Visitors

IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA UHAMIAJI HABARI BLOGU KARIBU KWENYE BLOG RASMI YA IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA TUNAKULETEA MATUKIO YANAYOTOKEA KILA SIKU KATIKA IDARA YA UHAMIAJI TAFADHALI TUNAOMBA TUFUATILIE PIA KATIKA MITANDAO YETU YA KIJAMII

07 Februari 2020

UHAMIAJI TABORA Yakamata Wahamiaji Haramu Zaidi ya 80 Katika Oparesheni Maalumu.

Tabora, Tanzania
Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Tabora imekamata wahamiaji haramu zaidi ya 80 kwa makosa mbalimbali ya Kiuhamiaji katika Oparesheni maalumu iliyoanza tarehe 20 Januari 2020.

Akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake, Afisa Uhamiaji Mkoa wa Tabora Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji (ACI) - Sadick Amiru Salim ameeleza kuwa, watuhumiwa wote wamekamatwa katika maeneo tofauti ya Wilaya za Mkoa wa Tabora kupitia Operesheni maalumu inayoendelea Mkoani humo.

Kutokana na Jiografia, Mkoa wa Tabora umekuwa ukipokea Wahamiaji haramu kutoka katika Mataifa ya Ukanda wa Maziwa Makuu ikiwemo Congo D.R, Burundi pamoja na pembe ya Afrika hususani mataifa ya Somalia na Ethiopia.

Akitoa takwimu za Operesheni hiyo Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji Sadick Amiru Salim amesema kuwa Manispaa ya Tabora imekuwa na idadi kubwa ya Wahamiaji haramu ambapo Watuhumiwa 51 walikamatwa na wengine 30 walikamatwa katika Wilaya nyingine za Mkoa  huo.

“Baada ya kuwahoji Wahamiaji hawa baadhi yao wameeleza kuwa walikuwa wanaelekea katika Mikoa mingine ikiwemo Dar es Salaam, Morogoro, Mwanza na Mbeya, ili hali wengine wamedai wanaenda nchi za  Zambia na Malawi kutafuta kazi” alisema ACI Salim

Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Tabora imewafikisha Mahakamani watuhumiwa wote wa makosa hayo ya Kiuhamiaji ili sheria ichukue mkondo wake kwa ajili ya kukomesha kabisa vitendo hivyo na hatimae kudumisha ulinzi na usalama wa Taifa.

“Operesheni hii bado inaendelea na tunawatahadharisha wageni kufuata utaratibu wa kuingia na kuishi nchini pamoja na kutii sheria bila shuruti” aliongeza ACI Salim

Aidha, ACI Salim amewapongeza wananchi na kuwasihi waendelee kutoa ushirikiano kwa Idara ya Uhamiaji pale wanapoona vitendo vya kihalifu au kukutana na watu wasiowajua na kuwatilia shaka kutoa taarifa mapema ili kuthibiti wimbi hili kubwa la wahamiaji haramu nchini, kwani jukumu la ulinzi wa mipaka ya nchi yetu ni jukumu letu sote.
HABARI PICHA NA MATUKIO
Afisa Uhamiaji Mkoa wa Tabora Kamishna Msaidizi (ACI) - Sadick Amiru Salim akitoa taarifa kwa vyombo vya Habari Kuhusiana na zoezi zima la oparesheni lilivyokwenda


Baadhi ya Watuhumiwa wa Makosa ya Kiuhamiaji waliokamatwa katika Oparesheni maalum Mkoani Tabora (Picha zote na Ofisi ya Uhusiano Uhamiaji Tabora)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni