Na. A/Insp Amani Mbwaga, Dodoma.
Mamia ya Maafisa, Askari Watumishi wa Umma na Wananchi wamejitokeza leo tarehe 28 Februari 2025 Chidachi Jijini Dodoma kuaga Mwili wa Marehemu Mrakibu Mwandamizi wa Uhamiaji (SSI)Amon Oscar Mogha aliyefariki ghafla jioni ya tarehe 25 Februari 2025 njiani alipokuwa anatoka mazoezini Jijini Dodoma.
Naibu Kamishna wa Uhamiaji DCI Julieth Sagamiko, Kwa niaba ya Kamisha Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala aliwaongoza mamia ya Watu Jijini Dodoma wakiwemo Maafisa, Askari, Watumishi wa Umma na Wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Dodoma na Tanzania kwa jumla kuuwaga Mwili wa marehemu.
Akitoa salamu za rambi rambi DCI Sagamiko amesema Marehemu SSI Mogha amefariki katika kipindi ambacho Idara ya Uhamiaji bado ilikuwa inahitaji mchango wake kwa kiasi kikubwa katika kutekeleza majukumu yake.
Marehemu SSI Amon Mogha alizaliwa tarehe 03 Septemba 1979 Tukuyu, Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya na kusoma shule na vyuo vikuu mbalimbali ndani na nje ya nchi, mpaka anaajiriwa na Idara ya Uhamiaji Mwaka 2007.
Akiwa kazini baaada ya kuajiriwa marehemu alijiendeleza kielimu ambapo mwaka 2010 alijiunga na Chuo Kikuu cha Amsterdam nchini Uholanzi na kutunukiwa stashahada ya juu ya "International Migration and Intercultural Relations" sanjari na baadae tena alijiunga na Chuo Kikuu cha Osnabruck nchini Ujerumani ambapo mwaka 2012 alitunikiwa Shahada ya Uzamili ya "International Migration and Intercultural Relations"
Marehemu akiwa kazini aliteuliwa katika nafasi mbalimbali na kupandishwa vyeo mbalimbali, ambapo mpaka umauti unamfika alikuwa na cheo cha Mrakibu Mwandamizi wa Uhamiaji huku akihudumu kama Afisa Utumishi Uhamiaji Makao Makuu Dodoma, aidha kabla ya kutumikia katika kitengo cha Utumishi alikuwa akihudumu katika kitengo cha Hati za Ukaazi Uhamiaji Makao Makuu Dodoma.
Marehemu ameacha watoto na mwili wake umesafirishwa leo majira ya saa tisa alasiri kuelekea Tukuyu Mbeya kwa ajili ya Mazishi, Tunamuomba Mwenyezi Mungu ailaze Roho ya Marehemu Mahali Pema Peponi Ameni.
#UhamiajiUsalamanaMaendeleo
#MjueJiraniYako
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni