Tanzania imekuwa mwenyeji wa
Mkutano wa Ngazi ya juu wa Kikanda
uliofanyika katika Hotel ya Serena, Dar es Salaam kuanzia tarehe 02-04 April mwaka
huu.
Mkutano
huo ulihudhuriwa na viongozi waandamizi kutoka nchi za Tanzania, Kenya, Ethiopia,
Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) na Wadau wa Maendeleo (Development Partners)
ambao ni Balozi za Uingereza, Marekani, Ujerumani, Norway, Ubelgiji, EU, UN-RCO,
na ICRC na kufunguliwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Kangi Alphaxad
Lugola ulilenga kutafuta njia ya namna
ya kukabiliana na ongezeko la wahamiaji haramu, wanaoingia kinyume cha sheria
hapa nchini kupitia njia ya Kusini (Southern route).
Mkutano
huo ulitanguliwa na mkutano wa Wataalamu
wa masuala ya uhamiaji kutoka nchi za Tanzania, Ethiopia na Kenya chini ya
Uenyekiti wa Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Peter Makakala.
Pamoja
na mambo mengine nchi hizo zimeweka mikakati ya pamoja katika kushughulikia changamoto
ya biashara haramu ya binadamu (Human Trafficking
& Smuggling) na usafirishaji kimagendo wa binadamu (Human Smuggling), kuangalia
namna bora ya kubadilishana taarifa za Wasafirishaji (Traffickers &
Smugglers) na mikakati ya kuwaondosha nchini wahamiaji haramu na kuhakikisha
hawarejei tena nchini bila kufuata taratibu.
“Ni
mkutano wenye nia njema kwa nchi yetu, kwani hapa tumekutana ili kuweka
mikakati namna ya kudhibiti mfumo mzima wa biashara haramu ya binadamu na usafirishaji
magendo ya binadamu kutoka pembe ya Afrika kupitia njia ya Kusini ambapo
Tanzania ni sehemu ya hiyo njia. Majadiliano yameenda vyema na tutegemee
matokeo mazuri. Kila nchi mwalikwa imeahidi kufanya juhudi katika kudhibiti
tatizo hili”
Alieleza Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala.
Tanzania
imekuwa ni njia ya Usafirishaji wa Magendo ya Binadamu kuelekea kusini mwa
Afrika ambapo Idara ya Uhamiaji nchini kwa kipindi cha mwezi Januari hadi
Disemba 2018 ilifanikiwa kuwamata na kuwachukulia hatua mbalimbali jumla ya wahamiaji
haramu 1024 kutoka pembe ya Afrika wengi
wao wakiwa raia wa Ethiopia.
Hatua
mbalimbali za kudhibiti tatizo hili zimeendelea kuchukuliwa, tayari jumla ya wahamiaji
haramu 583 kutoka Ethiopia waliomaliza adhabu ya kutumikia vifungo katika
magereza mbalimbali nchini walirejeshwa nchini kwao katika kipindi cha mwaka
jana.
Aidha
katika kipindi hicho, vyombo vya usafiri 10 vilitaifishwa na Serikali baada ya
kutiwa hatiani kwa kosa la kusafirisha wahamiaji haramu kinyume cha Sheria za Uhamiaji.
“Tunaishia
kuwakamata dereva wa Fuso anaepakia wahamiaji haramu, Tunataka madalali wenyewe
wasakwe wakamatwe, Kwahiyo Kamishna Jenerali wa Uhamiaji ndani ya mwezi mmoja
angalau basi kwa uchache uje na orodha ya hawa madalali wawili watatu hata kama
ntaambiwa kwamba wako nchi nyingine ili
tuweze kutumia sheria zilizopo kuweza kuwakamata na kuwarejesha nchini ili
kumaliza huo mtandao” Aliagiza
Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi, Mheshimiwa Kangi Lugola.
Mkutano
huu unategemea kuleta matokea chanya kwa Idara ya Uhamiaji katika suala zima la
udhibiti wa wahamiaji haramu kwani ni wa kwanza kufanyika na kuwashirikisha
wadau kutoka nchi za pembe ya Afrika ambako ndiko wahamiajii haramu wengi
wanaokamatwa nchini hutokea pamoja na Washirika wa Maendeleo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni