Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Bw. Christopher Kadio na Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Nchini Dkt. Anna Makakala wameongoza mamia ya waombolezaji katika safari ya kumzika marehemu Mzee Augustino Raphael Kubaga ambaye aliwahi kuwa Afisa Uhamiaji Mkuu ambapo alikitumikia cheo hicho toka mwaka 1969 hadi mwaka 1983 alipostaafu.
Wengine waliohudhuria ni Wakuu wa Uhamiaji wastaafu, Makamishna wastaafu, Makamishna wa Uhamiaji, Maofisa waandamizi wa Uhamiaji Tanzania bara na Zanzibar sanjari na Maofisa Askari na watumishi.
“Sisi kama familiya ya Uhamiaji tutamkumbuka sana kwa mchango wake, ambapo leo hii tunaitwa Jeshi, haikuwa jambo rahisi kwani kipindi chote alikuwa anaitetea Uhamiaji na kutuachia misingi imara hasa baada ya Uhamiaji kuondolewa katika Jeshi la Polisi ambapo Sheria, Kanuni na Taratibu mbalimbali zilibadilishwa ili Uhamiaji iweze kutekeleza majukumu yake kwa kujitegemea” alisema Dkt. Makakala.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Uhamiaji (Mstaafu) Kinemo WD. Kihomano kwa niaba ya wakuu wa Uhamiaji Wastaafu alisema marehemu Mzee Kubaga alijenga umoja na ushirikiano baina ya Tanzania bara na Zanzibar, alikuwa na dira ya Uhamiaji kuwa Jeshi na leo hii Uhamiaji imekuwa Jeshi na anaagwa kijeshi.
Mstaafu Kihomano aliongeza kwamba, Mzee Kubaga alikuwa na hekima na busara na anaejali Askari wa vyeo vyote.
Aidha, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kibali cha Uhamiaji kuwa Jeshi rasmi kwani toka uongozi wa marehemu Mzee Kubaga na viongozi wengine wote waliopita walikuwa wakifanya juhudi mbalimbali za kuifanikisha Idara ya Uhamiaji kuwa Jeshi kamili.
Akisoma wasifu wa marehemu katika ibada ya kumuaga Mzee Raphael Augustino Kubaga iliyofanyika katika Kanisa la Anglican St. Alban’s Cathedral lililopo Posta mpya Jijini Dar es salaam, Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji Dorah Luoga alisema Mzee Augustino Kubaga alizaliwa tarehe 24 Oktoba 1935 katika Kijiji cha Kiva Kata ya Kideleko Wilayani Handeni Mkoani Tanga.
Alisoma Shule ya Msingi St. Paul’s iliyopo Kata ya Kideleko Wilayani Handeni Mkoani Tanga na mwaka 1941 na baadae akajiunga na Middle School ambapo alihitimu mwaka 1949.
Mnamo mwaka 1950 Mzee Raphael Kubaga alijiunga na Shule ya Sekondari ya Minaki iliyopo Wilayani Kisarawe Mkoani Pwani wakati huo ikiitwa St. Andrew’s na kuhitimu mwaka 1956.
Tarehe 03 Machi 1957 marehemu alijiunga na Jeshi la Uhamiaji kipindi hicho ikiwa ni Idara ya Uhamiaji chini ya Uongozi wa Ukoloni yaani (Tanganyika Immigration Services) kama Junior Switch Board Operator wa simu na baadaye akafanyakazi kama Karani daraja la pili na kuendelea kupanda akiwa cheo na kuwa karani daraja la kwanza hadi kipindi cha uhuru wa Tanganyika, wakati huo kazi zote za ofisi zilikuwa zikifanywa na wazungu ambapo waingereza wakiwa maafisa, wahindi wakiwa makarani na waafrika wakiwa wahudumu wa ofisi (matarish).
Kipindi cha Utumishi wake Mzee Raphael Kubaga alipandishwa cheo kutoka katika kazi ya ukarani na kuwa Afisa Uhamiaji daraja la tatu baada ya kuwepo kwa changamoto ya kudhibiti wageni kwa kutumia wageni hao hao.
Kutokana na utendaji kazi wake mzuri katika nafasi hiyo Serikali ilifanya maboresho ya taratibu za utumishi Serikalini na kuwapandisha cheo Maafisa Uhamiaji daraja la III wawili akiwemo yeye kuwa Afisa Uhamiaji daraja la II
Marehemu alitumika kufundisha wenzake masuala ya kiuhamiaji kutokana na uzoefu wa muda mrefu na bidii yake kazini.
Hata hivyo mzee Kubaga aliendelea kupandishwa vyeo kwa ngazi mbalimbali hadi mwaka 1969 alipoteuliwa kuwa Afisa Uhamiaji Mkuu katika Idara ya Uhamiaji Tanzania ambapo cheo hicho alikitumia mpaka mwaka 1983 alipostaafu.
Marehemu Mzee Kubaga wakati wa uhai wake mwaka 1957 alipata mafunzo ya udhibiti wa mipaka kutoka katika bandari ya dover nchini Uingereza, pia alikuwa ni kati ya maofisa Uhamiaji wa kwanza kupata mafunzo ya Uhamiaji katika chuo cha usalama Moshi hivi sasa kinajulikana kama chuo cha Polisi Moshi (CCP) pia alifanya mafunzo kwa vitendo katika nchi za Japan, Ufaransa, India, China, Korea, Italy Australia na Urusi.
Marehemu Mzee Kubaga alikuwa ni mdau mkubwa wa Michezo ambapo katika safari yake ya michezo amewahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi ikiwemo kuwahi kuwa Mwenyekiti wa Chama cha ridhaa Mkoa wa Dar e s salaam mwaka 1969 hadi 1971, mwaka 1972 hadi mwaka 1982 alikuwa Mwenyekiti wa chama cha riadha Taifa yaani Tanzania Ameteur Athletic Association na mwaka 1977 hadi mwaka 2002 alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Olympic Tanzania yaani TOC na mwaka 1982 hadi 1986 alikuwa mlezi wa chama cha riadha cha Taifa yaani TAAA na mwaka 1982 hadi 2002 Makamu wa Rais wa Africa Michezo ya Jumuiya ya Madola, mwaka 1983 hadi 1986 alikuwa mlezi wa chama cha ngumi za ridhaa Taifa yaani TABA na mwaka 1984 hadi 1986 mlezi wa chama cha michezo kwa walemavu Tanzania.
Jeshi la Uhamiaji litamkumbuka kwa mchango wake wakati wa uhai wake alishauri Serikali kuimarisha udhibiti wa wageni hadi eneo la majini, aliwezesha Maafisa kupata mafunzo maalumu ya udhibiti wa majini kwa kutumia boti, alishauri Serikali kuimarisha shughuli za kiuhamiaji na hatimae kufungua vituo mbalimbali vya Uhamiaji ikiwemo Horohoro Mkoani Tanga na Taveta Mkoani Kilimanjaro.
Aidha alianzisha timu mbalimbali za michezo Kama vile ngumi, mpira wa miguu, riadha mpira wa pete, mpira wa kikapu na bendi ya Uhamiaji (Hama hama Jazz) sanjari na hayo yeye mwenyewe alikuwa ni mwana michezo wa kiwango cha juu aliyepata medali nyingi na kuwezesha idara na Taifa kwa ujumla kupata medali nyingi katika michezo ya Olympic hususani ngumi na riadha.
Mnamo tarehe 26 Februari 1963 Mzee Raphael Augustino Kubaga alifunga ndoa na Bi. Lilian Zayumba ambapo walifanikiwa kupata Watoto watano.
Marehemu alikuwa anasumbuliwa na tatizo la moyo figo na mapafu ambapo tarehe 03 Februari, 2022 hali yake ilibadilika na kupatwa degedege umauti ulipomfika.
Akihitimisha wasifu wa marehemu Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji Dorah Luoga alimshukuru mwenyezi Mungu kwa zawadi ya kuwa na Raphael Augustino Kubaga katika Jeshi la Uhamiaji pia alimshukuru Mungu kwa maisha yake hapa duniani na yale yote aliyoyafanya katika kuitumikia Uhamiaji na Taifa kwa ujumla kwa utii, uhodari na weledi wa hali ya juu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni