Dar es salaam
Kamishna Jenerali
Mpya wa Magereza (CGP) Suleiman Munyiya Mzee leo amefanya ziara ya
kujitambulisha katika Ofisi ya Uhamiaji Kurasini Jijini Dar es salaam na kupokelewa
na Mwenyeji wake Kamishna Jenerali wa Uhamiaji (CGI) Dkt. Anna Peter Makakala.
Akizungumza mara
baada ya kufika katika Ofisi hiyo Kamishna Jenerali Mzee ameiomba Idara ya
Uhamiaji kumpatia ushirikiano wa kutosha katika uongozi wake ili kusimamia
vyema maelekezo yaliyotolewa na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa Jeshi
hilo ikiwemo jukumu la kujitegemea kwa chakula cha wafungwa na kuhakikisha
Jeshi hilo linakuwa na miradi mingi ya uzalishaji mali na yenye tija.
“Kwa kweli mimi
sikutegemea kupata uteuzi huu, nilikuwa Mkuu wa Kamandi kule Pangawe (Morogoro)
lakini Mhe. Rais akaona nafaa kuja kulitumikia Taifa kupitia Jeshi la Magereza
namshukuru sana" alisema Kamishna Jenerali Mzee.
Aidha, amewashukuru wakuu wa Vyombo vya Ulinzi
na Usalama kwa ushirikiano wanaompatia
katika kutimiza adhma ya Mhe. Rais ya kutaka kuona Jeshi la Magereza linajitegemea
kwa chakula.
Kwa upande wake Kamishna
Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Peter Makakala amempongeza Kamishna Jenerali wa Magereza
Suleiman Mzee kwa kuaminiwa na Mhe. Rais kuliongoza Jeshi la Magereza na amemtakia
mafanikio mema katika majukumu yake mapya na kumuahidi ushirikiano wa kutosha
ili kufikia malengo ya uchumi wa Taifa kwa faida ya kizazi cha sasa na baadae.
Ikumbukwe kuwa Kamishna Jenerali Mpya wa Magereza Suleiman Mzee aliteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 31 Januari 2020 akichukua nafasi ya aliyekuwa Kamishna Jenerali wa Magereza Phaustine Kasike ambaye ameteuliwa kuwa Balozi.
HABARI PICHA NA MATUKIO
Kamishna Jenerali Mpya wa Magereza (CGP) Suleiman Munyiya Mzee akiwasili katika Ofisi ya Uhamiaji Kurasini Jijini Dar es salaam |
Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar Johari Masoud Sururu akisalimiana na Kamishna Jenerali Mpya wa Magereza Suleiman Munyiya Mzee alipowasili katika Ofisi ya Uhamiaji Kurasini Jijini Dar es salaam. |
Kamishna wa Uhamiaji wa Divisheni ya Vibali vya Ukaazi, Visa na Pasi Mary Palmer (ndc) akisalimiana na Kamishna Jenerali Mpya wa Magereza Suleiman Munyiya Mzee alipowasili katika Ofisi ya Uhamiaji Kurasini Jijini Dar es salaam. |
Kamishna Jenerali Mpya wa Magereza Suleiman Mzee akisaini Kitabu cha Wageni ofsini kwa Kamishna Jenerali wa Uhamiaji |
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Peter Makakala akimkabidhi Jarida la Uhamiaji Kamishna Jenerali Mpya wa Magereza Suleiman Munyiya Mzee alipowasili katika Ofisi ya Uhamiaji Kurasini Jijini Dar es salaam. |
Picha ya Pamoja |
Kamishna Jenerali Mpya wa Magereza Suleiman Munyiya Mzee (Kulia) na Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Peter Makakala wakiteta jambo wakati wa kuagana katika Ofisi ya Uhamiaji Kurasini Jijini Dar es salaam. |
(Picha zote na Kitengo cha Uhusiano Uhamiaji Makao Makuu) |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni