Kamishna
Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Peter Makakala leo tarehe 22 Februari, 2019
amefanya ziara ya kuwatembela Wachezaji wa Timu za Mpira wa Miguu na Kikapu
walioweka kambi katika Chuo cha Magereza Ukonga jijini Dar es salaam.
Lengo la ziara
hiyo ni kupata taarifa ya maandalizi, kukagua timu hizo na kuwatia hamasa katika
kuelekea katika Mashindano ya Majeshi yatakayoanza kutimua vumbi kesho Jumamosi
Februari 23. Michezo hiyo ya Majeshi hufanyika kila mwaka na huandaliwa na
Baraza la Michezo ya Majeshi Tanzania (BAMMATA).
Akitoa
taarifa ya Maandalizi na hali za wachezaji, Mwenyekiti wa BAMMATA Kanda ya
Uhamiaji Naibu Kamishna wa Uhamiaji Nasra Jumaa alimweleza Kamishna Jenerali
kuwa wachezaji wote wako katika hali nzuri na wana ari ya kushindana.
“Afande Kamishna Jenerali
tunashukuru kwa ujio wako hapa na napenda kukujulisha kuwa wachezaji wako
katika hali nzuri, wana ari kubwa na wako tayari kuiletea ushindi na heshima
idara yetu ya uhamiaji. Tunakuahidi ushindi tu” Alisema Naibu Kamishna Nasra.
Naye
Mwalimu wa Timu ya Mpira wa Miguu ya Uhamiaji maarufu kama Kimbunga FC, Kamishna Msaidizi
wa Uhamiaji Wahid Mmanga akitoa taarifa kuhusu timu yake alisema kwamba wako
tayari kupambana na kuleta ushindi dhidi ya timu nyingine za Majeshi kwani
safari hii hawatokubali kuwa wasindikizaji.
“Afande
sie tumekuja kucheza ili tushinde, miaka iliyopita timu kutoka majeshi mengine
walikuwa wakitumia wachezaji wa Timu zao ambazo ziko Ligi Kuu lakini kwa
utaratibu mpya mwaka huu hakuna kutumia wachezaji wa timu za majeshi zilizo
Ligi Kuu ya soka Tanzania hivyo tuna uhakika wa kuchukua kikombe” Alieleza Naibu Kamishna Mmanga.
Kamishna
Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Makakala alieleza kuridhishwa na maandalizi ya timu
na kuwatakia wachezaji kila la kheri kwenye Mashindano hayo. “Nimefurahishwa
na maandalizi, mnaonekana kweli mna ari na hamasa ya ushindi. Naomba mkacheze
ili kuiletea heshima idara yetu, mimi na watumishi wote wa Uhamiaji tuko pamoja
nanyi na tutawashangilia kila mnapocheza. Hii michezo inasaidia sisi kama jeshi
la uhamiaji kujenga mahusiano mazuri na majeshi mengine ya nchi yetu, pia ni
faida kwenu wachezaji kwani inawajengea afya bora kwa mazoezi mnayofanya.
Niwatakie kila la kheri” .
Michezo ya
Majeshi kwa mwaka huu itashirikisha timu za wachezaji wa Mpira wa Miguu,
Kikapu, Kuvuta Kamba, Kulenga shabaha na Riadha. Michezo hiyo itafunguliwa
rasmi kesho Jumamosi saa nne asubuhi katika Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es
salaam.
Wachezaji wa Timu ya Mpira wa Miguu ya Uhamiaji 'Kimbunga FC' wakipasha mwili katika Uwanja wa Chuo cha Magereza Ukonga jijini Dar es salaam walipoweka kambi yao tayari kuanza michezo ya Majeshi. |
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dokta Anna Makakala akiingia Uwanja wa Chuo cha Magereza Ukonga kukagua timu ya wanamichezo wa Uhamiaji watakaoshiriki Mashindano ya Majeshi |
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji akisikiliza ripoti ya Kambi ya wachezaji wa Timu za Mpira wa Miguu na Kikapu kutoka kwa Naibu Kamishna wa Uhamiaji Nasra Jumaa |
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji akiongea na Wachezaji wa timu ya Uhamiaji |
Mwalimu wa Tmu ya Kimbunga FC Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji Wahid Mmanga akitoa taarifa ya timu yake kwa Kamishna Jenerali |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni