Zanzibar
Katika shamra shamra za kuadhimisha siku ya
wanawake duniani iliyofanyika tarehe 8 Machi ya kila mwaka wanawake wa uhamiaji
kwa kushirikiana na wafanyakazi wote wa Idara ya Uhamiaji Zanzibar walitoa misaada
mbali mbali kwa watoto yatima ambao wanaishi katika mazingira magumu pamoja na
kufanya usafi wa mazingira yanayozunguka kituo hicho.
Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji Chiku Khamis Omar
alikabidhi misaada katika kituo cha watoto yatima kiitwacho Markaz Alyaqiin
Islamic Centre kilichopo Kinduni Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa niaba wanawake wa Idara ya
Uhamiaji Zanzibar.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi misaada hiyo
Kamishna Msaidizi Chiku amewashukuru viongozi wa watoto hao kwa kukubali
kupokea misaada hiyo na kuwaahidi kua wanawake wa Uhamiaji wataendelea kutoa
misaada zaidi kwa watoto hao kila hali itakaporuhusu.
Miongoni mwa misaada hiyo ni pamoja na mchele, sukari,
sabuni, vitakasa mikono na mipira ya kuchezea.
Nae kiongozi wa kituo hicho Maalim Adam Bakar Haji
ambae ni kaimu Mwenyekiti wa kituo hicho amewashukuru wanawake wa Idara ya
Uhamiaji Zanzibar kwa kuwapelekea watoto misaada hiyo na kuwaomba mashirikiano
zaidi juu ya suala la kuwalea watoto hao.
Aidha Watoto
hao yatima wakiongozwa na mtoto Abdulrahman Aly Mussa walisoma dua maalum ya
kuwaombea wanawake hao ikiwa ni shukran kwao.
Kwa upande wa Zanzibar Kauli mbiu ya mwaka huu ya siku ya wanawake duniani ni ‘’Badili fikra: imarisha ushiriki wa wanawake katika maamuzi kwa maendeleo endelevu’’.
HABARI PICHA NA MATUKIO
Vifaa mbali mbali vikitolewa na uhamiaji Zanzibar |
(Maafisa Uhamiaji Zanzibar wakishiriki kufanya usafi) |
(Picha zote na Kitengo cha Uhusiano Uhamiaji Zanzibar) |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni