Idara ya Uhamiaji Tanzania kwa kushirikiana na Shirika
la Uhamiaji la Kimataifa (IOM) limeanza kutoa mafunzo ya Ushirikishwaji wa Wananchi katika
Ulinzi na Usimamizi wa Mipaka katika Kijiji cha Horohoro, mpakani mwa
Tanzania na Kenya kwa siku tatu kuanzia leo tarehe 13-15 Machi, 2019.
Warsha hiyo ya Mafunzo ambayo imefunguliwa na Mkuu wa
Wilaya ya Mkinga Mhe. Yona Maki, inashirikisha wananchi waishio mpakani wenye
ushawishi katika jamii pamoja nao ni viongozi wa dini, wakulima, mgambo, viongozi
wa vijiji na waendesha bodaboda.
Awali akifungua warsha hii, Mkuu wa Wilaya ya Mkinga
aliipongeza Idara ya Uhamiaji kwa kuamua kutoa mafunzo yenye lengo la kuwashirikisha
wananchi wa kawaida katika suala zima la ulinzi na usimamizi wa mipaka.
“Kwanza niwashukuru sana Idara ya Uhamiaji pamoja na watu wa IOM kwa
kuamua kutoa mafunzo kwa wananchi wa kawaida. Ninaamini baada ya mafunzo haya,
washiriki kwa kuwa ni watu wenye ushawishi katika jamii ya vijiji vya kata hii,
watasaidia sana kufikisha ujumbe. Naona kuna viongozi wa bodaboda, hawa
bodaboda ndio wanaosafirisha watu, miongoni mwa watu hao kuna wahamiaji haramu
pia, naamini wakipewa elimu basi hawa bodaboda watakuwa ni sehemu muhimu katika
Ulinzi na Usimamizi wa mipaka yetu”.
Mkuu huyo wa Wilaya alieleza kuwa Baba wa Taifa
aliwahi kusema kuwa jukumu la ulinzi wa Taifa ni letu sote na hasa wazalendo. Hivyo
jukumu hili la ulinzi si la vyombo vya ulinzi na usalama pekee, bali ni la kila
Mtanzania.
Wakati akitoa taarifa kwa Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Afisa
Uhamiaji Wilaya Mkinga alisema kwamba jumla ya wahamiaji haramu 216 kutoka
mataifa ya Ethiopia, Somalia na Kenya walikamatwa katika wilaya ya Mkinga
katika Mwaka 2018.
Warsha hii ya siku tatu imelenga katika kuwajengea
uwezo washiriki juu ya Uhalifu wa Kimataifa, Makosa ya kiuhamiaji, Biashara ya
Magendo ya Binadamu, Usafirishaji Haramu wa Binadamu, Uraia wa Tanzania na
mambo yanayohusiana na Uhamiaji nje ya Mfumo rasmi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni