamishna Jenerali wa Uhamiaji aliyoifanya mapema leo hii.


Eneo linalotumiwa na wateja  mbalimbali wanaowasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa (JNIA) kunawa mikono ikiwa ni juhudi za kujikinga na maambukizi ya Corona


 Maofisa Uhamiaji wa kituo cha JNIA Wakijiandaa kumpokea Kamishna Jenerali wa Uhamiaji  (Kushoto) ni Msemaji Mkuu wa Uhamiaji Mrakibu Paul Mselle
 Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala akipokea maelezo  ya huduma zinavyotelewa katika kiwanja hicho kutoka kwa Mfawidhi wa Kituo hicho Naibu Kamishna wa Uhamiaji (DCI) Fredrick Kiondo
Baadhi ya kaunta zinazotoa huduma za kiuhamiaji 
Mfawidhi wa Kituo cha (JNIA ) Naibu Kamishna wa Uhamiaji (DCI) Fredrick Kiondo akitoa maelezo ya awali kuhusu shughuli zanazofanyika katika kituo anachokisimamia


Muonekano wa nje wa Jengo la Abiria Terminal III Katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa JNIA (Picha zote na Kitengo cha Uhusiano Uhamiaji Makao Makuu)