Visitors

IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA UHAMIAJI HABARI BLOGU KARIBU KWENYE BLOG RASMI YA IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA TUNAKULETEA MATUKIO YANAYOTOKEA KILA SIKU KATIKA IDARA YA UHAMIAJI TAFADHALI TUNAOMBA TUFUATILIE PIA KATIKA MITANDAO YETU YA KIJAMII

27 Februari 2022

JESHI LA UHAMIAJI WILAYA YA NGORONGORO LAZINDUA KAMPENI YA UPANDAJI MITI

Na. Paul Dudui, LOLIONDO, NGORONGORO

Suala la mabadiliko ya tabia ya nchi (Climate change) limekuwa ni changamoto kubwa katika maeneo mbalimbali Duniani kote, ambapo sasa Dunia ina haha kupambana na Mabadiliko haya ambayo yameathiri kwa kiwango kikubwa maisha ya watu na viumbe hai wengine, Mabadiliko ya tabia nchi yanaletwa pia na aina ya maisha ya binadamu, ambapo watu wengi hupenda kuharibu mazingira yanayo wazunguka jambo ambalo limesababisha hali mbaya ya hewa ambayo inazidi kuathiri ustawi wa watu na viumbe hai wengine

Kwa upande wa Wilaya ya Ngorongoro na hasa eneo la Loliondo ambalo ni eneo la nyanda za juu ambalo kihistoria lilikuwa sehemu ya baridi kali kutokana na uoto wa asili uliokuwepo wakati huo, hata hivyo hali imebadilika sana na kutokana aina ya maisha ya watu ambayo yameharibu mazingira ya asili na kusababisha Mabadiliko makubwa sana ya tabia ya nchi.

Kutokana na hali hii Jeshi la Uhamiaji Wilaya ya Ngorongoro limeibuka na kampeni kabambe ya kuhamasisha upandaji miti kama hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi na kuhifadhi mazingira ya Mji mdogo wa Loliondo, Kikosi hiki cha Uhamiaji Wilaya ya Ngorongoro kikiongozwa na Afisa Uhamiaji Wilaya ya Ngorongoro Mrakibu Lidya Angumbwike kimeendesha kampeni hiyo kwa kupanda miti katika maeneo mbalimbali ya mji wa Loliondo ambapo hadi kufikia leo ambapo ilikuwa siku rasmi ya kupanda miti Kiwilaya kimeshapanda miti zaidi ya 1200

Katika siku hii ya kupanda miti kiwilaya iliyoasisiwa na Jeshi la Uhamiaji Wilaya ya Ngorongoro, Mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa wilaya ya Ngorongoro, Mheshimiwa Mwalimu Raymond Mangwala, ambaye aliwakilishwa na Kamanda wa Polisi Wilaya ya Ngorongoro SSP Peter Lusesa, kutokana na Mkuu wa wilaya kuwa na majukumu mengine ya kikazi

Hafla ya upandaji miti Kiwilaya, iliyoasisiwa na Jeshi la Uhamiaji Wilaya ya Ngorongoro, ilifanyika katika vya Ofisi za Uhamiaji Wilaya na kuhudhuriwa na; Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya, Viongozi wa Dini, Watumishi wa Halmashauri na taasisi za umma wakiwemo TARURA, NMB, PCCB, Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), Viongozi wa kijamii na wananchi wa mji mdogo wa Loliondo wakiongozwa na Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Mji, Bwana Benezeth Bwikizu.

Akizungumza mara baada ya shughuli ya upandaji miti, Mgeni rasmi amesema kazi ya upandaji miti ni muhimu sana katika kupambana na  mabadiliko ya tabia ya nchi ambayo yanazidi kuathiri Duniani, lakini pia kupanda miti kunaongeza uwezekano wa kutunza mazingira yetu tunayoishi, kwa kuwa miti ni uhai wetu.

Nae Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Loliondo, bwana Benezeth Bwikizu, Akizungumza katika hafla hiyo, amelishukuru Jeshi la Uhamiaji kwa kubuni na kutekeza zoezi hilo ambapo amesema wao kama Mamlaka ya Mji wanalo jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa zoezi hilo linakuwa endelevu, ambapo ametumia nafasi hiyo kuwaelekeza wananchi wote wa mji mdogo wa Loliondo kuhakikisha kila mtu nyumbani kwake na maeneo yake ya kazi ana panda miti mitano kila mwaka ili kutokomeza upepo mkali uliopo katika maeneo ya mji wa Loliondo, Mtendaji huyo ameenda mbali zaidi ambapo alisema wao kama Mamlaka ya Mji mdogo wa Loliondo, itakuja na kampeni yenye ujumbe unaosema "Tokomeza Upepo Wasso, ambapo amesema kampeni hii iliyoasisiwa Uhamiaji, imekuwa kichocheo kikubwa sana.

Nao viongozi wa dini wakiongozwa na Mchungaji Wachira wa GCCT Loliondo, wamesema kampeni hii ni mhimu sana kuungwa mkono na kila mtu ambaye ana hofu ya Mungu kwa kuwa Mungu pia anapenda pia kuwa na mazingira mazuri, Viongozi hao wamesema watawasisitiza waumini wao katika maeneo yao ya Ibada (Kanisani na Misikitini) kuhakikisha kuwa ujumbe huu unafika kwa jamii ili kampeni hii iwe endelevu na itakayoleta matokeo makubwa

Awali akitoa taarifa ya kampeni hiyo Kamanda wa Uhamiaji Wilaya ya Ngorongoro, SI. Lidya Angumbwike amesema kauli mbiu ya Uhamiaji katika shughuli hiyo ni; "Uhamiaji na Maendeleo, Tunza Mazingira kwa Maendeleo ya Vizazi vya Sasa na Vijavyo"

Kwa upande wa wananchi wa Loliondo waliohudhuria katika hafla hiyo wamesema, wao wanalishukuru Jeshi la Uhamiaji Wilaya kwa kuwakumbusha wajibu wao na kwamba kwao kampeni hiyo itakuwa endelevu, aidha wananchi wamempongeza Afisa Uhamiaji Wilaya kwa kupanda miti katika maeneo mbalimbali ya Mji wa Loliondo ambapo wameahidi kuwa miti iyopandwa watailinda ili iweze kusitawi na kukua.

Mwandishi wa Makala hii naye anatumia makala hii kulipongeza Jeshi la Uhamiaji Wilaya ya Ngorongoro kwa namna ambavyo limejitikita katika kutoa elimu ya Uraia na Mazingira, kimsingi Uhamiaji Wilaya ya Ngorongoro pamoja na kufanya shughuli zao katika mazingira magumu lakini bado wamekuwa wabunifu katika upelekaji ujumbe kwa umma.

"Tunza Mazingira yakutunze"

HABARI PICHA NA MATUKIO

Afisa Uhamiaji Wilaya ya Ngorongoro Mrakibu Lidya Angumbwike akipanda mti

Maafisa na Askari wa Uhamiaji Ngorongoro wakipanda miti

Baadhi ya viongozi na wananchi Wilayani Ngorongoro walioshiriki zoezi la upandaji miti


Maoni 1 :