Visitors

IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA UHAMIAJI HABARI BLOGU KARIBU KWENYE BLOG RASMI YA IDARA YA UHAMIAJI TANZANIA TUNAKULETEA MATUKIO YANAYOTOKEA KILA SIKU KATIKA IDARA YA UHAMIAJI TAFADHALI TUNAOMBA TUFUATILIE PIA KATIKA MITANDAO YETU YA KIJAMII

16 Februari 2022

Naibu Waziri Mhe. Jumanne Sagini Aipongeza Uhamiaji kwa Utendaji Kazi Uliotukuka.

 Na. Konstebo Amani Mbwaga, Dodoma

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Jumanne Sagini (Mb) jana tarehe 15 Februari 2022 amefanya ziara ya kikazi ya kujitambulisha katika ofisi ya uhamiaji makao makuu Dodoma.

Alipowasili alipokelewa na mwenyeji wake Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Nchini Dkt. Anna Makakala na baadae kusaini kitabu cha wageni na kisha kupata taarifa fupi ya utendaji kazi.

Akiongea na Maofisa, Askari na Watumishi raia wa Uhamiaji Waziri Sagini alisema amefanya ziara hiyo ikiwa ni mara ya kwanza tangu kuteuliwa kwake katika nafasi hiyo ya Naibu Waziri sanjari na kujitambulisha na kufahamiana zaidi.

Mhe. Sagini amelipongeza Jeshi la Uhamiaji kwa utendaji kazi uliotukuka sanjari na kushiriki kikamilifu kwa mara ya kwanza katika Gwaride la Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 60 ya Uhuru na lile la Maadhimisho ya Miaka 58 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar jambo ambalo limeleta sifa kubwa kwa Uhamiaji, Wizara na Taifa kwa ujumla.

“Uhamiaji mnafanya kazi nzuri sana, nimewaambia viongozi wenu na nisiposema mbele yenu nitakuwa siwatendei haki, niwaombe muendelee na uzalendo huo wa kutimiza majukumu yenu kwa utii, uhodari na weledi wa hali ya juu” alisema Mhe. Sagini

Aidha amewataka kuendeleza upendo, mshikamano, uwajibikaji na kukataa rushwa kama ilivyo katika kauli mbiu ya Uhamiaji, zaidi Mhe. Sagini ameahidi kufanya kazi kwa bidii na kushirikiana na Jeshi la Uhamiaji ili liweze kutekeleza jukumu lake la msingi la kulinda usalama wa nchi kwa kudhibiti uingiaji, ukaaji na utokaji wa raia na wageni kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizopo.

Akitoa taarifa ya utendaji kazi ya Jeshi la Uhamiaji Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Nchini (CGI) Dkt. Anna Makakala alianza kwa kumpongeza Mhe. Naibu Waziri kwa kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

CGI Dkt. Makakala alieleza kwamba Jeshi la Uhamiaji ni chombo cha ulinzi na usalama chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, ambapo tarehe 11 Oktoba, 2021 Idara ya Uhamiaji ilitangazwa rasmi kuwa Jeshi kupitia gazeti la Serikali Namba 41 toleo la 102 kufuatia mabadiliko madogo ya sheria yaliyofanywa na bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi Septemba, 2021.

Hivyo kufuatia mabadiliko hayo masuala yote ya kiutawala yataendeshwa kwa kufuata sheria, kanuni na, miongozo ya Kijeshi ikiwemo ajira upandishwaji vyeo, maslahi ya maofisa na askari pamoja na masuala ya kinidhamu.

“Sambamba na haya tayari Jeshi limeanza utekelezaji wa majukumu yake ya kijeshi kwa kushiriki na vikosi vingine kuingiza gadi katika sherehe za Miaka 60 ya Uhuru zilizofanyika tarehe 9 Disemba 2021na pia tumeshiriki katika sherehe za Miaka 58 ya Mapinduzi Zanzibar Jeshi letu la Uhamiaji linaahidi kuendelea kushiriki katika sherehe zote za kitaifa” alisema Dkt. Makakala

Kwa kipindi cha hivi karibuni Jeshi la Uhamiaji limepata mafanikio katika maeneo mbalimbali ikiwemo kufanikisha marekebisho ya sheria ya Uhamiaji ya mwaka 2015 ambayo yemepelekea idara kuanza kujiendesha katika mfumo wa kijeshi kama ilivyo kwa vyombo vingine vya ulinzi na usalama vilivyo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Mafanikio mengine ni kuanzishwa kwa kambi mpya ya Mafunzo iliyopo katika eneo la Bomakichakamiba Wilayani Mkinga Mkoani Tanga, kupata kibali cha kuajiri askari wapya 820, kuendelea na ujenzi wa ofisi ya Makao Makuu ya Uhamiaji Dodoma, utekelezaji wa mradi wa Uhamiaji Mtandao (e-immigration), Kushiriki katika Ulinzi wa Amani kwenye nchi mbalimbali zenye migogoro ambapo kwa sasa baadhi ya maofisa na askari wa Uhamiaji wako nchini Lebanoni.

Jeshi la Uhamiaji nchini linaipongeza serikali ya awamu ya sita chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe.Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuwezesha mahitaji mbalimbali, Aidha Jehi hili linaahidi kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria, kanuni, miongozo na Taratibu zilizopo katika kuimarisha ulinzi na usalama kwa kudhibiti uingiaji na utokaji wa raia na wageni hapa nchini.

HABARI PICHA NA MATUKIO

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Jumanne Sagini (Mb) akikaribishwa na Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala ofsini kwake jana tarehe 15 Februari 2022 wakati alipofanya ziara ya kikazi ya kujitambulisha katika ofisi ya Uhamiaji Makao Makuu Dodoma.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Jumanne Sagini (Mb) akisaini kitabu cha wageni jana tarehe 15 Februari 2022 wakati alipofanya ziara ya kikazi ya kujitambulisha katika ofisi ya Uhamiaji Makao Makuu Dodoma.
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala (aliyesimama) akitoa taarifa fupi kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Jumanne Sagini jana tarehe 15 Februari 2022 wakati alipofanya ziara ya kikazi ya kujitambulisha katika ofisi ya Uhamiaji Makao Makuu Dodoma.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Jumanne Sagini (Mb) akiongea na Maofisa na Askari (Hawapo Pichani) jana tarehe 15 Februari 2022 wakati alipofanya ziara ya kikazi ya kujitambulisha katika ofisi ya Uhamiaji Makao Makuu Dodoma.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Jumanne Sagini (Mb) (Katikati) akiwa katika Picha ya Pamoja na Makamishna, Wakuu wa Vitengo na Afisa Uhamiaji Mkoa, Kulia kwake ni Kamishna Jenerali Dkt. Anna Makakala jana tarehe 15 Februari 2022 wakati alipofanya ziara ya kikazi ya kujitambulisha katika ofisi ya Uhamiaji Makao Makuu Dodoma.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Jumanne Sagini (Mb) (Katikati) akiwa katika Picha ya Pamoja na Makamishna(Waliokaa), Warakibu na Warakibu Wasaidizi wa Uhamiaji, Kulia kwake ni Kamishna Jenerali Dkt. Anna Makakala jana tarehe 15 Februari 2022 wakati alipofanya ziara ya kikazi ya kujitambulisha katika ofisi ya Uhamiaji Makao Makuu Dodoma.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Jumanne Sagini (Mb) (Katikati) akiwa katika Picha ya Pamoja na Makamishna (Waliokaa), Wakaguzi na Wakaguzi Wasaidizi wa Uhamiaji, Kulia kwake ni Kamishna Jenerali Dkt. Anna Makakala jana tarehe 15 Februari 2022 wakati alipofanya ziara ya kikazi ya kujitambulisha katika ofisi ya Uhamiaji Makao Makuu Dodoma.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Jumanne Sagini (Mb) (Katikati) akiwa katika Picha ya Pamoja na Makamishna(Waliokaa), Askari wa Uhamiaji, Kulia kwake ni Kamishna Jenerali Dkt. Anna Makakala jana tarehe 15 Februari 2022 wakati alipofanya ziara ya kikazi ya kujitambulisha katika ofisi ya Uhamiaji Makao Makuu Dodoma.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Jumanne Sagini (Mb) (Katikati) akiwa katika Picha ya Pamoja na Makamishna(Waliokaa), Watumishi Raia wa Uhamiaji, Kulia kwake ni Kamishna Jenerali Dkt. Anna Makakala jana tarehe 15 Februari 2022 wakati alipofanya ziara ya kikazi ya kujitambulisha katika ofisi ya Uhamiaji Makao Makuu Dodoma.
















(Picha zote na Konstebo Amani Mbwaga)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni