Visitors

IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA UHAMIAJI HABARI BLOGU KARIBU KWENYE BLOG RASMI YA IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA TUNAKULETEA MATUKIO YANAYOTOKEA KILA SIKU KATIKA IDARA YA UHAMIAJI TAFADHALI TUNAOMBA TUFUATILIE PIA KATIKA MITANDAO YETU YA KIJAMII

04 Machi 2021

Balozi za Heshima zafurahishwa na Utoaji wa Huduma za Uhamiaji Zanzibar

 Uhamiaji Zanzibar

Balozi za heshima Zanzibar kutoka Brazil, Ufaransa, Italy, Sweden, Spain, German, Uengereza na Canada zikiongozwa na Balozi wa heshima kutoka nchini Brazil Bw. Abdulsamad Abdulrahim wamesema kwamba wanafurahishwa na utoaji wa huduma za Ki-uhamiaji wakati wa kuingia na kutoka Zanzibar.

Hayo yamesema mapema leo katika Afisi Kuu ya Uhamiaji Zanzibar kwenye kikao kilichomshirikisha Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar pamoja na balozi hizo za heshima.

Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar Johari Masoud Sururu amezishauri Balozi za heshima zilizopo Zanzibar kuwashauri raia wao kuomba viza za kielektroniki pale wanapotaka kuingia nchini.

Aidha ameeleza kwamba Idara ya Uhamiaji imeanzisha viza za kielektroniki ambapo mgeni anaweza kuomba, kulipa na kupatiwa viza akiwa nje ya nchi jambo linalorahisisha kumhudumia mgeni kwa haraka zaidi wakati wa kuingia nchini.

“Mgeni anaeingia nchini kwa kuomba viza katika vituo vya kuingia hulazimika kufanyiwa mahojiano na Afisa Uhamiaji, kupatiwa namba ya malipo (control number) pamoja na kulazimika kufanya malipo katika kaunta za benki ya watu wa Zanzibar au CRDB zilizopo katika uwanja wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume (AAKIA)” alisema Kamishna Sururu.

Kwa upande wao balozi za heshima walisema Maafisa Uhamiaji wanatumia taaluma, uzoefu na bidii ya hali ya juu katika kutoa huduma kwa ufanisi, Balozi hizo zilielezea kufurahishwa na mfumo wa viza za kielektroniki ambapo sasa raia wao wanaomba na kupatiwa viza kwa njia ya mtandao hali inayorahisisha mgeni kuingia hapa nchini bila ya kupoteza muda.

Mabalozi hao wa heshima waliohidi kufanya kazi kwa pamoja na Idara ya Uhamiaji na waliahidi kuwatangazia raia wao kuomba viza ya kielektroniki.

Pamoja na kazi zao za kibalozi walifahamisha kuwa wanafanya jitihada za kuimarisha biashara hasa katika sekta ya utalii Zanzibar

Pia walifurahishwa na maamuzi ya Idara ya Uhamiaji katika kuongeza viza muda katika kipindi cha mlipuko wa ugonjwa wa covid 19, ambapo wageni ambao walishindwa kurejea nchini kwao kutokana na janga hilo lililoikumba dunia waliongezwa mwezi mmoja kuishi hapa nchini bila ya malipo.

Wameiomba Idara ya Uhamiaji kuangalia uwezekano wa kuanzisha utaratibu utakaowezesha wageni kupatiwa nyaraka zitakazowawezesha kurejea nchini kwao endapo watapoteza pasipoti zao wakiwa Zanzibar.

Kwa sasa mgeni anaepoteza pasipoti akiwa Zanzibar anatakiwa kwenda katika Afisi za Kibalozi za nchi zao zilizopo Dar-Es-Salaam, jambo ambalo linaonekana kuleta usumbufu hasa kwa wageni ambao safari zao zinakua siku za mwisho wa wiki au mapumziko.

HABARI PICHA NA MATUKIO

Picha ya pamoja mabalozi, Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar na Maafisa wa Uhamiaji Zanzibar
(Picha zote na Kitengo cha Uhusiano Uhamiaji Zanzibar)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni