Kamishna wa Uhamiaji
Zanzibar, Johari Masoud Sururu, amefanya ziara ya kikazi katika Mkoa wa Kusini
Unguja ikiwa ni utaratibu wa kawaida kutembelea vituo na ofisi za uhamiaji
Zanzibar.
Ziara hiyo iliyokuwa na
malengo makuu mawili, Kwanza ni kukagua miradi mbalimbali na viwanja vilivyopo
katika Mkoa huo. Miradi ya ujenzi wa nyumba za kuishi Watumishi na ofisi ni
hatua muhimu katika kutanua wigo wa utoaji huduma mbali mbali za Uhamiaji kwa
Wilaya zote za Unguja na Pemba ambayo ni utekelezaji wa ahadi za Serikali
kuwafikishia wananchi wake huduma katika maeneo wanayoishi.
Pili, ilikuwa ni kuhimiza askari na maafisa uhamiaji kufanya kazi kwa weledi, uaminifu na kujituma ili wananchi wapate huduma kwa wakati.
Mkaguzi Msaidizi wa
Uhamiaji Khamis Ali Juma kutoka katika ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Kusini Unguja
alimweleza Kamishna maendeleo ya miradi ya ujenzi wa nyumba za makazi ya
watumishi na ofisi katika mkoa huo pamoja na namna walivyojipanga kutoa huduma
kwa weledi.
Kamishna wa Uhamiaji
Zanzibar Johari Masoud Sururu, alieleza jinsi Idara ya Uhamiaji inavyopiga
hatua katika ujenzi wa Makazi ya Askari wake katika Wilaya zote Unguja na
Pemba.
"Nimekuja kukagua
maendeleo ya ujenzi wa nyumba za makazi ya Watumishi hapa Makunduchi, Wilaya ya
Kusini. Ujenzi unaendelea vizuri, tunategemea zikikamilika zitapunguza tatizo
la upungufu wa nyumba za makazi ya watumishi. Tunavyo viwanja katika mkoa huu,
tunategemea kununua viwanja vingine kwa ajili ya miradi hapo baadae.” Alieleza
Kamishna wa Uhamiaji huyo.
Ziara hiyo ya siku mbili
katika Mkoa wa Kusini Unguja imekuwa na mafanikio kwa kiasi kikubwa kwani kero
mbalimbali zilipatiwa majibu ya kuridhisha pamoja na miradi iliyokaguliwa
kubainika kuwa inakwenda vizuri. Kamishna Uhamiaji wa Zanzibar pamoja na
majukumu mengine amekuwa akitembelea Ofisi na Vituo vya Uhamiaji Unguja na
Pemba kuhimiza utendaji kazi unaofuta misingi na sheria.
Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar Johari Masoud Sururu akisisitiza jambo wakati wa kikao na watumishi wa Ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Kusini Unguja |
Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar Johari Sururu akisaini kitabu cha wageni katika ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Kusini wakati ya ziara yake katika mkoa huo. |
Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar akitoa maelekezo wakati wa ukaguzi wa nyumba za makazi ya watumishi zinazohitaji ukarabati. |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni