Idara
ya Uhamiaji imeshiriki zoezi la kufanya usafi katika shule ya msingi Matumaini iliyoko Kurasini jijini Dar
es salaam. Shule hiyo inayomilikiwa na Jeshi la Wokovu inasomesha wanafunzi
wenye mahitaji maalum toka Mikoa mbalimbali nchini na hata nje ya nchi.
Akiongea
kwa niaba ya Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Kamishna wa Utawala na Fedha,
Edward Peter Chogero ambaye ndiye aliyeongoza Maafisa, Askari na Watumishi wa
kada nyingine wa Idara hiyo, alisema zoezi hilo ni mwendelezo wa utekelezaji wa
agizo la Serikali la kufanya usafi katika kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi.
Aidha, Idara ya Uhamiaji ilitoa zawadi mbalimbali kwa wanafunzi wa shule hiyo
walio na mahitaji maalum ikiwa ni sehemu ya kuwafariji na kuwaonesha upendo ili
wajisikie ni sawa na watu wengine katika jamii.
Akiongea
kwa niaba ya Uongozi, Luteni Thomas Sinana ambaye ni Mkurugenzi wa Shule hiyo
aliishukuru na kuipongeza Idara ya Uhamiaji kwa moyo wa upendo waliouonesha kwa
wanafunzi hao wenye mahitaji maalum, kwa kushiriki kwao katika kufanya usafi
katika maeneo mbalimbali ya shule hiyo pamoja na kutoa zawadi mbali mbali kwa
watoto hao.
Luteni
Sinana alisema “kituo kina mahitaji mengi japo kuwa tunashirikiana na Serikali
kutoa elimu kwa vijana hawa kuanzia darasa la kwanza mpaka la saba ila watoto
wote waliopo hapa wana mahitaji maalumu kutokana na ulemavu wao hivyo tunapopata
vifaa kama hivi vinatusaidia sana kwenye kituo chetu” .
Mwisho
watoto hao walipata nafasi ya kuonyesha vipaji vyao mbalimbali ikiwa ni pamoja
na kazi za mikono wanazotengeza wenyewe, kuimba, kucheza na kuigiza.
|
Kamishna wa Uhamiaji (Utawala na Fedha) Edward Chogero akikabidhi zawadi kwa Kiranja Mkuu wa Shule ya Matumaini Ernest Thomas mara baada ya zoezi la kufanya usafi kumalizika shuleni hapo. |
|
Maafisa Uhamiaji wakifanya usafi katika Shule ya Msingi Matumaini leo Jumamosi Februari 24, 2018 |
|
Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Matumaini wakifuatilia tukio la kukabidhiwa zawadi |
|
Kamishna wa Uhamiaji (Utawala na Fedha) akiwa na Mkurugenzi wa Shule ya Matumaini Luteni Thomas Sinana |
|
Kikundi cha Sanaa cha Shule ya Msingi Matumaini kikitumbuiza wakati wa zoezi la utoaji zawadi shuleni hapo |
|
Wanafunzi wa Shule ya Msingi Matumaini wakitoa burudani kwa Maafisa Uhamiaji waliofika shuleni hapo kwa ajili ya kushiriki usafi na kutoa zawadi |
|
Wanafunzi wakisoma vipeperushi vyenye kuelezea maana ya Uhamiaji Mtandao |
|
Kamishna Edward Chogero akiangalia vitu mbalimbali vinavyotengezwa na wanafunzi wa shule ya msingi Matumaini |
|
Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Matumaini ambaye pia ndiye kaka Mkuu wa shule hiyo akitoa shukrani kwa niaba ya wanafunzi wenzake mara baada ya kukabidhiwa zawadi hizo. |
|
Maafisa Uhamiaji wakiwasalimia wanafunzi wa Shule ya Matumaini |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni