Kamishna
Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna P. Makakala jana alikabidhi Mradi wa Ujenzi wa jengo la ghorofa nane
ambalo litakuwa Makao Makuu mpya ya Uhamiaji
eneo la NCC, Kitalu na 18 na 19, jijini Dodoma kwa wakandarasi wa SUMAJKT.
Kamishna
Jenerali alisema " tunaijua sifa ya
SUMAJKT kupitia mifano mbalimbali ya
majengo bora ambayo wameyakamilisha kwa wakati, na kwa ukweli huu nina
imani kubwa nao ya kwamba jengo letu litajengwa kwa ustadi wa hali ya juu na
hivyo kuwa ni moja ya majengo ya kisasa yanayovutia hapa jijini Dodoma".
Kwa upande mwingine tukio hili lilihudhuliwa
na Afisa Mtendaji Mkuu wa SUMAJKT na Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, Meja
Jenerali Martin Busungu na Mkurugenzi Mtendaji wa SUMAJKT, Kanali Mabele ambaye
aliahidi kuwa shirika lake litajenga jengo ambalo litakuwa ni kioo cha ubora wa
kazi zao na kwamba watu hawata hitaji kwenda jijini Dar es Salaam kuona mifano
ya kazi zao bali hapa Dodoma tu.
Aidha,
tukio hili lilishuhudiwaa na Mkuu wa Timu ya washauri
waelekezi wa Mradi, Dkt. Msanifu Majenzi, Isabela Mtani kutoka Chuo Kikuu cha
Ardhi, Dar es Salaam ambaye alisema kuwa
makabidhiano ya Mradi huo wa Ujenzi kati ya Idara ya Uhamiaji ambayo ni mmiliki
na SUMAJKT ambayo ni Mkandarasi yatafuatiwa na shughuli nyingi ambazo
zimepangwa kwenda kwa haraka sana na bila kuathili ubora wa kazi yenyewe na
jengo linalojengwa.
Mradi wa
jengo hilo ambalo litakuwa kubwa kuliko lile la Kurasini, Dar es Salaam na
ambalo lilikuwa Makao Makuu ya zamani linatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi
cha miezi 18, na kuiwezesha Idara ya Uhamiaji kuanza kutumia jengo bora lenye
hadhi ya kimataifa jijini Dodoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni