Kamishna Jenerali wa
Uhamiaji, Dkt. Anna Peter Makakala amefanya ziara ya kikazi katika Mkoa wa
Pwani kwa lengo la kutambua vipenyo vinavyotumiwa na wahamiaji haramu kuingia
hapa nchini. Akiwa katika Mkoa wa Pwani, amefanya mazungumzo na Mwenyekiti wa
Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Pwani, Mhe. Mhandisi, Evarist Ndikilo
ambaye alimueleza kwamba wamejipanga katika kupambana na wahamiaji haramu katika
Mkoa huo.
"Kuna mtandao mkubwa nchi nzima
ambao unajihusisha na biashara haramu ya usafirishaji na magendo ya binadamu,
hivyo basi hatuna budi kuvishirikisha vyombo vyetu vyote vya ulinzi na usalama
katika kuhakikisha kuwa wale wote wanaojihusisha na vitendo hivi viovu
wanasakwa na kushughulikiwa kwa mujibu wa sharia,” alisema Mhe. Ndikilo.
Aidha, katika taarifa
yake, Mhe. Ndikilo alieleza kuwa Mkoa wa Pwani una urefu wa zaidi ya Kilometa
1300 katika mwambao wa bahari na una bandari bubu 39 zinazotumika na wahamiaji
haramu kuingia nchini.
Pia Kamishna Jenerali
wa Uhamiaji, ametembelea Wilaya ya Bagamoyo na kukutana na Kamati ya Ulinzi na
Usalama ya Wilaya ambapo, Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Zainabu Kawawa alimueleza kuwa Wilaya hiyo ina jumla ya
Vipenyo 19, pamoja na pori kubwa la Ruvu ambalo hutumiwa na wahamiaji haramu
kuingia nchini.
Mhe. Mkuu wa Wilaya alivitaja
baadhi ya vipenyo vinavyotumiwa na wahamiaji haramu kuingia nchini kuwa ni
pamoja na Kaole, Mbegani, Mlingotini, Changwahela, Gwaza na Kondo. Hata hivyo,
alimueleza kuwa, Kamati ya Ulinzi na Usalama imejipanga kufanya doria na misako
maalum (special operations) za mara
kwa mara ili kukabiliana na uhalifu katika katika maeneo hayo.
Aidha, Kamishna Jenerali
wa Uhamiaji aliishukuru Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya Bagamoyo kwa
ushirikiano wanaouonesha kwa Idara ya Uhamiaji katika kupambana na kudhibiti wahamiaji
haramu nchini.
Akizungumza na Wananchi katika Kijiji cha Ruvu Darajani, Kata ya Bigwaza,
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji amewataka wananchi kutoa taarifa za uwepo wa
wahamiaji haramu kwenye maeneo yao na kuacha tabia ya kuwahifadhi wahamiaji hao;
kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria na huhatarisha amani na usalama wa nchi
yetu. Pia amewataka wnanchi kuwa makini na wahamiaji haramu kwani baadhi yao wanatoka
kwenye nchi zenye machafuko hivyo, inawezekana wakawa wamekimbia na silaha.
“Napenda kutoa wito
kwa Madereva wa vyombo vya moto kama vile magari binafsi, mabasi ya abiria, malori
pamoja na bodaboda waache kuwasafirisha wahamiaji haramu, vitendo hivyo ni kosa
kwa Mujibu wa Sheria ya Uhamiaji Sura ya 54, Rejeo la Mwaka 2016 pamoja na Kanuni
zake. Ukithibitika kutenda makosa hayo adhabu yake ni Kifungo cha Miaka ishirini
(20) au kulipa faini isiyozidi Shilingi Milioni ishirini (20) au vyote kwa
pamoja,” alisisitiza Kamishna Jenerali
wa Uhamiaji.
Pia Kamishna Jenerali
wa Uhamiaji, aliwataka Watumishi wa Idara ya Uhamiaji pamoja na Maafisa na
askari wanaoshiriki katika misako na doria za wahamiaji haramu kufanya kazi kwa
weledi na bidii na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Peter Makakala akiwa na Mwenyeji wake Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mhe. Zainabu Kawawa wakati alipomtembelea Ofisini kwake Bagamoyo |
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Peter Makakala akizungumza na Wazee wenyeji katika moja ya maeneo yanayopitisha Wahamiaji haramu |
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Peter Makakala akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Ruvu Darajani, Kata ya Bigwaza, Wilayani Bagamoyo.
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni