Kamishna Jenerali wa
Uhamiaji Dkt. Anna Peter Makakala amepata fursa ya kukutana na viongozi
waandamizi wastaafu waliowahi kuiongoza Idara ya Uhamiaji katika kikao cha
pamoja kilichofanyika leo tarehe 15 Disemba 2017 katika Ukumbi wa Mikutano wa
TEC, Kurasini jijini Dar es Salaam.
Kikao kazi hicho kilikuwa
na lengo la kupokea ushauri, kubadilishana mawazo na kupeana uzoefu baina ya
viongozi wa sasa na viongozi waandamizi wastaafu wa Idara ya Uhamiaji.
Akifungua kikao hicho, Dkt
Makakala alielezea furaha yake kwa kupata fursa ya kipekee kwa kukutana
na wazee ambao ni waanzilishi wa Idara ya Uhamiaji, na kuwaomba waweze kutoa
ushauri wao na kubadilishana uzoefu na viongozi wa sasa wa Idara, juu ya
masuala mbalimbali kwa nia ya kuongeza ufanisi na kutatua changamoto ambazo
Idara imekuwa ikikabiliana nazo.
"Nina furaha kubwa
sana yaani leo, sijui nieleze vipi. Leo nipo na Wakuu wangu walionilea idarani
hadi na mimi nimekuwa Mkuu wa Idara. Ni jambo kubwa sana mmenifanyia kwa
kukubali kuja hapa ili mnifunde mimi na wenzangu. Nawashukuru sana." alisema Kamishna
Jenerali wa Uhamiaji wakati akiwakaribisha wastaafu hao.
Akizungumza kwa niaba ya
viongozi wastaaafu, Mkurugenzi mstaafu wa Uhamiaji, Kinemo Kihomano alimpongeza
Dkt Makakala kwa kuteuliwa kuwa Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, na kumtaka
kuendeleza yale mazuri yaliyoanzishwa na viongozi wastaafu na kuendeleza
ubunifu na utekelezaji wa mipango mbalimbali aliyokwishaanza kuitekeleza
kulingana na mahitaji ya wakati wa sasa.
Kwa upande wake Kamishna
Ally Mnyika, mbali ya kumpongeza Dkt Makakala, alimshauri kufanya kazi bila
woga wala upendeleo wa aina yoyote, kutekeleza na kusimamia maamuzi mbalimbali
atakayokuwa akiyafanya ili mradi amezingatia Sheria, Kanuni na Taratibu
zilizopo.
Katika kikao hicho, viongozi
mbalimbali wastaafu walipata fursa ya kutoa uzoefu wao juu ya masuala
mbalimbali ya kiuhamiaji na namna walivyoweza kukabiliana na changamoto
mbalimbali walizokutana nazo wakati wa uongozi wao kwa nia ya kuboresha
utendaji wa Idara ya Uhamiaji.
Ikumbukwe kwamba Idara ya
Uhamiaji imepitia mabadiliko kadhaa ya vyeo vya uongozi ambapo hapo awali Mkuu
wa idara alikuwa akijulikana kama Mkurugenzi wa Uhamiaji, baadae Kamishna Mkuu
wa Uhamiaji na sasa Kamishna Jenerali wa Uhamiaji.
Aidha katika Kikao hicho
walihudhuria Wakurugenzi Wastaafu wa Uhamiaji Ally A. Mnyika, Judith Vicky
Mtawali, Kinemo W. D. Kihomano na Magnus P. J Ulungi. Wengine ni Masauni Yusuf
Masauni, Makame Usi Ali, na Ali Khamis Ali kwa upande wa Zanzibar. Kadhalika
Makamishna Piniel O. Mgonja, Donald S. B. Ndagula, John Choma, Francis Kibula,
Cuthbert Samba, Faustina B. Rutaihwa, Barikiel Shayo, George J. Kashwende
pamaoja na Makamishna waliopo Madarakani kwa sasa na Viongozi Waandamizi wa Idara ya Uhamiaji kutoka
Makao Makuu, Zanzibar pamoja na baadhi ya Mikoa walihudhuria.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni