Visitors

IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA UHAMIAJI HABARI BLOGU KARIBU KWENYE BLOG RASMI YA IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA TUNAKULETEA MATUKIO YANAYOTOKEA KILA SIKU KATIKA IDARA YA UHAMIAJI TAFADHALI TUNAOMBA TUFUATILIE PIA KATIKA MITANDAO YETU YA KIJAMII

31 Januari 2020

Oparesheni Maalumu ya Uhamiaji Mkoa wa Mara yazaa Matunda

Mara, Tanzania
Afisa Uhamiaji Mkoa wa Mara Naibu Kamishna Albert Rwelamila
Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Mara inaendesha Oparesheni Maalum ya kudhibiti Wahamiaji haramu kwa kukagua viwanda, mashule, taasisi za dini, migodi, hoteli na nyumba za kulala wageni na kufanikiwa kukamata Jumla ya wageni 109, ambao wamekutwa na makosa mbalimbali ya kiuhamiaji kama vile kufanya kazi bila vibali, kuingia nchini kinyume cha taratibu na wengine kuzidisha muda wa ruhusa zao walizopewa kwenye vituo vya kuingia nchini (entry point).

Akizungumza  na Waandishi wa Habari Ofisini kwake Afisa Uhamiaji Mkoa wa Mara Naibu Kamishna (DCI) Albert Rwelamila alisema lengo la Operesheni hiyo ni utekelezaji wa  mkakati wa Idara ya Uhamiaji wa kudhibiti Uhamiaji usio zingatia sheria ambao ulizinduliwa mwezi septemba mwaka 2019.

Hadi kufikia  leo Uhamiaji Mkoa wa Mara imekamata wahamiaji hao haramu wakiwemo wenye utata wa uraia, ambao wanaotoka katika nchi mbalimbali  za Uganda, Kenya, Rwanda, Armenia, Urusi, Korea, Australia, Afrika Kusini, Nigeria, Uingereza Ethiopia, China, Congo, Senegal, India, na Indonesia.

Aidha Naibu Kamishna Rwelamila aliongeza kuwa wamekamata pia raia wengine wa kigeni ambao wamejiandikisha katika daftari la wapiga kura na wengine vitambulisho vya taifa, ambapo idara imefanikiwa kuzuia kwa muda nyaraka hizo kwa uchunguzi zaidi zikiwa idadi nyaraka 24.

Jumla ya Kesi saba zimefikishwa katika mahakama ya wilaya ya Musoma, kwa makosa ya kuingia na kuishi nchini  kinyume cha sheria  ya Uhamiaj ya  Sura ya 54 Rejeo la Mwaka 2016 na Kanuni zake,  ambapo  watuhumiwa watano walikutwa na hatia  na kuhukumiwa kwenda jela miaka mitatu au  kulipa faini ya Tsh 500,000/=, watatu wamelipa faini na kuondoshwa nchini, watuhumiwa wawili wanatumikia kifungo pamoja na watuhumiwa wengine wawili kesi zao bado zinendelea mahakamani.

“Operesheni hii bado inaendelea na tunawataadharisha wageni kufuata uraratibu wa kuingia na kuishi nchini pamoja na kutii sheria bila shuruti” aliongeza Naibu Kamishna Rwelamira

Sanjari na hilo Afisa Uhamiaji Mkoa wa Mara ametoa wito kwa Wageni wanapoingia nchini, wanatakiwa  kuwa na Pasipoti halisi ya kusafiria kutoka katika  nchi yake au hati yoyote ya kusafiria, apate ruhusa, kulingana na dhumuni la safari yake na pia  apite katika kituo rasmi cha  kuingilia nchini.

Ikiwa mgeni anataka kuja kufanya kazi hapa nchini anatakiwa kuomba kibali cha kazi kutoka katika Wizara ya Kazi Ajira na walemavu na baadae kuomba kibali cha ukaazi ambacho kinatolewa na Idara ya Uhamiaji.

Operesheni hiyo, maalumu ilipewa baraka na Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Peter Makakala, katika Mkoa wa Mara ikiwa na lengo la kuthibiti wahamiaji haramu ambao wanaweza kuhatarisha Usalama wa Taifa letu na inaendelea kufanyika kwa ufanisi mkubwa baada ya kuongezewa nguvu ya Askari wapya walioajiriwa hivi karibuni na kusambazwa katika Wilaya zote za Mkoa wa Mara  ambazo ni Bunda, Musoma, Tarime, Serengeti, Rorya na Butiama.

HABARI PICHA NA MATUKIO

Afisa Uhamiaji Mkoa wa Mara Naibu Kamishna Albert Rwelamila (kulia) akionesha baadhi ya Vitambulisho vya Taifa na Kadi za mpiga kura zilizokuwa zinatumika na watu wasiokuwa raia wa Tanzania kushoto kwake ni Naibu kamishna wa Uhamiaji Pima Salehe ambae ndiye Naibu Afisa Uhamiaji Mkoa wa Mara
Afisa Uhamiaji Mkoa wa Mara Naibu Kamishna Albert Rwelamila (kulia) akionesha baadhi ya Vyeti vya kuzaliwa vilivyopatikana kinyume na sheria.

(Picha zote na Ofisi ya Uhusiano Uhamiaji Mkoa wa Mara)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni