Visitors

IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA UHAMIAJI HABARI BLOGU KARIBU KWENYE BLOG RASMI YA IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA TUNAKULETEA MATUKIO YANAYOTOKEA KILA SIKU KATIKA IDARA YA UHAMIAJI TAFADHALI TUNAOMBA TUFUATILIE PIA KATIKA MITANDAO YETU YA KIJAMII

14 Desemba 2017

MHESHIMIWA RAIS NA AMIRI JESHI MKUU AKABIDHI NYUMBA 63 ZA UHAMIAJI KATIKA ENEO LA IYUMBU, DODOMA.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amemkabidhi Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna P. Makakala nyumba mpya 63 zenye thamani ya zaidi ya Sh. Bilioni 3 zilizonunuliwa toka Shirika la Nyumba la Taifa, NHC jana eneo la Iyumbu, Manispaa ya Dodoma.

Nyumba hizi 63 zilizokamilika ni za  Awamu ya Kwanza ya Mradi mkubwa unaogharamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ujenzi wake kutekelezwa na Shirika la Wazalendo la NHC, ambapo matarajio ya Mradi ni kujenga nyumba 150 ambazo zitagawiwa kwa Taasisi mbalimbali za Serikali zilizoko Makao Makuu ya Serikali, Mjini Dodoma.  

Aidha, nyumba 63 alizozipokea Kamishna Jenerali ni sehemu ya nyumba 103 ambazo Idara ya Uhamiaji imetengewa toka Mradi huo ambapo ujenzi wa nyumba 47 zilizobaki utafanywa kipindi cha Awamu ya pili ya Mradi unaotegemewa kukamilika ifikapo Mwezi Mei 2018.

"Kwa kweli Uhamiaji mnafanya kazi kubwa sana, sio kama zamani. Naona kila mara mmekamata wahamiaji haramu. Hata sasa nina taarifa kuwa maafisa uhamiaji pale Airport wamesaidia kukamata dola milioni moja zilizokuwa zinaingizwa nchini kinyume cha sheria. Hongera sana mama, pia naomba ufikishe salamu zangu kwa Maafisa Uhamiaji wote, nafurahi sana kwenye utendaji kazi wenu.  Ndio maana nimewapa hizi nyumba ili mfanye kazi kwa bidiii."  alisema Mheshimiwa Rais.

Akipokea nyumba hizo Kamishna Jenerali wa Uhamiaji amemshukuru Amiri Jeshi Mkuu na kuahidi kuwa Idara inakusudia kuhamia Dodoma haraka iwezekanavyo na kwamba  nyumba hizo zitasaidia kutatua tatizo la Makazi ya Maafisa na Askari watakaohamia Makao Makuu Dodoma.

“Idadi ya Maafisa, Askari na Watumishi raia wa Uhamiaji wanaotarajiwa kuhamia Makao Makuu ya Serikali mjini Dodoma ni 300, hivyo upatikanaji wa nyumba hizi utasaidia kuwapatia makazi bora watumishi hao watakaohamia Dodoma pamoja na kupunguza changamoto ya nyumba ya makazi” alisema Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna P. Makakala.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba alimshukuru na kumpongeza Rais Magufuli kwa hatua anazochukua katika kutatua changamoto mbalimbali serikalini ambapo ameongeza ari kwa watumishi na tija katika uwajibikaji hususani kwa Idara ya Uhamiaji.

“Uzinduzi wa nyumba za makazi katika eneo hili la Iyumbu ni hatua muhimu na inayostahili pongezi kwani ni sehemu ya uboreshaji wa makazi kwa watumishi. Ni Imani yangu kuwa, nyumba hizi zitatatua changamoto ya makazi kwa maafisa na askari wa Jeshi la Uhamiaji. Pia zitasaidia kuongeza ari mpya kwani makazi haya yatawezesha kufanya kazi kwa ufanisi na hivyo kutekeleza kauli mbiu ya HAPA KAZI TU.”  Aliongeza Waziri Mwigulu.

Kadhalika, hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Mej. Jenerali Projest Rwegasira, Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Nyumba la Taifa Bi. Blandina Salome Joseph Nyoni, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Nyumba la Taifa Ndugu Nehemiah Mchechu, Viongozi mbalimbali wa Taasisi za Serikali, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama na Viongozi kutoka Sekta Binafsi.
Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli akisalimiana na Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala kabla ya tukio la kukabidhi nyumba 63 kwa Idara ya Uhamiaji eneo la Iyumbu Manispaa ya Dodoma siku ya tarehe 13 Disemba 2017.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai  na Kamishna Jenerali wa Uhamiaji  wakiwa kwenye tukio la kukabidhi nyumba 63 za Uhamiaji eneo la Iyumbu-Dodoma.
Kamishna wa Uhamiaji-Utawala na Fedha akifuatilia kwa makini tukio la kukabidhi nyumba 63 kwa Idara ya Uhamiaji

Afisa Uhamiaji Mkoa wa Dodoma DCI. Peter Kundy akisalimiana na Mkurugenzi wa NHC Bw. Nehemiah Mchechu kabla ya tukio la Rais kukabidhi nyumba 63 za Uhamiaji.
Maafisa Uhamiaji wakifuatilia tukio la kukabidhiwa nyumba 63 kwa Idara ya Uhamiaji 
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Afisa wa NHC na Afisa Uhamiaji Mkoa wa Dodoma wakielekea eneo la tukio

Kamishna wa Uhamiaji-Utawala na Fedha (kulia) Edward Chogero akifuatilia tukio la makabidhiano ya nyumba 63 Iyumbu Dodoma, kulia kwake ni Afisa Uhamiaji Mkoa wa Dodoma DCI. Peter Kundy.
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji akisalimiana na Mkurugenzi Mkuu wa NHC kabla ya shughuli ya Rais kukabidhi nyumba 63 za Uhamiaji eneo la Iyumbu Manispaa ya Dodoma.
Maafisa Uhamiaji wakifurahia jambo wakati wa hotuba ya Mheshimiwa Rais katika eneo la Iyumbu Manispaa ya Dodoma
Kamishna wa Uhamiaji-Utawala na Fedha Peter Chogero akiongea na Afisa kutoka NHC kabla ya tukio la kukabidhiwa nyumba 63 kwa Idara ya Uhamiaji eneo la Iyumbu-Dodoma

Baadhi ya nyumba mpya zilizokabidhiwa kwa Idara ya Uhamiaji eneo la Iyumbu Manispaa ya Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Joseph Pombe Magufuli akifuatilia shughuli za burdani kwenye viwanja vya tukio la kukabidhi nyumba 63 za Idara ya Uhamiaji, kulia ni Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna P. Makakala, Iyumbu , Dodoma.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Joseph Pombe Magufuli akisoma ujumbe ulio kwenye Jiwe la la ufunguzi wa Nyumba mpya zilizokabidhiwa kwa Idara ya Uhamiaji, huku akizungukwa na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Waziri Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi, Iyumbu, Dodoma.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Joseph Pombe Magufuli akikata utepe kuashiria ufunguzi wa Nyumba eneo la Iyumbu,Dodoma.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni