Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi, Mhe Kangi Lugola ameitaka Idara ya Uhamiaji kuimarisha uwekezaji nchini.
Wito huo umetolewa leo Mjini Moshi wakati akifungua Mkutano wa Maafisa Uhamiaji
Waandamizi unao
lenga kujadili na kutathmini utendaji kazi wa Idara ya Uhamiaji.
Akizungumza na Maafisa hao, Waziri Lugola
amesisitiza kuwa nchi yetu inazo fursa nyingi za kiuchumi na Utalii hivyo
kuwavutia wageni na wawekezaji wengi kuiingia na kuwekeza nchini.
“Katika utendaji kazi
wake,Idara ya uhamiaji ndio kioo/taswira ya nchi yetu hivyo tufanye kazi kwa weledi na kuweka mazingira
bora ya uwekezaji na kuwahudumia wageni kwa ukarimu, lugha za staha na msiwe
kikwazo cha uwekezaji na utalii nchini”
alisema Waziri Lugola.
Aidha, Waziri Lugola
amemuagiza Kamishna Jenerali wa Uhamiaji kusimamia kikamilifu Ukusanyaji wa
Maduhuli ya Serikali na kudhibiti mianya inayopelekea upotevu wa maduhuli.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa
wa Kilimanjro, Mhe. Anna Mghwira ametoa wito kwa Idara ya Uhamiaji kushiriki
kikamilifu katika zoezi la uandikishaji na utoaji wa Vitambulisho vya Taifa
(NIDA).
“Mkoa wa Kilimanjaro una
idadi kubwa ya Wahamiaji haramu kutokana na jiografia yake pamoja na kuwepo kwa
fursa mbalimbali za uwekezaji na utalii. Ili kukabiliana na changamoto hii,
Idara iimarishe udhibiti wa mipaka ya nchi yetu ikiwa ni sambamba na kuwatambua
Watanzania na raia wa kigeni wanaoishi na kufanya kazi nchini”, aliongeza Mhe.
Mghwira.
Mhe. Mghwira ameitaka pia
Idara ya Uhamiaji kujenga mahusiano na Wananchi ili kupata taarifa za haraka na
sahihi kutoka kwa wananchi hao.
“Nitoe wito kwa Idara ya
Uhamiaji kubuni mbinu na mikakati kwa Maafisa wake kushuka chini kwa Wananchi
ili kuwa karibu zaidi na jamii na Watanzania kwa ujumla. Kwa kufanya hivyo
Wananchi watajua haki zao ikiwa pamoja na kufahamu vielelezo vinavyotakiwa
katika kupata huduma za Idara ikiwamo Pasipoti sanjali na kutoa taarifa juu ya
uwepo wa wahamiaji haramu katika maeneo yao amesisitiza Mhe. Mghwira.
Awali akimkaribisha Mhe.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi katika Mkutano huo, Kamishna Jenerali wa
Uhamiaji Dkt. Anna Peter Makakala amesema kuwa Idara imezindua mpango mkakati
wa kudhibiti Uhamiaji nchini. Mpango huo unalenga kuwatambua na kuwaorodhesha
wahamiaji wote nchini na zoezi hilo litafanyika nchi nzima kwa kuanzia Mkoa wa
Dar es Salaam.
Katika utekelezaji wake,
mpango huo utahusisha Viongozi wa Serikali za Mitaa au Vijiji (MEO/VEO),
Maafisa Watendaji wa Kata (WEO) na kuratibiwa na Idara ya Uhamiaji. Kupitia
Mpango huo Idara itaimarisha udhibiti na usimamizi wa mipaka yetu, kuimarisha
ulinzi na Usalama na pia kulipatia ufumbuzi suala la Wahamiaji Walowezi.