Dar es salaam,
Tanzania
Waziri wa Mambo ya
ndani ya Nchi Mhe. George Simbachawene aliyeteuliwa hivi karibuni na Mhe Rais
Dkt. John Pombe Magufuli amefanya ziara ya Kujitambulisha katika Jeshi la
Uhamiaji Tanzania na kufanya mazungumzo na Viongozi Waandamizi wa Jeshi hilo
Katika Ofisi ndogo ya Makao Makuu ya Uhamiaji Kurasini Jijini Dar es salaam.
Akitoa Maelekezo na
Mpango Mkakati wake katika Wizara amelipongeza Jeshi la Uhamiaji kwa kufanya
kazi kwa ufanisi na weledi wa hali ya juu.
“Niwe Mkweli tu,
Kusema kweli hata viongozi wakubwa wanaridhishwa sana na utendaji kazi wenu,
Mhe. Rais anaridhishwa sana na kazi yenu mnayofanya endeleeni kufanya kazi kwa
uhodari,ufanisi na kwa weledi wa hali ya juu kwa manufaa ya sasa na kizazi kijacho” Alisema Mhe. Waziri
Simbachawene.
Mhe. Waziri aliongeza
Kwamba tofauti ya Jeshi la Uhamiaji na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ni
kwamba ninyi ni ni Jeshi lakini
linaloshughulika sana na mambo ya kidiplomasia (Diplomatic Army) mchakato mnaofanya ni wa kushughulika na
wageni wanaokuja kwa madhumuni tofauti tofauti wakiwemo wawekezaji, watalii na kuhakikisha
wanaingia na kutoka salama.
“Mnashughulika na
maeneo nyeti sana, kwenye hili kusema kweli tunafurahi kwa namna mlivyojipanga
na mnafanya kazi vizuri hongereni sana, hata katika Maelekezo yangu
ninapokutana na viongozi sioni wa kuwanyoshea vidole endeleeni kuchapa kazi”
Alisema
Aidha amesisitiza
kuendelea kudhibiti na kusimamia kwa makini Uingiaji na utokaji wa raia wa
Tanzania na wageni ikiwemo kudhibiti uingiaji wa wahamiaji haramu na kupambana
na Biashara haramu ya binadamu (Human Trafficking & Smuggling) katika
mipaka yote.
Akitoa taarifa ya
utendaji kazi ya Jeshi la Uhamiaji kwa Mhe. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Kaimu Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Gerald Kihinga alieleza kwamba moja ya
jukumu kubwa la Jeshi hilo ni kulinda usalama wa nchi na mipaka yake kwa
kudhibiti uingiaji ukaaji na utokaji nje kwa raia na wageni kwa mujibu wa
sheria, kanuni na taratibu zilizopo.
Aidha Kaimu Kamishna
Jenerali Kihinga amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa
Kuajiri askari wapya 400 waliomaliza mafunzo yao ya kujitolea katika Jeshi la
Kujenga Taifa (JKT) wakiwa na Utii, Uhodari na weledi wa hali ya juu katika
kulitumikia Taifa lao na sasa wanatekeleza majukumu yao ipasavyo ndio maana
unaona idadi kubwa ya kukamata wahamiaji haramu imeongezeka sana kwa muda
mchache yaani hakuna atakayepona kwa sasa kwani tuko imara zaidi.
Mbali na hilo
amewatahadharisha wasafirishaji wa wahamiaji haramu na wale wanaohusika na
biashara ya binadamu (Human Trafficking & Human Smuggling) kuacha mara moja
shughuli hizo kwani wakikamatwa watachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo
kutaifisha chombo kilichohusika kubeba wahamiaji haramu, nyumba iliyowahifadhi,
lakini pia kifungo cha kwenda jela miaka 20, au faini milioni 20 au vyote kwa
pamoja hivyo waache mara moja kwani watashughulikiwa ipasavyo.
Ikumbukwe kuwa ziara
hii ni ya kwanza kwa Mhe. Waziri George Simbachawene Waziri wa Mambo ya Ndani
ya Nchi toka kuteuliwa kwake hivi karibuni na Mhe. Rais Dkt. John Pombe
Magufuli ambapo amekutana na viongozi waandamizi wa Jeshi la Uhamiaji Tanzania
ikiwa ni moja ya taasisi ya vyombo vya ulinzi na usalama nchini iliyopo chini
ya wizara hiyo na Kutoa Maelekezo muhimu ya kusonga mbele.
HABARI PICHA NA MATUKIO
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. George Simbachawene (Kushoto) akisasilimiana na Kamishna wa Uhamiaji anayesimamia Divisheni ya Vibali vya Ukaazi, Visa na Pasi Mary Palmer (ndc) katika Ofisi ndogo za Makao Makuu ya Uhamiaji Kurasini Jijini Dar es salaam |
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. George Simbachawene akipokea maelezo katika chumba cha kuchukulia alama za vidole ikiwa ni sehemeu moja wapo ya hatua za kuchakatwa kwa pasipoti mpya ya Kieleketroniki.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. George Simbachawene (Kushoto) akipokea maelezo katika chumba cha kuchakata pasipoti na kuzikagua ubora unaokidhi viwango vya Kimataifa |
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. George Simbachawene akifurahia aina tofautu tofauti za pasipoti ya Kielektroniki katika Ofisi ndogo za Makao Makuu ya Uhamiaji Kurasini Jijini Dar es salaam |
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. George Simbachawene (Kulia) akipokea maelezo ya namna Divisheni yake katika Ofisi ndogo za Makao Makuu ya Uhamiaji Kurasini Jijini Dar es salaam |
Baadhi ya Viongozi waandamizi wa Jeshi la Uhamiaji wakimsikiliza kwa makini waziri Simbachawene |
Picha ya Pamoja |
Waziri wa Mambo ya Ndani Mhe. Simbachawene akizungumza na waandishi wa Habari |
(Picha zote na Kitengo cha Uhusiano Uhamiaji Makao Makuu) |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni