Kaimu
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Hanelore Manyanga amekutana
na wafanya biashara na wajasiriamali wanaofanya biashara katika mtaa wa
Loliondo, Kurasini - Jijini Dar es salaam. Mtaa huo upo Mkabala na Ofisi za
Uhamiaji Makao Makuu na kuna shughuli mbalimbali za biashara ikiwamo Mamalishe,
Mawakili, Wapiga picha (Passport size)
pamoja na watoa huduma za Stationaries.
Kamishna Manyanga amewataka
wafanya biashara hao kuisaidia Idara ya Uhamiaji kupiga vita mawakala wa huduma
za Uhamiaji (Vishoka ambao wanawatapeli wananchi wanaohitaji huduma za Uhamiaji
katika maeneo hayo.
“Kumekuwepo
na wimbi la Matapeli wanaojifanya kuwa Maafisa Uhamiaji wanawatapeli Wananchi
kwa kuchukua pesa zao na kuwaahidi kuwasaidia kupata huduma za Uhamiaji ikiwa
ni pamoja na Pasipoti, Viza, na Hati za Ukaazi kwa haraka. Kupitia kikao hiki nawaagiza
kuwa mfanye biashara kwa mujibu wa matakwa ya leseni zenu kama inatokea kuna
mtu ambaye siyo mhusika au anatumia vibanda vyenu kuwatapeli wananchi, tafadhali
toeni taarifa Uhamiaji” alisema
Kamishna Hanelore Manyanga
Aidha, Kamishna Manyanga aliongeza
kuwa Idara ya Uhamiaji imedhamiria kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya
wale wote wanaojifanya Maafisa Uhamiaji na kuwatapeli Wananchi.
Wakitoa maoni yao katika kikao hicho baadhi ya
wajasiriamali hao wametoa maoni yao na kuonesha kuchukizwa na vitendo hivyo
ambavyo vinafanywa na watu ambao siyo waadilifu na kuchafua taswira nzuri ya
Idara ya Uhamiaji na biashara zao kwa ujumla.
“Ni
jambo jema kualikwa hapa kujadili suala hili, hata sisi tumekuwa tukichukizwa
na hawa watu lakini tunashindwa kutoa taarifa kwani hatujui tumwambie nani,
unakuta mtu anakuja pale mgahawani na mtu wanasaidiana kujaza fomu za Uhamiaji na
baadae wanaondoka. Kupitia kikao hiki sasa tutakuwa tunatoa taarifa Uhamiaji
lakini tunaomba tukitoa taarifa hizo zifanyiwe kazi na pia taarifa hizo ziwe
siri” alisema Bi. Praise
Kupitia Kikao hicho wafanya
biashara hao kwa pamoja wameahidi kushirikiana na Idara ya Uhamiaji na
kuwafichua Mawakala/Vishoka wanaotumia Ofisi za mawakili, stationeries na
migahawa kufanyia shughuli za Uhamiaji ili hatua za kisheria zichukuliwe kwa
yeyote atakayejihushisha na kazi za Uhamiaji katika maeneo yao ikiwa ni pamoja
kufikishwa Mahakamani.
Kwa upande wake Kamishna wa
Uhamiaji, Uraia na Pasipoti Gerald J. Kihinga, ametoa wito kwa Wananchi kuwa
hakuna Uwakala katika huduma zinazotolewa na Idara ya Uhamiaji. Hivyo mtu
anayeomba Pasipoti ya Tanzania au Vibali vya Ukaazi anatakiwa awasilishe maombi
yake kupitia tofuti ya Idara ya Idara ya Uhamiaji ambayo ni www.immigration.go.tz
Kikao hicho kilihudhuriwa pia
na Kamishna wa Uhamiaji, Uraia na Pasipoti Gerald J.
Kihinga, Kaimu Kamishna wa Usimamizi na Udhibiti wa Mipaka, Naibu Kamishna
wa Uhamiaji, Paul Eranga pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Uratibu, Mrakibu
Mwandamizi wa Uhamiaji Peter G. Mbaku.
Bi. Praise akichangia hoja katika kikao hicho. |
Bw. Mulokozi ambaye ni mjasiriamali katika moja ya vibanda vilivyo mkabala na Ofisi ya Uhamiaji akieleza utayari wake katika kukabiliana na tatizo la vishoka wakati wa kikao hicho |
Kaimu Kamishna wa Usimaizi na Udhibiti wa Mipaka, naibu Kamishna Paul Eranga akiongea wakati wa kikao hicho |
Kaimu Kamishna wa Uhamiaji, Kamishna Hannelore Manyanga akiongea wakati wa kikao hicho |
Kamishna wa Uraia na Pasipoti, Kamishna Gerald Kihinga akiongea wakati wa kikao hicho |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni