Visitors

IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA UHAMIAJI HABARI BLOGU KARIBU KWENYE BLOG RASMI YA IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA TUNAKULETEA MATUKIO YANAYOTOKEA KILA SIKU KATIKA IDARA YA UHAMIAJI TAFADHALI TUNAOMBA TUFUATILIE PIA KATIKA MITANDAO YETU YA KIJAMII

21 Februari 2018

Watuhumiwa wa Uhamiaji Haramu 48 wakamatwa Kampala International University (KIU) Tawi la Dar Es Salaam.

Idara ya Uhamiaji kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu ilifanya ukaguzi wa kushtukiza katika chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala na kufanikiwa kuwakamata Watuhumiwa 48, siku ya Jumanne ya tarehe 20 Februari 2018.


Watuhumiwa hao ni Wahadhiri, Wanafunzi na Wafanyakazi wa kada mbalimbali. Pia katika tukio hilo wamekamatwa Watanzania (9) kwa kosa la kuwahifadhi na kutokutoa ushirikiano kwa Maafisa Uhamiaji kinyume na sheria ya Uhamiaji.

Msemaji Mkuu wa Idara Uhamiaji Mrakibu wa Uhamiaji Ally Mtanda alifafanua kuwa Watuhumiwa waliokamatwa kwa mchanganuo wa uraia wao ni kama ifuatavyo, Uganda (30), Nigeria (5), Kenya (3) na Congo D.R (1).

Tukio hili ni muendelezo wa doria na misako inayofanywa na Idara kwa lengo la kuwasaka na kuwakamata Wahamiaji haramu ambapo awali walikamatwa Watuhumiwa wengine raia wa Nigeria (5) kwa kosa la kuishi nchini bila Vibali vya Ukaazi na kujishughulisha na biashara haramu ya madawa ya kulevya na raia watatu (3) wa Tanzania kwa kushirikiana na Wanaijeria hao.

Baada ya kuhojiwa ilibainika kuwa mmoja wa watuhumiwa raia wa Nigeria ni mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala tawi la Dar Es Salaam kilichopo Gongolamboto.

Watuhumiwa wote wanaendelea kuhojiwa na mara baada ya kukamilika kwa taratibu zote watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.


Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Peter Makakala akiongea na waandishi wa Habari mara baada ya timu yake kuwakamata wahamiaji haramu zaidi ya 40 katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala.

Kaimu Kamishna wa Udhibiti na Usimamizi wa Mipaka  Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji Hosea Kagimbo akiwa na Mheshimiwa Waziri wa Elimu Prof. Ndaliachako wakikagua vibali vya watumishi raia wa kigeni katika Chuo cha Kimataifa cha Kampala kilichopo Gongolamboto jijini Dar es salaam siku ya Jumanne tarehe 20 Februari 2018.

Kamishna Jenerali wa Uhamiaji pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Elimu wakijibu maswali ya Waandishi wa Habari katika chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala.
Baadhi ya Watuhumiwa wakiwa ndani ndani ya  Basi la Idara ya Uhamiaji tayari kwa kupelekwa kwenye ofisi za Uhamiaji kwa mahojiano zaidi.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni